Tanzania Haiwezi Kupingua Udugu na Watu wa Ulaya

 

Adeladius Makwega-MBAGALA.


“Angalia jamaa zako wa CCM, ati wamekata Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu ya Bunge la Ulaya kufanya ziara nchini Tanzania.”

Hii ni Mei 8, 2026, Mwanakwetu alitumiwa ujumbe na ndugu yake mmoja akisema maneno hayo huku akiambatanisha na makala yenye maudhui hayo. Jambo hili likamshitua Mwanakwetu na kuanza kufuatilia kulikoni? Alisaka huku na kule na baadaye alibaini haya:

“Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu ya Bunge la Ulaya (DROI) iliyokuwa imepanga kufanya ziara yake nchini Tanzania, imefutwa baada ya kinachodaiwa kuwa mamlaka za Tanzania kukataa kuidhinisha ziara hiyo. Ujumbe huo ulikusudia kutathmini hali ya haki za binadamu, demokrasia, na utawala wa sheria kufuatia vurugu kubwa zilizohusiana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 katika taifa hili lililo kando ya Bahari ya Hindi. Ziara hii ilikuwa ni ya Wawakilishi kutoka Bunge la Ulaya, shabaha ilikuwa ni kutathmini hali ya ndani Tanzania inavyoendelea, kufuatilia maazimio ya Bunge la Ulaya kusimamia miradi ya haki za binadamu inayofadhiliwa na umoja huo.”

Mwanakwetu alipitia zaidi taarifa hizo mithili ya kwamba alipewa jaribio lenye alama kwenye matokeo yake ya kuhitimu Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara (MBA) ya Chuo Kikuu cha Tumani Iringa mwaka wa 2008, enzi hizo Mwanakwetu akiwa kijana mdogo na mwanachuo hodari. Awali ziara hii iliahirishwa kutoka Februari hadi Mei 2026 ili kutoa muda kwa tume ya uchunguzi ya kadhia ya matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata nchini hapa ambapo tume hiyo iliwasilisha ripoti yake ambayo imepokelewa kwa shingo upande na wananchi wa kawaida.

 

Mwanakwetu alibaini kuwa inadaiwa mamlaka za ndani za Tanzania zilikataa ziara hiyo yote bila kutoa sababu maalum.

“Kwa hakika misheni rasmi za kimataifa, kama vile ile iliyopangwa ya Kamati Ndogo ya Haki za Binadamu ya Bunge la Ulaya na hatua za wataalamu wa Umoja wa Mataifa, hulenga kufuatilia demokrasia, utawala wa sheria na vurugu zinazohusiana na kadhia kadhaa.”

Athari ya maamuzi haya kwa ujumla ni kuongeza shinikizo la kimataifa na kuchochea mageuzi ya sera za ndani, licha ya kuwepo kwa migongano ya kisiasa mara kwa mara na kukataliwa huku kunaonyesha mazingira magumu kwa uangalizi wa kimataifa ambapo awali Umoja wa Ulaya ulichukua misimamo kadhaa dhidi ya Tanzania ambapo:

“Wabunge wa Bunge la Ulaya walipiga kura kusitisha mamilioni ya euro za misaada hadi changamoto za demokrasia na haki za binadamu zitakaposhughulikiwa na wakisisitiza kuwa msaada uliobaki uelekezwe kwa asasi za kiraia, waandishi wa habari, na watetezi wa haki za binadamu badala ya taasisi za serikali.”

Sambamba na haya yote Umoja wa Ulaya uliendelea kusisitiza kuundwa kwa tume huru ya Kiafrika kuchunguza madai ya mauaji, kutoweka kwa watu na kuwekwa kizuizini kwa wanasiasa wa upinzani akiwamo Tundu Lissu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA). Hatua hii ya Tanzania ya kupinga uangalizi wa kimataifa inafanana kama ramli potofu ikiwa sawa na hatua zilizochukuliwa na baadhi ya nchi nyingine duniani ambazo zilizuia au kukataa misheni za haki za binadamu au uchunguzi wa kubainika ukweli mathalani:

“Ethiopia(watu milioni 139) – ilizuia wachunguzi wa kimataifa kufikia eneo la Tigray wakati wa mgogoro, Venezuela(Watu milioni 29) ilikataa wataalamu wa Umoja wa Mataifa na kusitisha shughuli za ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Matifa mjini Caracas, Zimbabwe(Watu milion  17) ilizuia waangalizi wa uchaguzi na waandishi wa habari wa kimataifa mara kadhaa. Iran (Watu milioni 93) imekuwa ikikataa mara kwa mara waangalizi maalum wa Umoja wa Mataifa, Belarus (Watu milioni 9) ilizuia misheni za kimataifa kuchunguza ukandamizaji wa kisiasa. Huku hali mbaya kwa raia hao wanaokaribia milioni 300 ndani ya ardhi ya mataifa haya wakionja joto ya jiwe.”

Pitapita ya Mwanakwetu iliishia hapo na alipoelewa kwa kina hayo yote ndipo akaamua kuyaandika makala haya.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu hakubaliani kabisa na maamuzi haya ya kuikataza kamati ndogo ya Haki ya Binadamu ya Umoja wa Ulaya kuingia Tanzania na kufanya ziara yake ya kikazi maana kamati hii ikiwa ni mawakala wa Bunge la Ulaya ambao ni wawakilishi wa watu wa Ulaya ambapo kwa muda mrefu Watanzania tumenufaidika mno na misaada kadhaa kutoka kwa watu wa Ulaya.

“Nakumbuka wakati nasoma Tambaza Sekondari miaka 1990 gorofa za madarasa juu ya shule hii ya umma ya Tanzania zilipata nyufa hivyo basi madarasa haya yalikuwa yanavuja sana nyakati za mvua na hivyo kusoma ilikuwa vigumu huku vyoo vilikuwa chakavu mno. Shule ilifungwa katika mojawapo ya likizo zake mwaka kisha shule zilipofunguliwa tulikuta juu ya gorofa kumeezekwa vizuri, vyoo vimekarabatiwa na maji yanatoka chooni na hali ya kuvuja kule juu SAMITI ilikoma mara moja. Wanafunzi tulipofuatilia tulibaini kuwa ukarabati huu ulifanywa na DANIDA shirika la misaada kutoka Denmark ambaye ni mshirika mmojawapo wa Umoja wa Ulaya.”

Tanzania haiwezi kusimama kifua mbele na kuwakataa ndugu zetu wa Ulaya.

Kwa mujibu wa takwimu ya misaada na mikopo ambayo Tanzania imepokea kwa robo karne tangu mwaka 2000 hadi 2026 kutoka Umoja wa Ulaya ni karibu Euro Bilioni 3.3 ikiwa kutoka kwa ndugu pekee wa Umoja wa Ulaya na siyo mtu mwingine yoyote.

 

Viongozi wetu wa Tanzania lazima wafahamu kuwa Mjerumani na Mwingereza ni ndugu zetu ambapo wazee wetu walikaa nao wakati wa Ukoloni na hata leo hii masalia yao yapo maeneno mbalimbali ya taifa letu tukiwa tumechanganya nao damu na Ulaya hawakufahamu.

Hata kama kuna katazo lolote dhidi ya Wabunge wa Bunge la Ulaya lazima aliyakataza hilo atoke hadharani, atoe sababu zake ili jamii ipime maana baadhi ya Watanzania wana udugu wa damu na watu wa Umoja wa Ulaya.

 

Huyu aliyewakataza ndugu hao kuingia pengine ataweza kutuambia labda Tanzania imepata ndugu mwingine wa damu tumjue na sasa Tanzania Imepingua Udugu na Watu Ulaya.

“Akitupa majibu tukaridhika tutakubaliana naye na kama hatutaridhika tutamwambia kuwa uamuzi wako huo ni haramu, batili na ufutwe mara moja.”

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Tanzania Haiwezi Kupingua Udugu na Watu wa Ulaya”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments