Mlikuwa
Mnaandaa Mazingira ya Mchezo?
Adeladius Makwega-MBAGALA.
“Ili tuweze kushiriki vizuri michezo au kazi yoyote ile ya Sanaa za Maonesho jukumu la kwanza ni kufanya maandalizi kadhaa ikiwamo kwa timu/ wasanii wanaoshiriki kuwa na uwezo wa kucheza na kisha kuandaa mazingira au viwanja vya mchezo huo kuwa rafiki ili timu iweze kucheza vizuri.”
Ndiyo maana mashindano yoyote yale, utasikia timu zipo kambini sambamba viwanja vikikaguliwa kama vinakidhi ubora. Ndiyo kusema kama hautafanya maandalizi mazuri timu yako na viwanja vyako hauwezi kufikia shabaha yako.
Nakuomba msomaji wangu dhana hii mchezoni kama ilivyo ibebe twende kwa iliyokuwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo awali ikiwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kisha kurudishwa tena kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, haya ni kwa kipindi kifupi baada ya Kifo cha Rais John Pombe Magufuli.
Leo tuulizane maswali, hivi sisi kama Watanzania tumeweza kujiuliza shabaha ya mabadiliko haya ilikuwa nini? Kitendo cha kuiondoa Idara ya Habari MAELEZO na kisha kuirejesha tena pamoja na Idara za Utamaduni, Sanaa na Michezo kinatoa picha gani? Haya ni maswali ya Mwanakwetu kwako wewe unayeyasoma makala haya. Katika hiyo safari yote Idara ya Sanaa na Idara ya Utamaduni hazikupata misukosuko mikubwa lakini Idara ya Michezo hiki ni kipindi ambacho imenyumbishwa sana mithili ya mlevi aliyelewa pombe haramu ya Gongo iliyopikwa Mbagala nyumbani kwa akina Mwanakwetu baada ya kukamatwa na Askari wa Kituo cha Polisi Mbagala maarufu kama MATUBAI.
“Awali Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini Tanzania alikuwa ndugu Athumani Singo, baadaye huyu jamaa akapelekwa wizara nyingine nadhani TAMISEMI, kukawa kimya kwa muda kisha idara hiyo akapelekwa Ali Mayay (Tembele) ambaye alikuwa mgeni katika siasa za maofisini, hasa urasimu, fitna na majungu ya uongozi ili watu wafanikishe mambo yao. Japokuwa Ali Mayay alikuwa nahodha wa zamani wa Timu Mpira wa Miguu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).Ndugu Mayay tabia yake kazini alikuwa mtu mpole, mwema mtulivu ambaye hana maneno mengi, yeye anajua sana kupiga chenga uwanjani akijibu analoulizwa, kibaya na cha kusikitisha mazingira ya kazi hayakuweza kumfanya ashamiri katika nafasi hiyo, kama ilikuwa makusudi au la, kisha Ali Mayay akaondolewa na kupelekwa kijana mwingine ambaye kwa kumpima unaona uhakika na usalama Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini upo mashakani.”
Kipindi hiki hiki Mwanakwetu akashauri katika makala zake kadhaa kama nia Tanzania ifanye vizuri michezoni kimataifa, Serikali ya Tanzania iisuke upya Idara ya Maendeleo ya Michezo ya.
Tanzania tangu Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kwa kuchukua vijana kutoka Jeshi la Polisi Tanzania , Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Magereza na Jeshi la Wananchi Tanzania waende kufundisha Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na baadhi yao waiongoze Idara ya Maendeleo ya Michezo Wizarani wakishirikiana na vijana Watanzania wazalendo wachache watakaobakizwa na ili kuwapokea hawa askari, kisha tuone baada ya miaka 10 hali ya michezo itakuwaje? Kinyume chake unamchukua mtu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kisa Daktari ya Falsafa, huyu hana uwezo, hana ari ya kimichezo, yeye anaangalia kuandika muswada apate pesa, anatafuta vyuo vya kufundisha hapo Chuo Kikuu hata kuvitunza viwanja apate pesa, umri umesonga, vya maneno mengi, vitabu vingi, vitendo hakuna.
Watanzania tunataka ushindi, Watanzania wanataka ushindi michezo uwanjani, ushauri wa matumizi ya askari ni jambo la msingi, huyu ambaye atakuwa na kiburi cha kuwanyima askari ushirikiano tumuone. Huyu ambaye atakuwa anafanya kandarasi za ujenzi wa viwanja vya michezo na kupandisha gharama mara dufu tumuone.
Kwa hakika unapopiga hesabu ya fedha na miradi mikubwa iliyofikishwa katika Idara ya Maendeleo ya Michezo kwa kipindi hiki cha hekaheka hizi ni nyingi na ikiwa ya mabilioni kadhaa lakini tija viwanjani hakuna, mafanikio mengi katika hotuba.
Kipindi hicho chote Mwanakwetu aliandika makala kadhaa za uchambuzi hata juu ya Mkurugenzi Mpya wa Idara Maendeleo ya Michezo nchini Ali Mayay Tembele.
Mwanakwetu alijenga hoja kuwa ni heri ya Athumani Singo alikuwa nafuu maana alikuwa na uwezo wa kupinga baadhi ya mambo maana idara hii anaifahamu muda mrefu lakini Ali Mayay yule kuku mgeni hakosi kamba mguuni, ugeni wake ni tatizo, wajanja wanaweza kutumia fursa hiyo kutupiga chenga za mwili hapa kutakuja kuwa na shida mbeleni. Mwanakwetu alipiga ramli hadharani na makala hiyo ipo mtandaoni. Kipindi hiki ndipo ndugu Alex Mkenyenge akaondolewa Ukurugenzi wa Miundobinu na kupelekwa Malya kama Mkufunzi kwa uhamisho wa ndani na nafasi yake akapewa kijana mmoja kutoka Malya ambaye sasa ni marehemu aliyekuwa mkufunzi tu na akikosa uwezo wa kupambana na madhalimu. Wakati haya yanafanyika miradi kedekede inaanzishwa.
Kwa jicho la Mwanakwetu anasema wazi kuwa utumishi wa umma wa taasisi hii ulikuwa unachezewa mno huku Idara ya Habari haipo na hata wale waongeaji sana vikaoni, wale wenye tabia za kutoa mawazo waziwazi bila woga hadharani walihamishwa kwa uhamisho wa ndani au uhamisho wa Katibu Mkuu Utumishi.
Katika Utumishi wa Umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hauwezi kumuhamisha mtumishi kutoka taasisi moja kwenda taasisi nyingine nje ya wizara husika lazima Katibu Mkuu Utumishi ashirikishwe, yeye ndiyo karani wa kuiandika barua hii.
Msomaji wangu nakuomba ufahamu kuwa Utumishi wa Umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mojawapo ya mambo ambayo ni mali ya Watanzania ambao tumeupokea kutoka kwa Serikali ya Mkoloni.
Huu utumishi wa umma ni rasilimali kama ilivyo dhahabu na madini mengine. Japokuwa kuzungumzia Utumishi wa Umma kwa Tanzania inakuwa vigumu sana maana vitisho vingi lakini Mwanakwetu anasema vitisho hivyo haviwezi kufanya umiliki wa utumishi wetu wa umma kwenda kwa mtu yoyote yule awe mdogo au mkubwa.
“Ifahamike kuwa Tanganyika ndiyo ilikuwa na utumishi wa umma wenye idadi kubwa, hivyo chochote kinachofanyika vizuri kipongezwe na kibovu lazima tukiseme bila woga wowote .”
Hivi tujiulize unaanzisha miradi mingi wakati huo huo unazohofisha rasimali watu, huyu Meneja wa Uwanja unampeleka Halmashauri ya Wilaya, huko anakwenda kufanya nini? Huko anakwenda kupokea mshahara wa bure akingoja kustaafu tu.
“Waziri/Katibu Mkuu au taasisi fulani fulani zikisema huyu muamishe basi wewe unakubali tu ? Swali ni je kama huo uhamisho unatumika kutekeleza ajenda ya hujumu uchumi ? Hauoni na wewe uliyeandika barua ya uhamisho umeshiriki katika hujuma hizo?”
Katika hili Katibu Mkuu Utumishi awe makini.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hiyo Mwanakwetu anaamini hata hili la kupanda gharama kutoka Bilioni 187 za Uwanja wa Michezo wa Arusha na kuja kufika Bilioni 338.54 wale waliyokuwa Makatibu Wakuu Utumishi wa Umma waliowahi kuongoza wizara hii tangu 2021 waulizwe kwanini walikuwa wakihamisha hamisha watumishi hao kila mara? Leo Singo kesho Ali Mayay mara uhamisho wa ndani, hapa kulikuwa na nini ndani yake? Kunaweza kuibuka kuwa tunaingilia Wizara ya Utumishi inavyofanya kazi ni kweli lazima tuingilie na tufatilie hatua kwa hatua mtu na mtu maana ni wizara yetu.
“Utumishi wa Umma ni mali yetu na Tanzania ni nchi yetu, wazee wetu walifanya kazi ya kudai uhuru na sisi sasa jukumu letu ni kufuatilia kinachofanyika hatua kwa hatua na mienendo ya wanaofanya kazi hapo kama wanakidhi vigezo vya jamii yetu au la , kama kuna jambo tunalioa halijakaa sawa tunasema.”
Hoja ni yaleyale maelezo ya Mwanakwetu mwanzoni mwa makala haya kuwa:
“Ili tuweze kushiriki vizuri michezo au kazi yoyote ile ya Sanaa za Maonesho jukumu la kwanza ni kufanya maandalizi kadhaa ikiwamo kwa timu/ wasanii wanaoshiriki kuwa na uwezo wa kucheza na kisha kuandaa mazingira au viwanja vya mchezo huo kuwa rafiki ili timu iweze kucheza vizuri.”
Katika hili CAG yeye ameangalia rasimali fedha hapa makala haya inamkumbusha siku nyingine CAG kuangalia hata rasimali watu namna ilivyokuwa inachezewa kipindi hicho wakati tukio linatokea lakini Mwanakwetu bado anampa haki yake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Dkt. Charles Kichere kwa kazi nzuri aliyoifanya katika ripoti yake ya Ukaguzi kwa mwaka wa fedha ya 2024/2025. Hongera sana kaka.
Kwa hakika tukitaka kufanikiwa kimichezo nchini Tanzania tutumie vijana kutoka Jeshi la Magereza, Jeshi la Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Wananchi Tanzania na hata Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya mpeni Komandoo kutoka JKT na kisha Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Nchini mpe Komandoo wa JWTZ na hata Katibu Mkuu awe askari tuone.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Mlikuwa Mnaandaa Mazingira ya mchezo?”
Nakutakia siku Njema.
0717649257




.gif)
Post a Comment