Wanakwenda Kazini Wakiwa na Vitendea Kazi Vyao

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

Siku hii Mwanakwetu alikuwa anaisoma matini moja juu rafiki yake mhe.Eugene Wamalwa ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Haki na baadaye Waziri wa Maji wa Kenya kutoka chama cha Azimio la Umoja. Mwanakwetu akiwa anasoma matini hayo alipokea simu na kuwasiliana na ndugu yake mmoja katika mazungumzo ya kidugu, kisha Mwanakwetu akawa anataka kuuchapa usingizi, akiwa kitandani kwake akiuska usingizo alikumbuka tukio moja la mwaka wa 2014 kijijini Mbagala, Temeke Dar es Salaam Tanzania. Siku hii alikwenda Kata ya Mianzini ambayo ipo katika Jimbo la Mbagala kwa ndugu yake mmoja anayefahamika kama Jamila Ngogo -mama mmoja mwenyeji wa Lushoto kufuata paka maana nyumbani kwake Mwanakwetu alikuwa panya wengi, wanamsumbua sana, huku wakishambulia vitabu vyake kadhaa hasa kamusi zake.

 

Mwanakwetu akafika kwa huyu mama ambaye ni Binti Ngogo( Kwa wenyeji wa Lushoto hii familia ya Ngogo makazi yao ni vuli mlimani kama unakwenda Kwemashai). Huyu jamii pale Lushoto ana ndugu yake mmoja wa kiume huwa anazunguka mitaani Lushoto Mjini huwa anapiga kelele. Binti Ngogo huyu akampa paka mdogo mmoja mweupe, wakati anarudi akapita kwa ndugu mmoja anaitwa Bawji Athuman Mbwana, hapa akapita ili aombe paka dume maana yule wa awali alikuwa paka jike.

 

Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu fahamu hili:

 

“Bawji Athuman Mbwana ni ile familia iliyokuwa inamilika gazeti la SANI wakati likiwa jarida na huyu Bawji Athuman Mbwana alikuwa anagombea sana Ubunge kupitia CIVIC UNITED FRONT (CUF) huku akishika namba mbili na kura zake nyingi kama CHADEMA isingalikuwa inagombea basi Jimbo la Kigamboni na baadaye Mbagala leo hii tungesema Bawji amewahi kuwa Mbunge Kigamboni/ Mbagala lakini Bawji Athuman Mbwana hakubahatika na hili hadi akaamua kurudi CCM na kugombea Ubunge kura za maoni CCM na baadaye udiwani. Kwa wale wanaokumbuka CHADEMA alikuwa akigombea huyu Maulida Anna Komu. Baadaye Bawji Athuman Mbwana mwenye asili ya Tanga Mjini aliachana na siasa.”

 

Kumbuka Mwanakwetu anatoka kwa Jamila Ngogo ambapo ilikuwa eneo la Bondeni hapo Mianzini kisha anakwenda kwa Bawji ambapo kulikuwa mlimani kando la barabara kuu ya kwenda Chamanzi kufuata paka dume wa kufuga ili apambane na panya nyumbani kwake. Mwanakwetu akafika akapewa paka mdogo mweusi na walinzi wa nyumba hii kisha kumuweka katika mfuko na kupanda daladala kutoka Mianzini hadi Mbagala Rangitatu kisha Rangitatu hadi kwao Mbagala Sabasaba.

 

Mwanakwetu akiwa katika daladala zote alizopanda jioni hii abilia wanacheka huyu kijana mbona kabeba paka wanalia? Kondakta wa daladala ya kutoka Mbagala Rangitatu kwenda Tandika akawa anasema:

 

“Jamani achane kushangaa hiyo milio ya paka, watu wengine ndiyo wanajiandaa kuelekea kazini wakiwa na vitendea kazi vyao abilia wangu kuweni wavumilivu.”

 

Wakati huo hizo bodaboda ndiyo zinaanza, Mwanakwetu akafika Mbagala Sabasaba akashuka, kondakta akawa anamsindikiza Mwanakwetu kwa maneno:

 

“Kaka tunakutakia kazi njema…Kaka hongera sana kwa kazi hiyo.”

 

Mwanakwetu akaelekea nyumbani kwake Mbagala Bugudadi(Mbagala Baghadad) njiani paka hawa walikuwa wanapiga kelele awali njiani hakukuwa na neno lakini alipofika njia pande kwa Ndibalema(kulia) na Mbagala Kwa Selenge(kushoto) kuna nyumba moja ya mzee mmoja mwenyeji wa Morogoro ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM wa Tawi la Kizinga B anaitwa Chande, mzee huyu alikuwa barazani kwake akasema maneno haya:

 

“Wewe Mtoto wa Francis Makwega inakuwaje usiku huu umebeba paka katika mfuko?”

 

Huyu mzee Chande alisoma shule ya msingi na Baba wa Mwanakwetu na ndiyo maana alimtambua Mwanakwetu kwa jina la Baba yake (wewe mtoto wa Francis Makwega). Mwanakwetu alitoa majibu kuwa kwake kuna panya wengi hivyo anaenda kuwafuga ili wakapambane na panya hawa. Ndugu Chande akacheka mno kisha akasema paka wako wakizaa naomba jike na dume. Mwanakwetu akajibu kuwa hilo halina shida na kisha kuelekea nyumbani kwake. akaenda akavuka msikiti huku jamaa wanatoka kusali magharibi, mwendo kidogo akakutana na Mwalimu wake wa somo la Hisabati Darasa la Saba Shule ya Msingi Mtoni Kijichi(1990) miaka 24 nyuma , mama Bandio, mwalimu mmoja mwenye asili ya Mkoa wa Kagera, Mwalimu huyu yupo na mumewe mzee mmoja mrefu huku wanamsindikiza mgeni wao.

 

“Haya mwanafunzi wangu bora mbona paka wanalia mgongoni?”

 

Mwanakwetu jibu lake lilelile la kero ya panya anaenda kufuga, Mwalimu Bandio akasema wakizaa na mimi naomba. Mwanakwetu akajibu hakuna neno. Paka hawa walifika salama Mwanakwetu akawafuga vizuri na wakazaa watoto wengi wakiwa wa rangi mchanganyiko wengine nyeupe na nyeusi lakini watoto wawili mmoja alikuwa rangi nyeusi tupu kama baba yake na mwingine nyeupe tupu kama mama yake. Paka hawa wakachangamka na kazi ilikuwa ni kuwalisha, tabu ilikuwa Mwanakwetu akisafiri kwenda kutangaza Vipindi vya Leo Katika Bunge Dodoma, jirani yake mama mmoja wa Kihaya alikuwa na binti zake wawili ndiyo walikuwa wanaokoa jahazi, wanawapa chakula paka wa Mwanakwetu. Huku wakazoea nyumba hizi mbili : kwa Mwanakwetu na kwa mama jirani. Baadaye Mwanakwetu akachukua vitoto vinne akatafuta mfuko akaviweka na akapita kwa mwalimu Bandio na kisha kwenda kwa Mzee Chande kuwakabidhi paka wao. Maisha yakawa yanaendelea vizuri na yule paka dume mweusi alikuwa mkubwa sana watu wakawa wanamuogopa mno wakisema:

 

“Huyu paka mweusi wa Mtangazaji wa TBC Taifa jamani ni mweusi, paka huyu akikutazama anakuona hadi utumbo huku macho yake yanawaka kama kijinga cha moto.”

 

Wakati huo Mwanakwetu anajenga nyumba kubwa, hivyo basi nje ya eneo lake palikuwa vifaa kadhaa vya ujenzi nondo na mifuko ya saruji kama 100. Hakuna aliyediriki kuja kuiba hata mfuko mmoja wa saruji au nondo . 

 

 

Baadaye yule mama wa Kihaya jirani ambaye alikuwa Mkristo Mlokole akamwambia Mwanakwetu kuwa baba watu wanamuogopa huyu paka wako na ndiyo maana mifuko yako ya saruji na nondo zinapona wala haziguswi, wengine wanasema:

 

“Huyu jamaa ni mtu wa Tanga, hawa ni watu hatari sana, si unaona ameweka paka wake wa kazi wa rangi mbili nyeusi na nyeupe jaribu kuiba uone balaa la lile paka dume jeusi.”

 

Katika makazi haya kwa upande wa bondeni wa eneo la Mwanakwetu anapakana na mama mmoja anaitwa Donatea ambaye ni Binti Mangaya huku Ukoo wao ni maarufu sana wa Mbagala miaka mingi huyu mama kwa bahati nzuri walisoma pamoja na yule mzee Chande na Francis Makwega(baba wa Mwanakwetu). Donatea akawa anawaambia vijana:

 

“Msiogope hao paka anafuga tu kwa ajili ya kupambana na panya siyo paka wa ushirikina na huyu siyo mtu wa Tanga , huko Tanga ni nyumbani kwa mkewe, huyu Baba yake ni Mpogoro anaitwa Francis Makwega kwao Mbagala Sabasaba na mama yake anaitwa Dorothea Mgogo wa Dodoma/Singida, hawa watoto wanazaliwa ninawaona hawa ni watu wa Salaam Maria , umejaa neema, Bwana yu pamoja nawe…”

 

Kweli hali hii iliendelea hadi ujenzi unakamilika na paka wa Mwanakwetu mbegu yake ilisambaa eneo lote la Mbagala Bugudadi na huku paka wake wengine wakawa paka shume, baada Mwanakwetu kuhamia mikoani huku paka wengine wapo wanailinda nyumba ya Mwanakwetu ambayo kwa sasa inakaliwa na wapangaji, wapangaji wakiwa na ulinzi wa kutosha.

Hii simulizi siku ya leo Mwanakwetu ameikumbuka na kuamua kuandikwa na kuwa sehemu ya makala haya.

 

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Kwa hakika paka wa Mwanakwetu sasa wanatoa ulinzi kwa majirani zake huko Mbagala na huku Mwanakwetu amewakumbuka paka wale alipowapata kwa Binti Ngogo na kwa Bawji Othuman Mbwana mmiliki wa gazeti la SANI hapo Mbagala Mianzini.

 

Furaha ya Mwanakwetu siku ya leo ni moja tu paka wake bado wanatoa ulinzi kwa ndugu zake na hata akitaka kuwatumia tena paka wake pahala popote alipo hana haja ya kwenda Mbagala Mianzini bali anakwenda kwa wapangaji wake, kwa Mwalimu Bandio au kwa Mzee Chande ili awe na mbegu ya paka hawa hodari. Msomaji wangu kumbuka huyu siyo Jaji Mohammed Othuman Chande wa ripoti yake inayolalamikiwa. Msomaji wangu kumbuka leo hii Mwanakwetu amewakumbuka paka wake walinzi maana akitaka ulinzi yeye hana gharama.

 

Mwanakwetu anajua wapo wanaoweza kuwatumia paka hawa kwa manufaa yao kumbuka Mwanakwetu alivyo makini anakumbuka hata chanzo cha mbegu cha paka hawa alipowatoa.

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Wengine Wanakwenda Kazini na Vitendea Kazi Vyao.”

 

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

















 

0/Post a Comment/Comments