Nikipewa Talaka Utakuwa Unaleta Pesa ya Matumizi

 


Adeladius Makwega-MBAGALA

Mei 13, 2026 Mwanakwetu alimkumbuka mhadhiri wake wa Chuo Kikuu aliyemfundisha kozi inayoitwa News Writing and Reporting ndani ya Shahada ya Sanaa ya Habari, Profesa Gasper Mpehongwa huku akimfundisha Mwanakwetu namna ya kuandika/kutayarisha makala kwa kutumia picha iwe katika gazeti, redio, runinga na mitandao ya kijamii.

Siku hii Mwanakwetu aliamua kurudi Chuo Kikuu kwa Heshima ya Profesa Mpehongwa akaamua kupiga picha kadhaa huku akitaka kuzitumia picha hizo kutayarisha makala yake moja maridadi.

Katika zoezi la kupiga picha hizo ndani ya Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, picha zilikuwa nzuri sana na kisha mazungumzo ya watumishi wa ofisi hii ya umma na watu wengine wakati picha zinapigwa yalikuwa mazuri zaidi. Mazungumzo haya yakamuacha Mwanakwetu mdomo wazi na pia akiwa njia panda ya namna ya kutayarisha makala yake.

Wakati Mwanakwetu anazihariri picha hizo akawa njia pande je makala yake itumie picha au makala yake itumie mazungumzo ya watumishi wa RS MARA na wegeni wakati picha hizo zinapigwa? Baadaye Mwanakwetu alichagua kuyatumia mazungumzo ya wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na wageni siku hii wakati picha hizo zinapigwa kuyajenga makala yake.

Mwanakwetu akawa anachukua picha moja moja kisha anakumbuka maneno ya hawa watumishi wa umma yalivyokuwa siku hii.

Kwa ujumla hali ilikuwa hivi:

 

Mdau mmoja aliyasema haya:

“Mwanakwetu leo umenikumbuka! Lo salale haya makala yako yatakuwa na nini jamani? Maana nimebakiza siku chache kustaafu”

Mwanakwetu akapiga picha na kuingia chumba kingine, hapa alipiga picha na kuyasikia maneno haya:

“Leo watumishi wa Masijala tumo katika makala ya Mwanakwetu? Nayangoja makala haya kwa hamu ili nimtumie shemeji yako.”

Mwanakwetu kigulu na njia hadi ofisi nyingine, hapa alipigwa na maswali kadhaa:

“Sisi wakaguzi wa ndani hatupaswi kuonekana katika picha zako. Hapa hakuna kupiga picha.”

Hili halikumkatisha tamaa Mwanakwetu, japokuwa hapa hakuweza kuwapiga picha ndugu zake Dkt. Charles Kichere Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Mwanakwetu hakuchoka pita hapa na pita pale iliendelea.

“Ehee Mwanakwetu nipige picha vizuri, nataka picha hii imfikie Waziri wa TAMISEMI Profesa Riziki Shemdoe, natamani aone hapa RS Mara tunavyochapa kazi.”

Mwanakwetu kimoyomoyo akawa anacheka lakini hana la kusema wala la kutamka hapa yu kazini, huku anatoka ofisi moja hadi nyingine.

Pita pita hii njiani anakutana na wananchi wakiingia na kutoka kumuona Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi, miongoni mwao ni kikundi cha wachimbaji madini wadogo wadogo Cha Nyamlicha kutoka Wilayani Rorya ambapo walifiika kuomba ushauri wa soko la madini ya chuma wakiongozwa na  Mugoka Nyabanga

 

Mbele kidogo ya hwa jamaa Mwanakwetu akakutana na mama mmoja kapendeza kweli:

“Baba kwema? Hivi Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara ndugu Gerald Musabila Kusaya ipo wapi?”

Mwanakwetu alimuelekeza mama huyu ofisi ya kiongozi huyu na kisha safari za Mwanakwetu shuka na panda ngazi akipiga picha ikiendelea.

“Mwanakwetu nakwambia mimi sitaki kupigwa picha maana shemeji yako anawivu, hivi akiiona picha hii nimepiga na mtu atakuwa na maswali mengi, nikipewa talaka nitakutwisha jukumu la kuniletea pesa ya matumizi.”

Ilani yenye maneno haya ilimchekesha mno Mwanakwetu, ilani ya kubeba mzigo wa kupeleka pesa ya matumizi, hapa Mwanakwetu akawa hoi bini taabani.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu ameyatayarisha makala haya kama mojawapo ya makala mafunzo kwa wanachuo wanaosoma taaluma ya habari wakipewa mbinu ya namna nyingine wanayoweza kutumia picha na kutayarisha makala hasa kwa kutumia maneno ya wale waliyokutwa njiani wakati picha zinapigwa kama mojawapo ya somo kwa wanahabari vijana.

 

Pili makala haya ni salaam kwa Waziri wa TAMISEMI Profesa Riziki Shemdoe kutoka kwa watumishi wake hapa Mkoani Mara kwa namna wanavyochapa kazi na wapo kazini wakitoa huduma kwa jamii ya Watanzania wakifanya kazi kwa amani na bashasha tele.Pia Mwanakwetu ana hakika wanakikundi cha wachimbaji madini walifika kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara wamekutana nayo na ombi lao linafanyiwa kazi.

Mwisho Mwanakwetu anatuma ujumbe kwa wale wenye wivu jamani punguzeni wivu maana watu wanaogopa hata kupiga picha wakiwa kazi.

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Nikipewa Talaka Utakuwa Unaleta Pesa ya Matumizi.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257





















 





 

 

0/Post a Comment/Comments