Kanali Mtambi Ashiriki Misa ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu

 


Adeladius Makwega, Musoma - Mara

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Kanali Evansi Alfred Mtambi, mapema Mei 31, 2026, ameshiriki Ibada ya Misa ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Parokia ya Songe, Jimbo Katoliki la Musoma.

Akihubiri katika Ibada ya Misa hiyo, Paroko wa Songe, Padri Wilbert Matembo, kwanza alielezea dhana ya Utatu Mtakatifu:

"Utatu Mtakatifu ni imani yetu katika Kanisa Katoliki, hasa tukiamini uwepo wa Mungu Baba, Mungu Mwana na Roho Mtakatifu. Huu ndiyo msimamo wa Ukristo ambapo makanisa kadhaa yametokea katika Kanisa letu."

Akiendelea kuhubiri, Padri Matembo aligusia suala la amani akisema ni jambo la kuzingatiwa na kila mmoja, huku akisisitiza umuhimu wa kuombeana na hata kuwaombea viongozi.

 

Akihitimisha homilia yake, Padri Matembo alisema kuwa anashukuru sana Mkuu wa Mkoa wa Mara kusali nao pamoja katika sherehe hiyo ya Kanisa Katoliki.

Parokia ya Songe ni miongoni mwa parokia kadhaa katika Jimbo Katoliki la Musoma, na ipo jirani na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma.

Katika ibada hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mara, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, ndugu Humphrey Kongoke, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka.

✉️ makwadeladius@gmail.com

📞 0717 649 257







 


 

0/Post a Comment/Comments