Adeladius Makwega – Mbagala
Mei 26, 2026, Mwanakwetu aliwasiliana na mhandisi mmoja ambaye alimwuliza,
“Leo kaka una mada gani?”
Kwa kuwa Mwanakwetu alielewa dhamira ya swali hilo, alicheka kidogo. Mhandisi akasisitiza akitaka jibu. Ndipo Mwanakwetu akasema:
“Injinia, unapaswa kutambua kuwa unapokuwa mekoni, umebandika maharage yako na kuchochea kuni vizuri. Juu ya chungu cha maharage umeweka chungu kingine chenye maji. Maharage yanapokuwa yameiva tayari, kuna haja gani ya kuendelea kuchochea kuni? Kazi iliyobaki ni kuipua ile sufuria ya juu yenye maji yaliyochemka, uyaunge kwenye maharage, kisha uandae ugali wako. Ukishakamilisha, kula kwa utulivu maana kazi imekamilika. Hakuna sababu ya kupoteza muda kutafuta kuni au kujichosha kwa moshi usio na tija.”
Baada ya maelezo hayo, mhandisi aliagana na Mwanakwetu na kuondoka zake.
Mwanakwetu naye akaendelea na shughuli zake, akafika sehemu nyingine ambapo alikaribishwa na watu waliokuwapo. Mmoja wao akasema:
“Leo Mwanakwetu kafika kwetu? Bahati iliyoje! Au pengine amekuja kwa sababu Asha amerudi?”
Mwanakwetu akajitetea:
“Jamani, mbona mimi huja hapa mara kwa mara! Huyo Asha alikuwa wapi?”
Mwingine akajibu:
“Asha alikuwa kwenye mkutano wa Waandishi Waendesha Ofisi. Unajua naye ni mdau wa taaluma hiyo.”
Mwanakwetu akashangaa:
“Hilo sikuwa nalijua.”
Waliokuwapo wakacheka, mmoja akasema:
“Usijifanye hujui. Wewe na Asha ni watu wa karibu sana. Labda leo umekuja kujiandaa kwa sherehe ya Idi, maana Waswahili husema: Penye pengo ulimi hupita.”
Kauli hiyo ilizua mjadala mdogo. Mmoja akauliza:
“Jamani, methali hii ina maana gani hasa?”
Hata hivyo, kabla ya mjadala kuendelea, ugeni uliingia na mazungumzo yakakatika. Mwanakwetu akaagana nao na kuondoka. Alipofika sehemu yake tulivu, akaamua kuyaandika mawazo yake kama yalivyomjia.
Tafakari ya Mwanakwetu
Mwanakwetu anasema kuwa matukio haya mawili—la maharage yaliyoiva na lile la methali ya Penye pengo ulimi hupita—yalimpa tafakari kubwa.
Anafafanua kuwa:
“Methali hii ina maana kwamba pale panapokuwa na udhaifu, hata kama ni mdogo, jambo linaweza kupenya na kusababisha athari kubwa bila kutarajiwa. Kama ilivyo kwa ulimi wa binadamu, hupita pale penye pengo, si sehemu iliyofungwa. Vivyo hivyo katika maisha, udhaifu mdogo unaweza kufungua mlango wa matatizo makubwa.”
HitimishoMwanakwetu anauliza:
“Je, makala hii iitwe ‘Maharage Yakishaiva Hakuna Haja ya Kuchochea Kuni’ au ‘Penye Pengo Ulimi Unapita?’Hatimaye, anachagua:‘Penye Pengo Ulimi Unapita’”
Nakutakia siku njema
📧makwadeladius@gmail.com
📞 0717 649 257
.gif)











.gif)
Post a Comment