Musoma Waongeza Redio Nyingine ya Kijamii

 




Adeladius Makwega – Musoma

Wilaya ya Musoma, mkoani Mara, imeongeza redio nyingine ya kijamii ambayo inarusha matangazo yake kupitia 97.3 FM, iliyopachikwa jina la GM.

Katika utafiti wa Mwanakwetu hapa Musoma Mjini, redio hii ipo mtaa wa Nyakato, ambapo jina la GM linamaanisha kumbukumbu ya Ghati (Ghati Memorial).

Mwanakwetu hakuweza kufahamu sababu ya jina hilo kuwa hivyo, lakini ameshuhudia mitaani Musoma redio hii ikisikilizwa.

“Mimi ni Patrick Mnubi… kutoka hapa Musoma…, tukirusha matangazo yetu kutoka Nyakato, GM 97.3 FM.”

Akizungumza kandoni mwa majengo ya GM 97.3 FM Radio, Patrick Mnubi ambaye ni mtangazaji alisema kuwa redio yao inasikika Musoma, Bunda, Butiama, Serengeti na maeneo mengine ya mkoa wa Mara.

“Redio yetu itawaunganisha kwa pamoja watu wa mkoa wa Mara. GM itakuza udugu baina yetu.”

Katika utafiti wa Mwanakwetu, alibaini majina ya watangazaji kadhaa kama vile Imani Luoga na Rambo Elia wakirusha matangazo katika redio hii ya kijamii.

 

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dodoma, Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji Kigera, alisema kuwa yupo pamoja na GM 97.3 FM katika kuwahabarisha watu wa Musoma huku akiongeza:

“Redio ina mchango mkubwa katika kujenga udugu baina yetu. Binafsi natambua kuwa nchini Tanzania mchango wa redio unafahamika mno. Nina matumaini kuwa GM 97.3 FM itakuza mchango wa redio katika maendeleo ya watu wa Musoma, mkoa wa Mara na mikoa jirani.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa sasa vyombo vya habari vinaanzishwa kwa wingi huku mitandao ya kijamii ikishika kasi, ambapo redio, runinga na magazeti yamelazimika kuwa na mitandao yake ya kijamii ili kwenda sambamba na wakati. Huko Tanzania inakadiriwa kuwa na redio 250 zinazorusha matangazo yake kote nchini.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Musoma Waongeza Redio Nyingine ya Kijamii.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 










0/Post a Comment/Comments