Adeladius Makwega-MBAGALA.
Mapema ya Mei 25, 2026 Mwanakwetu alikwenda kunywa chai mkahawani, kwa bahati mbaya hadi saa 3 ya asubuhi mkahawa huu walichelewa kuandaa kinywaji hicho , hivyo basi Mwanakwetu alirudi alipotoka.
Njiani alikutana na ndugu mmoja mtu mzima akasalimiana nae , wakati salama zinaendelea akapita mtu mzima mwingine akatusalimu sote kwa maneno HABARI ZENU! Sote tukajibu NJEMA. Ndugu huyu akaenda mbali zaidi na kumsalimia huyu ndugu kando ya Mwanakwetu kwa salaam ya SHIKAMOO. Ndugu kando ya Mwanakwetu akajibu MARAHABA.
Ndugu aliyewasabai aliendelea na safari yake. Ndugu aliyepewa SHIKAMOO akauliza swali kwa maneno haya:
“Mwanakwetu hivi kati ya mimi na huyu ndugu aliyenisalimia SHIKAMOO nani mkubwa?”
Mwanakwetu akajibu kuwa umri wetu sote hapa unalingana.
Ndugu huyu akaja na swali lingine:
“Hivi ni haki mimi kusalimiwa SHIKAMOO na yule ndugu?”
Mwanakwetu akajibu kuwa inawezekana ikawa haki maana SHIKAMOO ni salaam inayoweza kutolewa kutokana na sababu mbalimbali. Ndugu huyu akawa na kiu ya kuzijua sababu hizo.
Mwanakwetu akajibu:
“Shikamoo ni neno linalotumiwa kumsabahi mtu aliye jirani nawewe au mbali na wewe kutokana na kuwepo kwa tekinolojia za sasa za mawasiliano mathalani video, simu na mitandao. Neno SHIKAMOO linatokana na maneno mawili ya Kiswahili SHIKA maana yake gusa kitu na MOO maana yake miguu huku kiitikio MARAHABA kinatokana na kuundwa na maneno mawili MARA hapa ni kitu kinachofanyika zaidi ya moja na HABA ikimaanisha uchache. Maana yake Nipo Chini ya Miguu yako huku anayeitikia anajibu kwa kebehi kuwa ni mara chache.
Pia yako madai kuwa MARAHABA ni salamu inayotumiwa ikimaanisha sawa kabisa.”
Historia ikidai kuwa hii salaam ilitumika na kuenea mno kipindi cha biashara ya utumwa na biashara ya Pwani na Bara, biadhara ya mtumwa na muungwana ambapo mtumwa alisema SHIKAMOO huku Mwaarabu alijibu MARAHABA.
Kumbuka Mwanakwetu anaongea na jamaa yake kisha akasema:
“Matumizi ya Shikamoo yanaweza kuwa kati ya mtu mdogo kwa mtu mkubwa mathalani mtoto kwa baba , binti kwa mamaye mwanafunzi kwa mwalimu. Pia shikamoo inaweza kutumika kati ya mtu mkubwa ambaye hana nafasi akamsalimu mtu mdogo ambaye ana nafasi, hili huwa linatokea sana mathalani kiongozi japokuwa ana umri mdogo inawezekana mtu ambaye na umri mkubwa akaingia ofisini kwake na kusema SHIKAMOO hapa unawajibu wa kujibu MARAHABA ili kuitikia maamkizi yake na hii inalingana kabisa na hali ilivyokuwa wakati wa Waarabu na biashara ya utumwa, hapa heshima inapewa yale mamlaka. Pia Shikamoo inaweza kutumika kwa baba mdogo , mama mdogo, shangazi japokuwa anayetoa SHIKAMOO akawa nana umri mkubwa lakini kinachosalimiwa ni ule ukubwa wa UBABA na ule UMAMA maana katika mila za Kiswahili haitarajwi Baba Mdogo au Mama Mdogo amsalimie SHIKAMOO mtoto wa Kaka yake au mtoto wa dada yake.”
Mwanakwetu kumbuka yupo na jamaa yake kando hapa kisha akasema:
“Wewe umepewa SHIKAMOO na yule mzee pengine kutoka na wewe kumuendesha kiongozi mkubwa kwa hiyo mzee yule amekupa SHIKAMOO ya kimamlaka tu.”
Jamaa huyu akasema hapa anakubaliana na Mwanakwetu na amejifunza hata kweo mathalani akifika ukweni mke wake ana dada zake ambao huyu jamaa amewazidi umri lakini akikutana nao huwa anawasalimu kwa SHIKAMOO na hii ni kwa heshima ile ya Udada kwa mke wake na wala siyo SHIKAMOO ya umri.
Baadaye Mwanakwetu aliagana na huyu ndugu na kisha kwenda kuyaandika makala haya kama yalivyo.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Makala haya ya Mwanakwetu siku ya leo yanashabaha kadhaa . kubwa ni ufahamu juu ya namna salaam ya SHIKAMOO- MARAHABA inayopaswa kutumika kulingana na muktadha mbalimbali na bila ya shaka msomaji wangu umejifunza vizuri.
Kwa hakika ukipewa SHIKAMOO na mtu aliyekuzidi umri usiwe mzito kuitikia maana kunakuwa na sababu kutoka kwa yule anayekusalimia hiyo SHIKAMOO, pale unapoitikia MARAHABA inasaidia huyu aliye jirani yako kujiamini zaidi na pia kukueleza shida yake mathalani wewe ni mwalimu salaam ya SHIKAMOO imetolewa na mzazi au wewe ni daktari salaam ya Shikamo imetolewa na mgonjwa hivyo unaitikia kwa sababu ya ualimu wako na sababu ya udaktari wako ni siyo sababu ya umri.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Hekima ya Salaam ya Shikamoo.”
Nakutakia Siku Njema.
Mwandishi wa makala haya ni mwalimu wa Somo la Kiswahili nchini Tanzania kwa miaka 10 na mwanahabari kwa ziadi ya miaka 20.
.gif)




.gif)


Post a Comment