Adeladius Makwega.Musoma.
Mara nyingi katika maisha yetu hapa duniani tunapata taarifa nyingi za watu kufunga ndoa huku tukitoa ahadi tele ya ile michango ya kufanikisha harusi hiyo, huku tukisahau jambo moja muhimu ya kuombea mema shabaha hiyo ya ndoa
Mei 20, 2026 Mwanakwetu alipokea ujumbe kupitia simu yake kuwa ndugu Phares Magesa anatarajiwa kufunga ndoa na Dkt. Mbiki Msumi.
Jambo hili lilimshitua mno Mwanakwetu kutokana na sababu nyingi mojawapo ni kuwa hawa ndugu wote wawili yaani Phares na Mbiki ni watu anaowafahamu kwa karibu miaka mingi nyuma wakiwa vijana wadogo katika harakati zao za maisha. Ujumbe huu Mwanakwetu aliupata akiwa Musoma Mjini majira ya jioni ya siku hii.
Mwanakwetu akiwa na anautazama ujumbe huu kwanza alimkumbuka ndugu Phares Magesa:
“Tangu akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Azania miaka ya 1990katikati ya Jiji la Dar es Salaam akiwa na shati lake jeupe na kaptura ya khaki. Baadaye Phares Magesa akiwa na mavazi yake ya Skauti Tanzania, kisha Pharesa Magesa kama Rais wa Mchezo wa Mpira wa Kikapu na mwisho akawa mwanasiasa wa CCM wilaya Temeke akisaka tiketi ya kura za maoni ndani ya CCM hasa Ubunge Jimbo la Kigamboni na baadaye jimbo la Mbagala nazo hekaheka hizi baadaye zilimpeleka akachaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wa Wilaya ya Temeke ambapo wakati huo CCM ilikuwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia kila Wilaya kabla ya kufutwa utaratibu huu, huku watu wa Mbagala wakimuunga mkono mno ndugu Phares Magesa ambaye ni mbobezi wa masuala la TEHAMA.”
Kumbuka Mwanakwetu anamkumbuka ndugu yake Phares Magesa mara baada ya kujulishwa kuwa anafunga ndoa na Dkt. Mbiki Msumi. Baadaye Mwanakwetu ilimjia akilini taswira ya Dkt. Mbiki Binti Msumi ambaye ni msomi wa sheria nchini Tanzania ambaye ni mbobezi wa sheria tangu ngazi ya chini kabisa hadi shahada ya uzamivu akiwa mhadhiri katika Chuo Kikuu Huria:
“Wakati Mbiki Msumi anasoma Shahada ya Kwanza ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa kati ya mwaka wa 2005-2008 , alikuwa binti mmoja mrefu, mweusi , mpole na mtulivu. Binti maarufu ambaye hakuwa na majivuno.”
Akilini mwa Mwanakwetu aliyakumbuka maneno haya kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa wakati huo Profesa Nicolous Bangu dhidi ya Mbiki Msumu:
“Huyu binti ni mrembo hadi akilini mwake, angalia namna alivyokuwa anayajibu haya maswali katika kamati yetu kumbe kweli binti huyu anauwezo mzuri wa sheria.”
Haya maneno aliyasema Profesa Bangu katika kamati mojawapo ambapo Mwanakwetu alikuwa mjumbe katika kikaoni hicho cha Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa wakati huo mwaka wa masomo wa 2007/2008.
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu anayakumbuka haya ya ndugu zake hawa wawili Ndugu Phares Magesa na Dkt Mbiki Msumi ambao ni Watanzania wenzake aliyokutana nao katika harakati kadhaa za maisha mkoani Iringa na Jijini Dar es Salaam. Baada ya tafakari hii ndipo Mwanakwetu aliamua kuyaandika haya yote.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu anajua namna Phares Magesa alivyo mtu muungwana, asiyekasirika kwa haraka, mtu anayesaidia watu sana kwa ujuzi, uwezo au mamlaka aliyonayo au yale Mungu aliyomjalia na huku Mbiki Msumi akiwa dada mmoja mpole, mnyenyekevu, mtulivu,mshika dini, mwenye akili za maisha na kitaaluma, mrembo na mwenye kulinda heshima yake. Kwa hakika Mwanakwetu anatoa pongezi za dhati kwa Phares Magesa na Mbiki Msumi kwa uamuzi wao wa kuamua kufunga ndoa, ndugu zangu:
“Phares na Mbiki hili ni jambo jema, Mungu awabariki katika maisha hayo ya ndoa mliyoamua kuyafanya baina yenu na hakika Mungu atawafungulia milango ya neema tele.”
Kwako wewe msomaji wangu tambua kuwa niliamua kuyaandika haya ili kuyafahamu na kujua dunia namna ilivyo na Mwanakwetu kama Mwanahabari kuweka mkono wake katika kusudio hili la ndoa la ndugu zake hao.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Binti Huyu Mrembo Hadi Akilini Mwake.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
.gif)







Post a Comment