Adeladius Makwega-MBAGALA.
Unapotembelea nyumbani kwa akina Mwanakwetu Mbagala utabaini kuwa eneo hili limejaliwa kuwa na miti kadhaa ya asili inayostawi katika majimaji, japokuwa kwa sasa maeneo haya yanakaliwa na watu kama makazi lakini kwa sehemu za bondeni uoto wa asili wa Mbagala unaonekana vizuri kwa maeneo jirani na Bahari ya Hindi, Mbagala ikipambwa ma miti inayokua kando kando ya bahari ni kama vile mikoko na mivinje ikiwa miti muhimu sana maana ina kazi muhimu za kimazingira na kiikolojia:
“Mizizi mikubwa ya mikoko huzuia mmomonyoko wa udongo unaosababishwa na mawimbi makali ya bahari na dhoruba. Misitu ya mikoko ni makazi salama kwa viumbe wadogo wa baharini kama samaki, kaa, na kamba wanaokua kabla ya kwenda bahari kuu. Miti hii inasaidia kufyonza hewa ukaa (carbon) nyingi, hivyo kusaidia kupunguza joto duniani. Pia kuna Mivinje ambayo ni miti ya pwani hufanya kazi kama vizuizi vya upepo mkali, kulinda maeneo ya makazi ya watu wa Mbagala kama vile Mbagala wa Buruda, Mbagala Misheni na Mbagala Msikitini,Mbagala Mangaya, Mbagala kwa Selenge na Mtoni Kijichi. Miti hii pia inasaidia kuchuja uchafu na udongo unaotoka nchi kavu kabla ya kuingia baharini, hivyo maeneo husika huwa na maji safi na isitoshe mimea hii ni kinga muhimu kati ya nchi kavu na bahari.”
Msomaji wangu hizi ni simulizi za Mbagala.
Kwa hakika wakazi wa Mbagala kwa umasikini wetu, kwa ufukara wetu ukifika kando ya Bahari ya Hindi mikoko na mivinje utaiona imestawi vizuri haikatwi hovyo maana ulipo Mkoko ni mazalia ya Dagaa Kamba na Kamba Kochi. Japokuwa mara mojamoja tunakata miti ya kupachikia ndoano, ebo shamba letu wenyewe nani atuwekee masharti?Tunatumia ili kwenda kuvua samaki ili tuapate madini ya samani na ndio maana nduguze Mwanakwetu watu wa Mbagala wana akili sana maana Mbagala tunakula sana Dagaa Kamba , Udufu, Kamba Kochi na samaki wengi wa maji jumvi.
Msomaji wangu pia nakuomba ufahamu hili
“Mkoa wa Dar es Salaam una mito kadhaa inayopita katikati yake na kumwaga maji katika Bahari ya Hindi. Mito hii ni muhimu kwa ajili ya mifumo ya maji taka, kilimo cha umwagiliaji, na mazingira na huku Mbagala ikibarikiwa kuwa na mito muhimu miwili inayopitisha maji mwaka mzima.
Mito hiyo ni Kizinga na Mzinga. Kizinga ni mto unaotiririka maji mwaka mzima, ukianzia Pugu na kuingia Bahari ya Hindi upande wa kusini wa Dar es Salaam (Mbagala) na Mto wa pili ni Mzinga ni mto wa kudumu unaotiririka na kumwaga maji yake Bahari ya Hindi, ukipita eneo la Mbagala.”
Huku mito mingine Mkoani Dar es Salaam ni Mpiji, Mto huu unaunda mpaka wa kaskazini kati ya Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, na huingia Bahari ya Hindi na mto mwingine ni Msimbazi: Huu ndio mto mkuu zaidi unaopita katikati ya jiji ukianzia Kisarawe na kumwaga maji yake katika Bahari ya Hindi karibu na Daraja la Selander. Pia kuna Mto Mbezi: Huu ni mto mwingine unaotiririka hadi Bahari ya Hindi katika eneo la Kawe:
“Mito hii inasaidiwa na vijito vidogo vidogo kama vile Luhanga, Sinza, Tabata, Kijitonyama, na Mlalakuwa ambavyo vyote kwa pamoja vinaingia kwenye mifumo mikuu ya hiyo mito.”
Mwanakwetu ana hakika leo hii msomaji wake atatambua kuwa Tabata kwa asili lilikuwa jina la mto na siyo eneo kama lilivyo leo hii hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Sinza, Mlalakuwa, Luhanga na Kijitonyama (Kijito chenye Wanyama)
Msomaji wangu nakuomba nikupe siri ya kazi kuu inayofanywa na mito inayomwaga maji baharini kwanza ni kusafirisha na kuingiza maji safi, madini, mchanga, na matope kutoka nchi kavu kwenda kwenye bahari.
Kazi zingine ni:
“Mito huleta maji safi ambayo husaidia kuongeza kiasi cha maji baharini na kurekebisha msongamano wa chumvi. Mito huleta mchanga na matope mengi na kuyatua baharini inapomwaga maji. Baada ya muda, mchanga huu hujenga ardhi mpya ambayo ni delta. Mito pia husafirisha Lishe hapa hubeba rutuba na lishe kutoka nchi kavu ambayo ni muhimu kwa viumbe wa baharini kama vile mimea na samaki. Mito ni sehemu ya mzunguko wa maji duniani, ikirudisha maji ya mvua yaliyokusanywa nchi kavu kwenda baharini ili mchakato wa uvukizaji uanze tena, pia mito inaweza kulingana na misuli ya mwili wa binadamu.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika mito mikubwa miwili ya Mkoani Dar es Salaam yaani Mzinga na Kizinga, Mwanakwetu amekunywa maji yake, ametafuta chambo, amevua samaki na ameongelea mno tangu akiwa mdogo na kizuri zaidi mito hii hufanya kazi ya kuwapa maji safi watu wa kando kando ya bahari kama vile kupikia, kunywa na kuonga baada ya kutoka baharini ambapo maji ya bahari ukioga unapauka hivyo ukitoka bahari unajisuuza katika maji ya mito ya kando ya bahari. Miaka ya zamani ukienda eneo ambapo kuna ngalawa za wavuvi wengi utaona mafiga ya kupikia yapo kando ya mito hii ya maji baridi ambapo hupika chakula chao hapo huku wakikaa katika miti ya kivuli kusubiria mitengo ya nyavu zao kunasa samaki aua kungojea pepo kutulia.
Msomaji wangu nakuomba nikwambie hili , kwa utaratibu wa watu wa Pwani ya Tanzania kama kutatokea kifo ndani ya bwawa, mito na hata Bahari eneo husiku huwa watu hawaendi kwa muda mrefu ikionekana kana kwamba eneo hili limenajisika, watu hawanyi maji na wanakula kiapo kutoyatumia maji hayo milele. Ipo mifano ya visima vingi vilivyotelekezwa baada ya mtu kudumbukia na kufa ndani yake.
Hapa utakutana kisima kina maji tele, kina maji masafi, maji yapo mwaka mzima, kipo jirani na kijiji lakini watu wanafunga safari ndefu kufuata maji mbali, ukiuliza mbona maji haya hamuyatumii? Kwanza wanakuficha lakini wakikupenda watakwambia. Kisima kile kilificha mtu, hivyo hakitumiki tena, maana Kisima Kilichoficha Mtu Hakitumiki Tena.
Mtu alitolewa kisimani na akienda kuzikwa yale ni maji lakini -Maji ya Kisima Najisi Hayanywekwi.
Msomaji wnagu ebu angali umuhimu wa miti kando ya mito, tazama umuhimu wa mito kando ya bahari ambapo Dar es Salaam imejaiiwa kuwa na mito kadhaa, kwanini sasa mito hii iwe hodari wa kupokea miili na damu ya watu waliuwawa? Kweli Mwanakwetu na nduguze waikache mito yao ya Dar es Salaam?Iwe Kizinga, Mpiji , Msimbazi, Mzinga , Mbezi na mito mingine midogomidogo?Hii mito ni uhai wa binadamu na mimea.
Kwa makala haya Mwanakwetu anatoa tahadhari kubwa kwa kila atayeyasoma makala haya hivi vifo vya watu na miili yao kuelekezwa katika mito hii havina maana , wanaofanya hivyo hawezi kuwa salama bali wanazidi kujiangamiza wao wenyewe.
“Mnaofanya haya mauwaji tambueni jamii itawasusia , mtanuka damu na mtakataliwa na hakuna atakayeweza hata kuwasabahi kwa Asaalam Aleikuum wala kuwapa mkono, mtakataliwa nyinyi wenyewe, watoto wenu, wajukuu zenu , vitukuu vyenu hadi Dahari.”
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Maji ya Kisima Najisi Hayanyweki”
Nakutakia Siku Njema.
0717648257












.gif)
.gif)
Post a Comment