TUWAJALI WAJANE

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Mjane ni mwanamke aliyefiwa na mumewe; Mgane ni mwanaume aliyefiwa na mkewe.

Huku ikifahamika kuwa pale anapobaki hai mmoja wa wenza hao inawezekana kutakuwa na tunda la ndoa yaani watoto.

Katika hili vitabu vya dini vimekuwa vikisisitiza kuwajali na kuwathamini mno wajane. Kwa hakika katika kila mwanadamu awe mume au mke ni mjane au mgane tarajiwa hapa duniani hili kila mmoja atake asitake.

Biblia inasema:

"Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia na kutokuwa unajisi nayo."

Haya ni kulingana na Kitabu cha Yakobo 1, 27.

Nayo Korani inapaza sauti yake kuwa:

"Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake, wawausie wake zao wapewe matumizi ya mwaka mmoja bila kuondolewa nyumbani..."

Hii ni kulingana na Surah Al Baqarah 2:240.

Nao Waswahili wa Mbagala nduguze Mwanakwetu wanasema kuwa Yatima/mjane adeki maana hakuna wa kumfanyia hayo hapa duniani yu peke yake.

Kwa hakika msomaji wangu tumeona msimama wa Ukristo, Uisilamu na hata tamaduni za Waswahili wa Mbagala juu ya Mjane kila upande kwa nyakati tofauti ukimlitia maanani mjane.

 

Kutokana na hayo yote Mwanakwetu siku ya leo alitaka kujua mkoa wa Mara kwa  unafanya kitu gani juu ya maboresho ya maisha ya wajane? Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Bi. Neema Ibamba alisema kuwa wanawake wa Mkoa wa Mara sasa wamekihuisha Chama cha Wajane Mkoa huo huku wakihimizwa wajiunge na umoja huo maana ndani yake kuna fursa tele.

“Wanaweza kufahamiana na wajane wenzao, wanaweza kupata mikopo ya vikundi na hata kupata mikopo ya mtu mmoja mmoja, pia wanaweza kupata mbinu za kupambana na changamoto zao ikiwamo kurithiwa.”

Mwanakwetu akiongea na Bi Ibamba katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara nchini Tanzania alijiuliza hali ikoje katika mikoa mingine ya Tanzania?

Akilijibu swali la pili la Mwanakwetu juu Wagane mbona chama chao hakipo? Bi Ibamba alisema hata Wagane wakifika katika umoja wa Wajane hapa Mkoani Mara wanapatiwa baadhi ya huduma ikiwamo ushauri lakini pia uwepo wa Chama cha Wajane ni chagizo kwa wanaume kuona umuhimu wa kuwa umoja wa wagane.

 

Msomaji wangu nikuulize swali je hali ikoje katika eneo ulipo? Vipi kipo chama cha wajane/wagane?

Akizungumza kandoni mwa mjadala huu hapo hapo ofisini Mratibu wa Chama cha Wajane ambaye pia ni miongoni mwa Maafisa Maendeleo Mkoa wa Mara Bi Upendo Kiswaga amesema kuwa kwa Halmashauri ya Musoma chama hiki kina wanachama zaidi ya 200 huku akina mama wajane wengi wanaendelea kujitokeza kujiandikisha akihimza wajane wasisite kujiunga na wakati ni sasa.

 

Baada ya majibu haya ndipo Mwanakwetu akaamua kuyaandika makala haya.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Juni 23 ya kila mwaka ni siku ya wajane duniani ambapo wanawake milioni 258 ulimwenguni wanakadiliwa kuwa ni wajane wakiwa na watoto zaidi ya milioni 584 ambapo wanatunzwa na wanawake hawa hawa wajane. Jumla ya wajane na yatima inakadiliwa ni kuwa milioni 842 ambayo inaweza kufika bilioni 1 muda si mrefu, hii ni idadi kubwa ya watu wenye changamoto duniani ambapo hawa yatima wanapitia kipindi kigumu mno. Takwimu hizo zinagonga kengele ya hatari kuwa nusu ya wajane ulimwenguni wanaishi katika umasikini wa kutupwa.

Kwa Tanzania takwimu hizo zinadokeza kuwa asilimia 4.7 ni ya wajane/wagane na huku idadi hiyo inaongezeka kila uchao. Katika haya yote ndiyo maana Mwanakwetu anaamini kuwa:

“Dini safi mbele za Mungu ni kuwatembelea na kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao.”

Kama Biblia ilivyodokeza katika Kitabu ya Yakobo 1.27. Kwa hakika Juni 23 ya kila mwaka ni siku ya wajane ulimwenguni hapa ifahamike wazi kuwa wajane na wagane hawaishi siku moja tu katika mwaka, hivyo basi mtu mmoja mmoja, taasisi binafsi na serikali katika kila taifa na hata mashirika ya kimataifa kila mmoja atimize wajibu wake kumfikia mjane/mgane na yatima aliye jirani naye.

Mwanakwetu Upo?

Makala haya ya Mwanakwetu yameandikwa kwa heshima ya Bi Misambo Gambona ambaye ni Mwandishi Mwendesha ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara.

Kumbuka:

“Tuwajali Wajane.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257














 

0/Post a Comment/Comments