Tume Batili na Ripoti Haramu

 

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Aprili 25, 2026 Mwanakwetu alikwenda pahala kununua bidhaa kadhaa, wakati anarudi aliamua anywe chai katika mkahawa mmoja wa makabwela, aliingia na kuagiza chai hiyo, mkahawani kulikuwa na watu watatu; mhudumu na wateja wawili baadaye aliongeza mhudumu wa pili sasa kukawa na watu wanne.

Mwanakwetu akiwa hapa mteja mwenzake anakunywa chai huku mikono yake miwili inatetemeka sana, akijitahidi kubeba kikombe kwa tabu nacho kikombe kinacheza sana huku mkono wa pili ambao unatetemeka ukimsaidia hivyo hivyo kuisogeza chai hiyo hadi kunywani na kisha kuchukua kipande cha chapati kukipeleka mdomoni.

Mwanakwetu anakunywa chai huku moyoni akisema Mungu mjalie huyu jamaa apone.

 

Wateja mkahawani hatuongei kitu zaidi ya ile salaam ya awali tu lakini nje ya eneo hili kulikuwa na watu wanaongelea Tume ya Matukio ya Oktoba 29, 2026 na siku zilizofuata:

“Wewe uliona wapi mahakimu wa Tanzania wanatenda haki? Sebuse JAJI! Haki ya Tanzania ni pesa yako tu.

Yaani wale waliofariki Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ndiyo basi tena hakuna lolote pale, hawa jamaa zetu siyo watu wema.”

Hapa Mwanakwetu akanywa chai yake na kutoka zake kuanza kurudi alipokuwepo awali, akiwa njiani akasema moyoni:

“Waliofanya upuuzi huu hawana amani huku jamii bado inawakumbuka wapendwa wao hivi hii hali inatoa tafsiri gani?

Viongozi hawaaminiki na maswali ya majibu hakuna.Taifa linakwendaje kwa hali kama hii?”

Hapo hapo Mwanakwetu aliamua kumpigia simu ndugu yake mmoja ambaye anashahada mbili za habari: ile ya Shahada ya Sanaa ya Habari na Shahada ya Uzamili ya Habari na huku akiwa mjuzi wa masuala ya Ulinzi na Usalama wa Ndani na ya Kimataifa. Ndugu huyu aliyasema haya:

“Hii ripoti ni kama inafunika kombe mwanaharamu apite tu na hailengi kulikombea taifa hili bali ni kusaidia kikundi cha watu wachache tu waonekane wema.

Angalia idadi ya watu waliouwawa mitaani na takwimu zao ni kichekesho kabisa maana hauwezi kutuhumiwa wewe kisha uje na taarifa nzuri. Nina Imani na Watanzania ni wastamilivu na tuombe Mungu tupite salama katika hili.”

Mwanakwetu alimuuliza mwanahabari huyu juu ya hali ya Kupiga Kura inaweza kurejea katika chaguzi zijazo?

“Hii ripoti imeongeza chuki kwa wananchi maana Watanzania wamebadilika siyo wale kuhongwa vitu vidogo vidogo maana naona wale watakaoshiriki chaguzi zijazo ni wachache mno watakuwa wale watakaotumika tu.

Hata Katiba Mpya kupatikana mapema hakuna dalili. Sasa Tanzania haina mahakama imara, hawa majaji kana kwamba wanatumika tu tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Jacob Mwambegele ..Hawa Majaji wa Mahakama Kuu kwa Tanzania nafuu ya Majaji wa zamani walikuwa wakweli lakini Majaji hawa tuwe nao makini. Hivi hatuoni? Hauwezi kutangaza matokeo wakati intaneti imezimwa hii nchi ni kubwa. Kura hizo zilipigwa na nani? Wapi? na lini? Au walijiandaa na matokeo yao na mshindi wao?”

Mwanakwetu pia aliuliza je vipi kwa wale Watanzania waliotekwa ambao mustakabali wao haujulikani huku tume inasema watu wametekwa kwa wivu wa mapenzi?

“Hauwezi wewe kuwa mtuhumiwa na kisha ujichunguze mwenyewe hata haya maelezo ya wivu wa mapenzi yanaondoa uhalisia wa matukio ya utekaji, Watanzania wakiongelea utekaji wanakamatwa na kufungia nyumba zao za ibada mathalani Askofu Dkt.Josephart Gwajima.

Hivi kwlei Humphrey Polepole na Mdude Nyagachi walitekwa kwa hoja ya mapenzi ? Haigii akilini. Huyo mwanamke wanayemgombania ni nani?Huyu mwanaume wanayegombania naye mapenzi mbona hajakamatwa? Hili siyo kweli. Tume batili na Ripoti halamu.

Msomaji wangu, haya ni mahojiano ya Mwanakwetu na mdau mmoja wa habari na mambo ya Ulinzi na Usalama wa Ndani na Kimataifa ambapo mahojiano haya yalifanywa na Mwanakwetu baada ya kusikia zile hoja za vijana nje ya mkahawa wakijadili kwa kumrushia tuhuma tele Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Othman Chande na Mahakama ya Tanzania.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Msomaji wangu mkumbuke yule mteja mwenzake Mwanakwetu aliyekuwa anakunywa chai kwa tabu mkahawani huku viungo vyake vikitetemeka kwa maradhi. Taswira hii Mwanakwetu anaibeba na kuilinganisha na Tanzania ya mwaka wa 2025/ 2026tangu viongozi na wananchi sote tuna maradhi makubwa ya kilichotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata. Sasa hivi kila linalofanyika ni kwa mashaka kama alivyokuwa huyu mteja hapa mkahawani, lazima maradhi ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata yapatiwe ufumbuzi vinginevyo hali ya Tanzania haiwezi kutengemaa milele. Kwa hali kama hii watu wanauwawa kwa wingi kisha hakuna kinachofanyika unadhani Watanzania wanaweza kujitokeza kwa amani katika mambo ya umma? Hili ni gumu, Je Tanzania inakwenda hivi hadi lini? Hii ni tafakari ya Mwanakwetu siku ya leo.

Mwanakwetu Upo? Kumbuka:

“Tume Batili na Ripoti Haramu.”

Nakutakia Siku Njema

makwadeladius@gmail.com

0717649257









 

0/Post a Comment/Comments