Adeladius Makwega-MBAGALA
Mei 17, 2026 ilikuwa ni siku ya kushangaza mno kwa Mwanakwetu maana alimkumbuka marehemu Omari Idd Bini Waziri kada wa CCM ambaye awali alikuwa ni Staff Sajenti wa Jeshi la Wananchi Tanzania Kikosi cha Mbagala kabla ya kustaafu ambaye alikuwa akiishi Mbagala Kizinga, nyumba namba moja, huku akina Mwanakwetu wakiishi kwao nyumba namba 7. Omari Iddi Waziri alikuwa na mkewe aliyefahamika kama Amina Seleiman Binti Kilemile hawa wote wakiwa jamii ya Wazaramo na Wandengereko wa Mbagala na Mkuranga.
Katika kumkumbuka huyu ndugu Waziri, Mwanakwetu alikumbuka tukio hili:
“Siku hii ilikuwa Jumamosi ya mwaka wa 2003, mimi nikiwa mwalimu wa Shule ya Sekondari Dar es Salaam International School&Sinza Tower Sekondari, nikaitwa nyumbani kwa ndugu Waziri…nilipofika hapa kwake ambapo kulikuwa na mti wenye kivuli, kulikuwa na kundi wa wana CCM akaniambia: ‘Sasa mwanangu nimekuita uje tusaidiane kuchagua jina la Tawi la CCM hapa kwetu maana hapa tuna shina tu la Wakereketwa na idadi ya wanachama inaturuhusu kuwa na tawi kamili la CCM, sasa natamani ndugu zangu tuwe na tawi. Mimi huwa napata tabu sana kila ninapokwenda kuchagua viongozi wa kata huwa ninaunganishwa na matawi ya mbali na kwetu maana sisi hapa hatuna tawi. Jamani kumbukeni hapa ni nyumbani kwa Ngamba, yeye ni kada anayeheshimika mno.
Hapa lazima tuwe na tawi la chama chetu.’ Wajumbe wakasema sawa na hilo ni wazo zuri, majina yaliyopendekezwa pale kikaoni yalikuwa haya: Kizinga namba 4, Mandwanga, Mbuyuni na Kimicha. Kikaoni tukajadili wee jina moja baada ya lingine. Kizinga namba 4 lilikataliwa kisa ni kurudia majina yale huku kukiwa ni tawi namba 1, namba 2 na namba 3. Mandwaga lilikuwa jina la ukoo maarufu sana hapo mtaani lakini lilikataliwa kwa sababu lilikuwa jina la ukoo unaounga mkono Chama cha Wanachi (CUF). Mbuyuni lilikataliwa kisa lilikuwa jina linalotumika mno na hoja ikaja kwa jina la Kimicha. Hapa jina la Kimicha lilijadliwa mno mama mmoja akasema kama mmelikata jina la Mandwanga mbona hata hao vijana wa Jaji Kimicha wana nongwa tele? Wao wanamiliki ardhi kubwa watoto wetu wanakosa shule jirani? Mabinti zetu wanafunga safari ndefu hadi wengine wanabakwa njiani na isitoshe binti Kimicha ni polisi Kituo cha Chang’ombe, ukiwa na shida yako ukienda kituo cha Polisi Chang’ombe binti Kimicha ambaye ni WP ukifika pale kaunta anajikausha kama hawatambui watu wa Mbagala, wakati kazaliwa hapa hapa, kasoma hapa hapa na kavunja ungo hapa, kwanini jina hili tulikubali? Mimi nalikataa jina hili 100 kwa 100. Mjadala ukawa mzuri sana ngazi ya shina wajumbe wa kikao tunajadili. Mwenyekiti wa Kikao hiki ambaye alikuwa Mjumbe Serikali la Mtaa wa Mbagala Kizinga kwa Kanda hiyo Omari Idd Waziri akasema Makwega unashauri nini? Makwega akajibu Mwenyekti tupige kura. Mwenyekiti akakubali ushauri wa Mwanakwetu na kura zikapigwa .
Majina pendekezwa yalikuwa mawili Mandwanga na Kimicha, kumbuka Kimicha ni jina la Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Kura zikapigwa na jina la Kimicha kushinda. Huku baada ya kura Omari Idd Waziri akasema nina matumaini kuwa Jaji Kimicha kwa kuwa ana ardhi kubwa eneo hili hata kama tukimuombwa pengine atatoa ardhi yake kujenga ofisi ya CCM ya tawi lenye jina lake. Kikao hiki kilihitimishwa na jina pendekezwa la tawi ilikuwa Tawi la CCM Kimicha Kizinga Mbagala.”
Msomaji wangu kumbuka haya yote ni rejea akilini mwa Mwanakwetu tu na hii ni Mei 17, 2026. Hapa Mwanakwetu anakumbuka kisa cha Tawi la CCM Kimicha Mbagala miaka 23 iliyopita.
Msomaji wangu ngoja nisibakize mkia maana nimemla ng’ombe mzima:
“Japokuwa jina la Kimicha lilishinda wana CCM hawa hawakupata hata ardhi kidogo ya kujenga Ofisi yao ya chama, awali walikuwa wapangaji katika nyumba kadhaa kama vile Kwa Bwenzi na maeneo mengine na baadaye wakapata ardhi lakini ikaporwa na tofali kuibiwa hadi baadaye diwani wa CCM wa Kata ya Mbagala mwaka wa 2020-2025 alipofanikisha kupatikana ardhi na kujengwa ofisi hii ya tawi la CCM na hadi leo hii tawi la CCM Mbagala Kimicha wana ofisi kamili.”
Hii ni kumbukumbu ya Mwanakwetu kama mwana CCM miaka 23 iliyopita nyumbani kwao Mbagala akiwa katika kikao cha CCM ngazi ya Shina.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Viongozi wa CCM Taifa mfahamu kuwa uwe diwani, uwe mbunge au uwe Rais ndani ya CCM wewe siyo mheshimiwa wewe ndugu tu. Kumbukeni mnapochaguliwa kushika nafasi hizo iwe diwani, iwe ubunge iwe urais lazima uwe makini kuwalinda ndugu zako wa ngazi ya chini ambao ni wanachama wenzako na hata wale wasio wana CCM maana CCM ina amini kuwa sisi sote na Afrika ni moja. Wewe kiongozi usijione bora kuliko wenzako,wanachma wenzako tunakutambua kuwa wewe ni ndugu tu.
Sasa kilichotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ndugu zetu , wanachama wenzetu wamuuwawa kwa kushambuliwa na risasi , hawa waliuwawa ni wana CCM wenzetu ambao ndiyo tulikuwa tunachagua nao majina ya matawi yaweje? Tulikuwa tunachangia nao ujenzi wa ofisi za chama tunajengaje? Nani huyu aliyeagiza kushambuliwa ndugu zetu?
Hili alikubaliki hawa waliowashumbulia wanachama wetu, ndugu zetu, hawa waliobeba silaha mitaani na kuwadungua watu tukiwaomba waje kutusaidia kufungua ofisi za chama chetu mitaani na vijijini zilifungwa kwa hasira ya wanachama wanaweza kujitokeza?
Kwa hakika Mwanakwetu anasema wazi kuwa hili alikubaliki lazima aliyeagiza hili, aliyefanya haya, wote wawajibike mara moja na kama yupo mwana CCM anayekalia kimya huyu ni adui namba moja kwa kila mtanzania maana thamani ya uhai wa Mtanzania, damu ya Mtanzania haiwezi kulinganishwa na cheo chochote kile iwe udiwani, ubunge au urais
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Lazima Wawajibike.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
.gif)







.gif)
Post a Comment