.gif)
Adeladius Makwega-MBAGALA
“Kwa namna fulani, kujadiliana na kusaini makubaliano ya amani ni sehemu rahisi. Utekelezaji wake ni mgumu zaidi na changamoto mno. Makubaliano, bila kujali maandishi yake yalivyo mazuri, hubaki kuwa karatasi tu yasipotekelezwa kwa uaminifu—kwa kuzingatia si tu maneno yake bali pia dhamira yake.”
Haya ni maelezo ya hotuba ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan Oktoba 1, 2009 katika Mkutano wa Kimataifa wa Mazungumzo na Maridhiano ya Kenya: Mwaka Mmoja Baadaye. Katika hotuba yenye karatasi nne za A4.
Kofi Annan ambaye alikuwa raia wa Ghana anasimulia namna alivyopigiwa simu na Rais wa Ghana wakati huo:
“Mnamo Januari 2008, nilipokea simu kutoka kwa Rais Kufuor wa Ghana, ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, akiniomba kwa niaba ya umoja huo kusaidia kusuluhisha mgogoro nchini Kenya, nilijua kwamba kazi hiyo haitakuwa rahisi. Kenya ilikuwa taa ya matumaini kwa Afrika. Ilikuwa nchi yenye utulivu wa kiasi, ikiwa na uchumi uliokuwa unakua kwa kiwango cha wastani na tabaka la kati lililokuwa likipanuka. Kenya ilikuwa muhimu kisiasa na kiuchumi kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na hali yoyote ya kutokuwa na utulivu wa muda mrefu nchini humo ingeathiri vibaya ukanda mzima. Kwa hiyo, ilikuwa muhimu sana kuchukua hatua za haraka mapema iwezekanavyo. Hili lilithibitishwa wakati wageni mbalimbali walipoanza kuwasili Nairobi katika hatua za awali, wakiwemo Askofu Mkuu Desmond Tutu, pamoja na marais wa zamani ambao ni wanachama wa Jukwaa la Viongozi wa Afrika: Marais Chissano, Kaunda, Mkapa, na Masire. Rais Kufuor aliniambia pia kwamba angeomba Rais Benjamin Mkapa na Mama Graça Machel, kuungana nami katika Jopo la Watu Mashuhuri wa Afrika kusaidia katika mchakato wa usuluhishi.”
Katika hotuba yake hii Kofi Annan aliwataja viongozi kadhaa huku Benjamin William Mkapa Rais wa Awamu ya Tatu wa Tanzania ndiye Rais Pekee aliyetajwa mara mbili hotubani. Hapa Tanzania haikutajwa mara mbili kwa ngekewa bali mchango wa Tanzania kwa mataifa ya Afrika ulitambulika, uliheshimka huku ukipambwa na utulivu ulikuwa silaha kubwa. Watanzania wa leo ebu tujiulize kweli leo hii anatumwa Rais Nicoraous Chakwera Rais Mstaafau wa Malawi kuja kusaidia kuweka mambo sawa nyumbani kwetu? Jamani viongozi wa sasa wa Chama Cha Mapinduzi mmelogwa na nani? Ili tumtafute muaguzi aje kuweka mambo sawa.
Je viongozi wa sasa wa Tanzania waliyo madarakani na wastaafu hawajiulizi wao wamechukua hatua gani kuyaweka mambo haya sawa? Je kama Benjamin Mkapa angekuwa hai maana yake haya mambo yasingalitokea? Viongozi wa sasa wa Tanzania wanatakiwa kukwepa ubinafsi na umimi ili Tanzania iweze kuvuka hatua hii.
Katika hili Watanzania wanatiliana mashaka wakisema maneno haya:
“Yule hawezi kulitatua hili yeye ni chanzo cha wote na isitoshe mwanae ni waziri.”
Kwa hakika uwaziri kwa yoyote yule hauna tija kama hali ya Tanzania haijatengemaa, lazima tufahamu kuwa zipo koo nchi hii zipo tangu uhuru hazijawahi hata kuwa watumishi wa umma ngazi yoyote ile, wala viongozi ngazi ya shina lakini maisha yao yanakwenda vizuri, viongozi lazima wawe na nia njema kwa jamii na siyo kingine.
Msomaji wangu nakuomba ulitazame hili la Tanzania vizuri sambamba na ule mgogoro wa Kenya ambapo ulianza mara baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi ule wa Disemba 27, 2007 na Mungu Bahati Januari 22, 2008 Kofi Annan na wenzake walikuwa wamewasili Kenya na waliingia kazini na hadi Februari 28, 2008 kazi ilikuwa imekwisha na kitabu kikafungwa na ndiyo maana Oktoba Mosi, 2009 Koffi Annan akiwa Geneva anasema maneno haya:
“…kujadiliana na kusaini makubaliano ya amani ni sehemu rahisi. Utekelezaji wake ni mgumu zaidi na changamoto zaidi. Makubaliano, bila kujali maandishi yake yalivyo mazuri, hubaki kuwa karatasi tu yasipotekelezwa kwa uaminifu—kwa kuzingatia si tu maneno yake bali pia dhamira yake.”
Hata katika hili la Tanzania linahitaji dhamiri safi kwa kila kiongozi na kila mmoja wetu anaweza akaja huyu akaenda akaja yule akaenda akarudi kisha kusiwe na jipya.
Hali ya Tanzania ya mashaka imeenza hata kabla ya Uchaguzi Mkuu, pengine wengine wanaiona tangu 2021 watu kutekwa na kuuwawa na wakati wa uchaguzi hali ikawa tete zaidi bunduki nje nje watu waliojeruhiwa na maiti hadharani , kutekana na mauwaji yakiendelea na miezi inasonga, ilikuwa mmoja sasa inakwenda saba baada ya Oktoba 29, 2025. Swali ni je nani huyo anauwezo wa kumshawishi Mtanzania kutoka kwake na kujongea tena katika sanduku la kura ili apige kura kumchagua kiongozi wake? Katika baadhi ya maeneo watu wamezikataa kabisa ofisi za CCM na sare zao zimefichwa michagoni. Haya ni ya ndani ya CCM hasa kwa wanachama wa mashinani, nani huyo mwenye uwezo wa kurejesha hali upya?
Msomaji wangu hii ni tafakari yangu ya leo ambayo niliamua kuiweka katika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika hali hii inavyopimwa na Mwanakwetu anaona kuwa ndani ya CCM kwa viongozi wetu wa sasa hayupo mwenye uwezo wa kufanya mizungu na kuikoa CCM na huku uimara wa chama ndiyo uimara wa serikali na maana yake muitikio ndani ya chama ndiyo unatoa imani ya muitikio kwa serikali yake. Katika hali hii Mwanakwetu bado anaamini ile simulizi ya Idris Abdul Wakil inaweza kuwa mwongozi wa sasa hata kama tumechelewa, hapa hakuna Chakwera wala nani bali kisa cha Wakili hicho pekee kinaweza kuwapa moyo makundi yote yenye malalalimiko iwe ndani ya CCM, kundi la Wapinzani wa Kweli (CHADEMA) na Watanzania kadhaa ambao hawapo katika vyama vya siasa lakini wanalitakia mema hili taifa.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Mizungu ni Kisa cha Idris Abdul Wakil.”
Nakutakia Siku Njema
0717649257






.gif)
Post a Comment