.gif)
Adeladius Makwega-MBAGALA
“Matumizi ya wanamgambo wa kukodi (mamluki) yana madhara makubwa na ya muda mrefu kiusalama, kibinadamu, na kisiasa. Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na zile za Umoja wa Mataifa (UN) zinazohusisha vikosi kadhaa vya mamluki, athari hizo ni pamoja na: Kuchochea na Kuendeleza Migogoro: Wanamgambo hawa mara nyingi huongeza nguvu ya kivita, na kusababisha migogoro kudumu kwa muda mrefu na kuwa mikali zaidi. Ukiukwaji wa Haki za Binadamu: Kwa sababu hawaongozwi na sheria za kijeshi za nchi hizo (rules of engagement), wanamgambo wa kukodi mara nyingi wanahusika na mauaji ya kiholela mitaani, mateso, ubakaji, ulawiti, unyanyasaji na utekaji wa raia wasio na hatia. Kuvuruga Usalama wa Kikanda: Uhamishaji wa wapiganaji kutoka nchi moja kwenda nyingine, unasambaza silaha na mafunzo ya kijeshi, jambo linalotishia utulivu wa nchi jirani.
Uharibifu wa Miundombinu: Mapigano yanayohusisha makundi haya mara nyingi husababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya kijamii kama hospitali, nyumba, na shule na matakwa yao ya kilaghai hili likiwa jambo linalosababisha majanga ya kibinadamu. Kudhoofisha Jeshi la Taifa husika: Uwepo wa vikosi vya kukodi unaweza kupunguza mamlaka na uwezo wa jeshi rasmi la nchi, na wakati mwingine kuleta migongano kati ya vikosi hivyo. Ukali wa mapigano ya wanamgambo hawa husababisha raia kukimbia makazi yao na kuzidiwa kwa uwezo wa nchi jirani kupokea hao wakimbizi. Kwa ujumla, matumizi ya mamluki yanahatarisha utu na kuchelewesha utatuzi wa kudumu wa Amani na kuyanyima maendeleo maeneo yenye changamoto hizo.”
Maelezo haya yalipigiwa chapuo zaidi Februari 4, 2019 kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na wajumbe wa kikao hiki cha juu cha umoja huu wakitilia maanani ni kwa jinsi gani askari wa kukodi wanatishia siyo tu amani na usalama duniani bali pia uhuru na mamlaka ya mataifa barani humu.
Akihutubia mkutano huo ulioongozwa na Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea ambaye nchi yake ndio ilikuwa inashikilia kiti cha Urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati huo Katibu Mkuu Profesa Antonio Guterres alisema kuwa askari wa kukodiwa ni suala ambalo limekuwepo tangu enzi na enzi na kutokana na kufanyika kisiri, inakuwa vigumu kupata takwimu sahihi na hata kuwabaini:
“Ripoti zinadokeza kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya askari hao na wapiganaji wa kigeni hali inayofanya mizozo kuzidi kuwa migumu kutatuka na baadhi ya askari mamluki wanahama kutoka vita moja hadi nyingine huku wakilipwa pesa nyingi, wakitekeleza majukumu yao haramu kwa uthabiti mkubwa, wakijikusanyia utajiri mkubwa iwe wa fedha au madini bila uwajibikaji wowote na kupuuza kabisa sheria za kitaifa na kimataifa .”
Hali hii inafanya kuwa ni vigumu hata kuwabaini sura zao, majina yao na mataifa wanapotokea baada ya kukamilisha kazi zao, wahusika hao mara nyingi wakiwa wamevalia kiraia huku wakiwa wamebeba silaha za moto, nzito nzito wakiwa na ujuzi na uzoefu mkubwa wa kivita.
Profesa Guterres alisema kuwa shughuli za wanamgambo mamluki zinatia hofu kubwa kwa kudaiwa kuchochea ghasia zaidi huku akigusia dunia inaweza kutatua kwa kuyafanya yafuatayo:
“Kuimarisha mifumo ya kisheria, kitaifa na kimataifa ya kudhibiti askari hao kutoka eneo moja kwenda linguine akitolea mfano mkataba wa kimataifa wa mwaka 1989 dhidi ya kuajiri, kutumia, kufadhili na kufundisha askari wa kukodiwa; International Convention against the Recruitment, Use, Financing and Training of Mercenaries. Kuongeza ushirikiano wa pande mbili, kikanda na kimataifa ikiwemo kwenye usimamizi wa mipaka ambako silaha na wapiganaji wa kigeni wanamiminika na kupenya na kuchochea mizozo, huku idara za uhamiaji zikitakiwa kutunza kumbukumbu za wale wanaohisiwa ni wanamgambo wa kukodi. Pia kuchunguza sababu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kisaikolojia zinazochochea kuimarika kwa shughuli za askari wa kukodiwa. Juhudi zaidi za kuweka fursa kwa vijana zitakuwa ni jambo jema katika kupunguza vitendo vya vijana kuvutiwa na kazi za wanamgambo wa kukodi na pia kuwa na misimamo mikali na huku viongozi na vyama vya siasa wakubali kushindwa kisiasa na watoe fursa kwa wengine kuingia madarakani kidemokrasia maana vijana wenye nguvu wakikosa fursa zaidi wanaweza wakatumia nguvu zaidi kunyakua madaraka.”
Msomaji wangu hizi ndizo simulizi za wanamgambo wa kukodi kama zilivyotayarishwa na Mwanakwetu siku ya leo.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika wanamgambo wa kukodi ni biashara ambapo yapo makundi yanamiliki magenge haya huku yakishirikiana na watu maarufu katika biashara ya silaha na biashara hii haramu katika maeneo mbalimbali yakitumia ugumu wa maisha ya vijana kuwapa kazi hii.
Kulingana na ripoti za hivi karibuni inadaiwa kuwa dhana ya ‘mawakala wa wanamgambo wa kukodi’ au makampuni ya kijeshi ya kibinafsi imekuwa ikitumika katika migogoro mbalimbali duniani, Mawakala hawa mara nyingi hutumika kama mbadala wa majeshi ya serikali, wakijihusisha na ulinzi wa rasilimali, mafunzo, au mapigano ya moja kwa moja.
Kwa Maeneo menginne makundi haya huwa kama makampuni ya ulinzi tu lakini kumbe yanakuwa mawakala wa wanamgambo wa makundi ya kukodi na hata pale ukikagua na kutafiti maisha ya wanamgambo hao huwa ni mazuri sana kwa kazi hiyo ya ulinzi kumbe wakiwa na kazi nyingine na kukodiwa kwa kazi maalumu wakizunguka kutoka taifa moja hadi lingine kwa malipo manono.Upo mtazamo kuwa mawakala wa wanamgambo wa kukodi wanaweza kuwa watu maarufu, wenye ushawishi, wanamitindo, wanamichezo na hata wafanyabiashara wakubwa wakubwa ambapo ni vigumu kutambuliwa kwa haraka kama wadau wa hizi harakati.
Kwa hakika dunia lazima ipambane kwa pamoja kupinga wanamgambo wa kukodiwa huku mataifa ya Afrika yawe makini ili kuzuia mauwaji ya raia wake wasio na hatia yoyote ile kwa kutumia magenge ya kihalifu na wanamgambo wa kukodi wenye malengo kadhaa.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Kataa Uwakala wa Wanamgambo wa Kukodi ”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257




.gif)
Post a Comment