Adeladius Makwega-Musoma.
Mei 29, 2026 Mwanakwetu alikuwa miongoni mwa maafisa wa Serikali waliombatana na Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi, ambapo Kiongozi huyu alikwenda kufanya uzinduzi wa redio mpya Mkoani Mara inayofahamika kama GM 97.3 FM Redio ya Musoma Mjini.
Akiwa ziarani Kanali Mtambi alipiga Bismilahi ya ziara yake kwa kuingia studio za redio hii mpya kwanza aliingia ofisi ya utawala kisha, chumba cha uzalishaji vipindi, halafu chumba cha habari na kumalizia studio inayorusha matangazo.
Awali meneja wa redio hii ambaye alikuwa dada mmoja mwembamba, mrefu, mweupe ambaye Mwanakwetu hakulifahamu jina lake, binti huyu alimwambia Mkuu wa Mkoa wa Mara maneno haya:
“Redio yetu tuna vipindi kadhaa ikiwamo magazine ya saa nzima vipindi vya matangazo ya DW Kiswahili huwa tunajiunga kutokea Bonn Ujerumani, hii ni asubuhi, mchana na jioni katika saa 24 za siku DW inasikika kwa saa tatu.”
Muda huu Kanali Mtambi akakaribishwa katika kiti hapa studioni yakazungumzwa mambo mengi ikiwamo ufugaji, kilimo, biashara na ulinzi na usalama huku wananchi wanne walipiga simu na kuuliza maswali ambayo Kanali Mtambi aliyajibu kwa ufasaha mkubwa.
Wakati haya yanaendelea Kanali Mtambi alikuwa akiitaja miziki huku watangazaji hawa wakawa wanaisaka katika benki yao ndani ya kompyuta studioni.
Mtu mmoja studioni akawa anasema kwa sauti ya chini:
“Mkuu wa Mkoa alikuwa mtangazaji? Mbona ametulia katika kipaza sauti? Je tumpokonye bunduki tumpe kipaza?”
Jamaa aliyeongea alikuwa akisema kwa sauti ya chini sana maana hata kama tuliongea studioni kama tungeongea basi msikilizaji huko alipo angesikia maana matangazo yalikuwa live, jamaa waliosikia juu ya kumpoka bunduki na kumpa kipaza wakawa wanacheka lakini kicheko cha kimya kimya.
Upande aliokuwepo Mwanakwetu ulikuwa kule walipo watangazaji na kompyuta yao ilikuwa inaonekana vizuri.
Kanali Mtambi akautaja wimbo mmoja ambao haukuwepo katika benki ya kompyuta hii na mtangazaji anayefahamika kama Patrick Mnubi akafungua YouTube haraka haraka akautafuta wimbo huu na kuupata kisha akaucheza, pale pale YouTube bila Mkuu wa Mkoa Mara kujua kama wimbo huo haukuwepo katika benki ya kompyuta yao.
Kitendo hiki kilimkumbusha Mwanakwetu miaka mingi nyuma namna redio zilivyokuwa zinafanya kazi katika ulimwengu wa analojia hasa pale mtangazaji/mtayarishaji vipindi alivyokuwa anachagua nyimbo ili zichezwe studioni.
“Hapa kwanza zilipokelewa barua za maombi ya nyimbo kupitia sanduku la barua na kisha mtangazaji au mtayarishaji anakwenda maktaba ya santuri anachagua santuri iliyochaguliwa kisha anaingia nayo studioni anasoma barua ya santuri alizozipata kisha fundi mitambo anazicheza nyimbo hizo. Hii ilifanyika katika vipindi mathalani kile cha RTD Chaguo la Msikilizaji hapa ilikuwa kabla ya ujio wa kompyuta. Kompyuta zilipoingia studioni nyimbo nyingi zilihamishiwa kutoka katika santuri na kuwa katika kompyuta kisha wimbo ukichaguliwa fundi mitambo/injinia au DJ anautafuta haraka na kisha unachezwa. TBC wana programu moja ya Japan inaitwa MYRIAD ambayo ina visanduku vingi vyenye nyimbo, viashiria vya vipindi na hata vipindi vya redio na mathalani kisanduku namba 2025 kina wimbo Magreth Dar International, hii namba 2025 inaitwa Cart Number, inawezekana Cart Number 2026 ina kipindi cha afya na huku Cart Number 2027 ina kiashiria cha kipindi cha Zilipendwa. Hapa unaweza kuutafuta wimbo kwa jina lake, jina la mtunzi, jina la bendi au Cart Number kama unaikumbuka.
Wakati kwa redio kama DW Kiswahili kuna intaneti ya ndani ambapo redio hii nyimbo zilizowekwa maktaba ambazo shirika lina mikataba nayo zinapatikana, hivyo basi mtangazaji ni marufuku kucheza wimbo ambao haupo maktaba ili kuepuka shirika kushitakiwa na kulipa fidia nyingi kama utachezwa wimbo ambao hawana mkataba nao.”
Hapa studioni Mei 29, 2026 nyimbo zote alizoagiza Mkuu wa Mkoa Mara zilichezwa bila ya mtu kujua kama zilikuwa jirani au la huku uwepo wa mtandao na kuhama kutoka analojia kwenda digitali kumerahisisha mno kazi ya utangazaji.
Haya msomaji wangu Mwanakwetu alikumbuka tu na akaamua kukusimulia na hili kuweka kumbukumbu ya ziara hii ya Kanali Mtambi hapa GM 97.3 FM Redio Musoma. Huku hapa studioni yalizungumzwa mengi kisha Kanali Mtambi kuelekea katika uzinduzi wa GM 97.3 FM Redio hapa Musoma Mjini.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Tumpokonye Bunduki Tumpe Kipaza Sauti?”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
.gif)
.gif)









Post a Comment