Adeladius Makwega-Musoma MARA
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evansi Alfred Mtambi, amezipongeza taasisi za dini na madhehebu mbalimbali kwa kujihusisha na shughuli za utoaji huduma za jamii, ikiwamo sekta za afya, elimu, kilimo, ufugaji na misaada mingine ya kibinadamu.
Amesema kwa kufanya hivyo, taasisi hizo zinaisaidia serikali kwa kuipunguzia mzigo wa utoaji huduma kwa wananchi.
“Haya yamekuwa yakifanyika bila kujali dini zetu, rangi zetu wala nasaba zetu. Sisi sote ni Watanzania na sisi sote ni ndugu,” alisema.
Kauli hiyo ilitolewa katika harambee ya maboresho ya miundombinu ya Kanisa la Bikira Maria wa Fatima pamoja na ununuzi wa gari la Parokia ya Songe, iliyofanyika Musoma, mkoani Mara, Mei 31, 2026. Katika hafla hiyo,
Kanali Mtambi alimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba (Mb).
Akiongoza harambee hiyo, Kanali Matambi alisema kuwa yeye, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara pamoja na mchango wa Waziri Mkuu wamechangia jumla ya shilingi milioni 75. Waumini na viongozi wengine walichangia shilingi milioni 40, hivyo kufanya jumla ya michango kufikia shilingi milioni 115.
Akizungumza na hadhara hiyo, Kanali Mtambi aliwaomba viongozi wa dini mkoani Mara kuendelea kukemea vitendo vya ukatili, mila potofu na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
“Taifa lisilo na hofu ya Mungu ni taifa mfu. Viongozi wa dini, tupo pamoja nanyi, na mkiwa na mahitaji yoyote ya msaada mtapatiwa ili Tanzania iendelee kuwa taifa lenye maadili na kumcha Mwenyezi Mungu,” alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa mshikamano miongoni mwa Watanzania kwa kusema:
“Imani, itikadi na nasaba zisiwe sababu ya kutugawa, bali ziwe chachu ya kutuunganisha zaidi.”
Akizungumza kwa niaba ya walei na Baraza la Walei la Parokia hiyo, Padri Wilbert Manembo alimshukuru Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, kwa mchango wake na kusema kuwa parokia itaendelea kuwaombea viongozi wote wa serikali.
Awali, akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mheshimiwa Juma Chikoka, alisema harambee ya Parokia ya Songe imekuwa ya kipekee kutokana na mwitikio mkubwa wa waumini na washiriki wote waliochangia kwa hiari bila malalamiko.
“Mimi, kutoka katika kilindi cha moyo wangu, nasema kuwa leo nimekuwa sehemu ya ujenzi na maboresho ya miundombinu ya parokia hii. Nitaendelea kupita hapa mara kwa mara kukagua maendeleo ya mradi huu,” alisema.
Kabla ya harambee hiyo, Kanali Matambi pamoja na viongozi wengine walishiriki Ibada ya Misa ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Parokia ya Songe.
0717649257






Post a Comment