Nifike Kule Alipo Bibi Harusi

Adeladius Makwega-MUKENDO

Jioni ya Mei 22, 2026 Mwanakwetu alikuwa safarini akitoka Wilayani Tarime kuelekea Musoma Mjini ambapo ni umbali wa karibu KM 83 kwa gari ndogo , mwendo wa dakika 50 mpaka 60 ndani ya Mkoa wa Mara. Safarini Mwanakwetu alikuwa anasinzia na kuamka huku dereva wa gari hii akiendesha na akipiga soga na mtu mwingine aliyekuwa katika safari hii.

Walipofika pale Mto Mara unapokatiza kuelekea Ziwa Victoria Mwanakwetu alishituka usingizini baada ya ndugu mmoja kumpigia simu. Mwanakwetu aliogea na ndugu huyu kisha kuitazama simu yake katika ukurasa mmoja wa mitandao ya kijamii.

Hapo hapo alibaini kuwa ndugu mmoja anayefahamika kwa jina la mtandaoni CNM Mercy alitembelea ukurasa wa Adeladius Makwega ambaye hakuwa rafiki yake hivyo basi Mwanakwetu aliukagua ukurasa wa huyu ndugu na ndipo alikutana na wimbo mmoja wa Kikirsto wenye jina Nimekubali Bwana Utawale Moyo wangu:

 

“Nimekubali Bwana. Nimekubali Bwana, Nimekubali Bwana Utawale Moyo wangu. Nimekubali Bwana, Nimekubali Bwana, Nimekubali Bwana Utawale Moyo, Nimekubali Bwana Utawala Moyo wangu…”

Ndugu hawa wanaoimba wimbo huu katika ukanda mfupi walikuwa Wakristo wakiwa katika chumba kimoja kidogo kilichojaa waamini, kikiwa na ubao mbele yao, mithili ya darasa huku waamini wakikaa katika mabechi ya kawaida kabisa yasiyopigwa randa wala polishi, ukuta ukuwa hauna palasta , tofali zikionekana huku wakimba kwa nguvu, moyo wao wote wakimtukuza Yesu Kristo.

 

Jambo lilimkumbuka Mwanakwete Ukrsto wa miaka 1980- 1990 nchini Tanzania ambapo baadhi ya madhehebu ya Kikrsto yalitumia vyumba vya shule za msingi kusali siku za jumapili.Video hii ilimvutia mno Mwanakwetu na alipokagua vizuri alibaini kuwa huyu ndugu Cnm Mercy wimbo huu aliunakili kutoka kwa ndugu yake mwingine mwenye jina la Emmah Bonaneri.Hapa hapa Mwanakwetu aliutembelea ukarasa wa Emmah Bonaneri na hapohapo alikutana nyimbo kadhaa za dini ya Kikristo lakini wimbo uliomvutia kwa mara ya pili ulikuwa na jina Ndipo Yesu Akaja:

“Ndipo Yesu Akaja Kwao, Ndipo Yesu Akaja Kuwaokoa, Ndipo Yesu Akaja, Ndipo Yesu Akaja.

Ndipo Yesu Akaja Kwao, Ndipo Yesu Akaja Kuwaokoa, Ndipo Yesu Akaja Ndipo Yesu Akaja…”

Mazingira yaliyoimbwa wimbo huu yalikuwa yale yale, huku waamini wakiwa wamechangamka mno na wakiimba kwa moyo wote.Mwanakwetu aliusikiliza wimbo huu huku akisoma maoni ya waliyoutazama ambapo ndugu Tresor Mwaka aliyasema maneno haya:

“Mungu wetu awabariki sana waimbaji hawa.”

Huku maoni mengi yakiwapongeza Wakristo hawa.

Mwanakwetu aliendelea kuukagua ukurasa wa Emmah Bonaneri na mbele kidogo akakutana na wimbo mwingine ambao ulitambulisha ukiitwa Amenitendea Mema Huyu Yesu:

“Amenitendea Mema Huyu Yesu, Amenitendea Mema Tena Sana, Amenitendea Mema Huyu Yesu , Amenitendea Mema Tena Sana, Amenitendea Mema Huyu Yesu, Amenitendea Mema Tena Sana...”

Hapa muktadha ulikuwa ule ule waamini wakiimba kwa moyo wote huku makofi, miruzi vigelegele na shangwe kubwa zikiusindikiza wimbo huu na kumvutia yule anayeutazama. Hapa Mwanakwetu akiona kuwa haya yakiwa siyo mazingira ya makanisa makubwa kama vile lile la Mtakatifu Albano, Kanisa la Azania Front au Kanisa la Mtakatifu Yosefu pale posta Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, bali haya ni mazingira ya kijijini huku kukiwa na vifaa vya kawaida mno, waamini wamevaa kawaida wakimsifu Bwana.

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yu safarini anaelekea Musoma Mjini akitokea Tarime ambapo walikwenda katika kazi za habari na wenzake wawili na sasa walikuwa Bweri Stendi Kuu ya Mabasi ya mkoa wa Mara ambapo wakati hii ilikuwa inajengwa. Hapa Mwanakwetu akiwa na simu yake akakutana na wimbo mwingine uliokuwa na jina Wakristo Halisi Walio na Ujumbe:

“Wakristo Halisi Walio na Neno , Wakristo Walio na Ujumbe, Wakristo Halisi Walio na Neno , Wakristo Walio na Ujumbe…”

Hapa Mwanakwetu alikuwa amevutwa na hisia kubwa na nyimbo hizi na hili likafanya hata kumtafakari Yesu Kristo, huku Mwanakwetu akikumbuka dhambi zake kadhaa ambazo anatakiwa kutubu. Huku dereva wa gari hili na yule mtu mwingine hawafahamu kile kinachotafakariwa na Mwanakwetu akilini mwake. Mara Mwanakwetu alifika Musoma mjini na dereva akasema Mwanakwetu twende nikupeleke hadi unapoishi, kweli Mwanakwetu alifikiswa hadi anapoishi na haya yalikuwa majira ya jioni sana. Akiwa kwake hakuiweka kando simu yake bali aliendelea kuikagua na ndipo akakutana na wimbo mwingine uliyokuwa na maneno haya:

“E Bwana Uniongoze, Nikifike Ng’ambo ya Pili, Alipo Bibi Harusi na Mimi Niwe  Mmoja Wao, Nifike Ng’ambo ya Pili Alipo Bibi Harusi na Mimi Niwe Mmoja Wao…”

Sasa Mwanakwetu yu kwake usiku uliingia na baadaye Mwanakwetu aliuchapa usingizi wenye uchovu wa safari na kulipokucha yaani Mei 23, 2026 ndipo akaamua kuyatayarisha makala haya.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika nyimbo zote tano yaani: Nimekubali Baba, Ndipo Yesu Akaja, Amenitendea Mema Huyu Bwana , Wakristo Halisi na Ee Bwana Uniongoze zimeimbwa vizuri katika mazingira halisi ya Wakristo wa kawaida ambalo hili ni jambo zuri maana nyimbo zinazoimbwa na makanisa ya kawaida ni vigumu kurekodiwa kutokana na gharama kubwa na uwezo mdogo wa makanisa ya shirikani, parokiani mashinani na hasa za vijijini , wakati huku pia wapo Wakristo wenge vipaji vya hali ya juu.Mara nyingi matumizi ya Nyimbo ni aina mojawapo muhimu ya mbinu ya kufundishia somo lolote liwe la dini au elimu ya duniani na mbinu hii inasadia sana yule anayejifunza kukumbuka haraka.

 

Wanataaluma wa Ualimu wanasema haya:

“Kufundisha kwa kutumia nyimbo ni mbinu yenye ufanisi mkubwa, inayovutia na inayohusisha hisia nyingi na kuongeza uwezo wa kukumbuka. Melodia zinazojirudia na kuvutia zinashauriwa kutumika, zikipunguza wasiwasi wa wanafunzi na kuunda mazingira mazuri ya darasani au pahala wimbo unapotumika.

Watoto Wadogo mara nyingi tumia nyimbo zinazojirudia, zenye vitendo na rahisi kueleweka ili kuwafanya washiriki kwa mwili na vitendo.

Hata kwa Vijana pia tumia nyimbo za kisasa za kuwaruhusu kupendekeza nyimbo maarufu au zinazovuma huongeza ushiriki. Hata kwa Watu Wazima pia tumia nyimbo zenye hadithi nzito na zinazofahamika na wengi.”

Kwa hakika yapo mazingria ya makanisa fulani wimbo unaimbwa haufahamika na wengi na hilo ni kosa maana linapunguza ushiriki wa moja kwa moja wa muumini katika ibada hiyo inapendeza nyimbo kuimbwa na kila mmoja. Mwanakwetu anaamini kuwa hata Bwana Yesu anakuwa na furaha kama wimbo unaimbwa na wote na siyo watu wachache au wanakwaya peke yao. Ukitazama nyimbo hizi tano zote zinaimbwa na kila mmoja tangu viongozi mbele, watu wazima na watoto.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Nifike Kule Alipo Bibi Harusi.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257
















0/Post a Comment/Comments