.gif)
Adeladius Makwega - MBAGALA
“Tukio la almasi nyeusi au almasi ghafi linalomhusu mrembo na mwanamitindo kutoka Uingereza, Naomi Campbell, linahusiana na kashfa ya almasi za damu (blood diamonds) zilizohusishwa na aliyekuwa Rais wa Liberia, Charles Taylor, ambapo mnamo mwaka 1997, Naomi Campbell alihudhuria chakula cha jioni cha hisani nchini Afrika Kusini kilichoandaliwa na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Nelson Mandela. Usiku huo, inadaiwa kuwa mrembo Naomi Campbell alipewa vipande vya almasi ghafi kama zawadi na wanaume wawili waliotumwa na Charles Taylor. Akiwa mahakamani mwaka 2010, Naomi alilazimika kutoa ushahidi jijini The Hague katika kesi iliyokuwa ikimkabili Charles Taylor, ambapo mrembo huyu alieleza mahakamani kuwa ni kweli aliamshwa usiku wa manane na kukabidhiwa mfuko wenye mawe hayo. Alipoupokea, kisha aliuchapa usingizi, na kulipokucha alikagua na kubaini ni mawe madogo madogo, madongo yanayong’aa ambayo yalikuwa machafu. Kwa kuwa hakujua ni nani hasa aliyempatia, kulipokucha ndipo alibaini kuwa alipewa na Charles Taylor, na baadaye aliamua kuyakabidhi kwa shirika la watoto la Nelson Mandela (Nelson Mandela Children's Fund) ili yatumike kwa hisani.”
Hapa msomaji wangu unaweza ukajiuliza: ilikuwaje Charles Taylor amkabidhi Naomi Campbell mfuko huo wa madini ya almasi saa nane ya usiku?
“Ushahidi kutoka kwa aliyekuwa wakili wa Naomi ulieleza kuwa wakati wa chakula hicho cha jioni walionekana Charles na Naomi wakiwa na ukaribu wa kimapenzi, na walionekana wakitaniana. Wakati wa hafla hiyo ikiendelea, ndipo Charles Taylor aliahidi kumpa mwanamitindo huyo zawadi, na baadaye usiku huo huo wa manane, watu wawili walifika katika chumba cha Naomi Campbell na kumkabidhi mfuko wenye mawe hayo yasiyochongwa.”
Msomaji wangu tambua kuwa katika mapenzi kila mmoja huonga kulingana na uwezo wake, mwingine anatoa baiskeli, mwingine pikipiki, mwingine gari , mwingine nyumba na mwingine mzigo wa madini, kila mmoja hujikuna pale anapoweza.
Kupitia mashtaka yaliyofunguliwa katika Mahakama Maalum ya Sierra Leone (SCSL), ilielezwa kuwa Taylor alikuwa akitumia almasi hizo zilizochimbwa kwa mateso kufadhili vita vya wenyewe kwa wenyewe, na kitendo chake cha kumpa Naomi Campbell zawadi hiyo kilionyesha utajiri wake, kushiriki kwake kwenye mambo ya Sierra Leone na kusisitiza ushawishi wake.
“Japokuwa Charles Taylor na Naomi Campbell hakuna ushahidi wa wao kuwa na mahusiano ya kimapenzi, lakini ujirani wa Charles Taylor na Naomi ulikuwa pia na nia ya kujenga ushawishi kimataifa. Hali ya kuwa jirani na mwanamitindo huyo wa kimataifa ilikuwa na maana kubwa kwa taifa la Liberia, ambalo lilikuwa limetoka katika migogoro na uchaguzi wake mkuu miezi michache nyuma.”
Swali muhimu la kujiuliza, je, hali ya Liberia ilikuwaje wakati huo?
“Mwaka 1997 ulikuwa
muhimu sana katika siasa za taifa la Liberia kwa sababu uliashiria mpito kutoka
vita vya wenyewe kwa wenyewe kwenda utawala wa kiraia.
Liberia ilikuwa imetoka kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe (1989–1996)
vilivyosababisha vifo vingi na uharibifu mkubwa wa nchi. Makubaliano ya amani,
hasa yale ya Abuja, yaliweka msingi wa uchaguzi wa mwaka 1997. Vikosi vya
kikanda (ECOWAS/ECOMOG) na Umoja wa Mataifa vilisimamia mchakato wa kusitisha
mapigano na uchaguzi.
Uchaguzi wa rais na bunge ulifanyika Julai 19, 1997. Wagombea wakuu walikuwa:
Charles Taylor (kiongozi wa zamani wa waasi) na Ellen Johnson Sirleaf (mpinzani
wake mkuu). Charles Taylor alishinda kwa asilimia 75 ya kura. Chama chake
(National Patriotic Party) pia kilipata wingi mkubwa bungeni. Aliapishwa kuwa
rais Agosti 1997. Ingawa uchaguzi ulionekana kuwa huru kwa kiasi fulani,
kulikuwa na hofu na vitisho: wananchi wengi waliamini kuwa kama Taylor
angeshindwa, vita vingerejea. Miundombinu ilikuwa imeharibiwa na vita, na
kiwango cha watu kutokujua kusoma na kuandika kilikuwa juu, jambo lililofanya
mchakato wa kisiasa kuwa mgumu. Mwaka 1997 uliashiria mwisho rasmi wa vita ya
kwanza ya wenyewe kwa wenyewe na mwanzo wa serikali mpya ya kiraia chini ya
Taylor. Hata hivyo, nchi ilibaki na changamoto kubwa: uharibifu wa uchumi,
wakimbizi wengi na migawanyiko ya kisiasa na kikabila.”
Kwa hakika, Charles Taylor akiwa katika chakula cha jioni nchini Afrika ya Kusini Septemba 26, 1997, ilikuwa ni siku muhimu mno kwake kuionesha dunia kuwa Liberia imekuwa taifa jipya, na karata ya kuwa jirani na Naomi Campbell ilikuwa muhimu. Tatizo lilikuwa ni zawadi aliyoitoa na namna mzigo huo ulivyopatikana, ukibebwa na mwenendo mbaya wa maisha ya Charles Taylor. Katika haya yote, Mwanakwetu anakumbuka msemo huu:
“Wafugaji wanasema ukiwa na kundi kubwa la mifugo, hata kama utalipitisha katika josho kila mara, kumbuka mifugo hiyo haiwezi kukosa kupe.”
Kwa nini Mwanakwetu amekumbuka tukio hili la Naomi Campbell na almasi chafu?
Taifa la Tanzania, kwa miezi ya mwanzoni na katikati ya mwaka wa 2026, limepokea ugeni wa watu maarufu katika sekta ya michezo, akiwamo Didier Drogba na Rio Ferdinand, ambao ni wachezaji wa soka wa zamani duniani. Miongoni mwa mambo kadhaa, wanasoka hawa waliwahi kuwika katika mchezo wa mpira wa miguu, waliingia hadi bungeni na kutambulishwa na kupiga picha na viongozi.
Ugeni huo umekuwa ukimpa tafakari kubwa Mwanakwetu, na miongoni mwa mambo yaliomjia akilini ni tukio la Naomi Campbell na almasi chafu. Mwanakwetu anaamini kuwa wanaowaleta wanasoka hao shabaha yao ni kujenga jina zuri la Tanzania kimataifa. Hili hana shida nalo, maana hata Februari 17, 1992, akiwa mwanafunzi wa kidato cha pili pale Tambaza Sekondari, Tanzania ilimpokea mwanamuziki Michael Jackson. Ugeni huo ulipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam na Ahmad Hassan Diria, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, na baadaye Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, alikutana naye Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam kabla ya kurejea Marekani.
Kwa wale waliokuwepo, watakumbuka maneno mengi yaliyosemwa mitaani dhidi ya Michael Jackson:
“Jamaa alifika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam akasema Tanzania inanuka. Akakataa hata kwenda mbuga ya Ngorongoro, na hivyo akaamua kukaa Kilimanjaro Hotel kidogo kisha kurudi zake Marekani.”
Huku kukiwa na hoja kuwa Michael Jackson alitaka kwenda Ngorongoro kwa ndege yake binafsi akiwa na kikosi chake cha watu karibu 80, lakini wakati huo mbuga hiyo haikuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa kama hiyo.
Mwanakwetu ana hakika kuwa kama wakati ule kungekuwa na mitandao ya kijamii kama mwaka wa 2026, Michael Jackson angepokea lawama nyingi kutoka kwa Watanzania. Ujio wake haukuwa bure, kwani Tanzania ya mwaka 1992 ilikuwa katika kipindi cha mabadiliko, ikiwa ni pamoja na kuanguka kwa Ujamaa wa Sovieti, Mgogoro wa OIC na kuanza kwa harakati za vyama vingi.
Kwa hakika, Mwanakwetu anaamini kuwa changamoto ni moja: Tanzania haiwezi kutatua matatizo yake ya ndani kwa kuwaleta wageni. Matatizo ya ndani, kama yapo, yanahitaji viongozi kuyakiri hadharani, kuomba radhi na kuwasikiliza wananchi ili jamii yenyewe iamue mustakabali wake.
Kinyume chake, yote haya yatakuwa sawa na kile cha Naomi Campbell na Charles Taylor: unapiga naye picha kuonesha jina zuri la Liberia, lakini usiku unampelekea almasi chafu.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Ng’ombe wa zizini hakosi kupe.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257















.gif)
.gif)
Post a Comment