Siku Njema Huonekana Asubuhi

 

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Siku hii alifika Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukagua mradi mmojawapo wa Michezo nchini Tanzania, kwa bahati nzuri Naibu Katibu Mkuu aliambatana na viongozi wa Wilaya hii akiwamo Mkuu wa Wilaya. Mkuu wa Wilaya akawa mkali kidogo akasema maneno haya:

“Huu mradi ni Wizara ya Utamaduni, Sanaa na michezo na upo katika wilaya yangu, kila tunapotaka kuuingiza katika miradi ya Mwenge kila mwaka tunashindwa maana, mradi huu una shida kadhaa, kwanza haumaliziki kwa wakati, miaka nenda miaka rudi, ukija hapa mkandarasi hayupo. Kila ukija majibu anatoa Mkandarasi wa Mkoa wa Mwanza, sasa zege wanapandisha kwa ndoo gorofani na isitoshe gharama za mradi zinapanda kila mwaka, shida nini? Kila nikija hapa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Utamaduni Sanaa na Michezo analalamika hoo unaniharibia, ninamuharibia nini?”

Msomaji wangu kumbuka Katibu Mkuu wa Wizara hii aliyetajwa na Mkuu wa Wilaya alikuwa amehamishiwa Wizara nyingine.

Msomaji wangu katika wahusika hao Katibu Mkuu anayetajwa alishahamishiwa wizara nyingine kama nilivyodokeza Mwanakwetu anamfahamu, Naibu Katibu Mkuu Mwanakwetu alikuwa anamfahamu zaidi, huku Mkuu wa Wilaya anamfahamu tangu akiwa Katibu Tawala wa Wilaya. Siku hii jambo hili lilimkera sana Mwanakwetu ambaye alikuwa hapo kama mwanahabari tu, akajiuliza moyoni kwani huu mradi wa baba yake huyo Katibu Mkuu? Moyoni Mwanakwetu alijijibu huu mradi ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwanini watu wafanye miradi ya umma kama yao? Huku usimamizi siyo mzuri? Hata baada ya hapo hakuna kilichofanyia mambo yalikuwa hayo hayo.

 

Hali ya usimamizi wa mradi huo ulibaki hivyo hivyo na hata kama mradi huu utakuwa umekamilika ni kwa kiwango cha chini na kwa gharama kubwa.

Katika hii la miradi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa hakika ipo shida kubwa sana ambayo kuivumilia ni kuwapa mzigo Watanzania, nakuomba msomaji wangu nikwambie hoja hili:

“Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo inayo rasimali watu ambayo ina uwezo wa kusimamia miradi mikubwa? Wizara hii imeshawahi kuwa miradi mikubwa? Inakuwaje serikali inapeleka miradi mikubwa wakati rasilimali watu ni ile ile?

Tangu kwa Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbas, Balozi Said Yakub na Gerson Msigwa mamlaka ya uteuzi inao ushahidi kuwa hawa ndugu waliwahi maishani mwao kusimamia miradi mikubwa kama hiyo? Mamlaka ya uteuzi inao ushahidi kuwa hawa ndugu wanao uwezo wa kusimamia vizuri rasilimali watu katika maisha yao? Hawa ni Watanzania wenzetu, tunawapenda, inawezekana ni watiifu sana kwa mamlaka lakini jamii inawafahamu vizuri ukiwatazama sifa hii ya usimamizi wa rasimali fedha hawana, usimamizi wa rasimali watu hawana rekodi hiyo na usimamizi wa miradi mikubwa wanakosa sifa hiyo na huko ni kuweka rehani rasimali fedha za Tanganyika maana Wizara hii siyo ya mambo ya Muungano.”

Katika ripoti yake Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania Dkt Charles Kichere, kaka yetu huyu anasema maneno haya:

“Wakati wa utiaji saini wa mkataba wa Uwanja wa Arusha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo hawakuwa makini.”

Haya maneno siyo utani, ni kweli na lazima wahusika tushugulike nao mmoja baada ya mwingine.

 

Kama taasisi hii ya umma hawakuwa makini wakati wa kusaini mkataba, je watakuwa makini katika kusimamia mradi? Watu wa Mbagala tunaamini Siku njema Huonekana Asubuhi. Hawezi kuwa makini hapo wataendelea kupiga ugali mbichi na ugali huo mbichi lazima wale wao wenyewe. CAG ametaja mradi wa Kiwanja cha Arusha tu lakini ukifanya utafiti kampuni inayofanya kazi nyingi ni ile ile yaani Mkandarasi yule yule na huku Mshauri Elekezi ni yule yule na hapa ndipo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ilivyojichanganya zaidi na kujikaanga na mafuta yake yenyewe.

Naomba msomaji wangu nilieleze vizuri jambo hili:

“Mathalani Mwanakwetu ana jenga miradi yake mitano ya Soko (2.5 Bilioni), Jengo la Makazi(1Bilioni), Hoteli(5 Bilioni), Shule ya Sekondari(2 Bilioni) na Chuo cha Ufundi 3 Bilioni). Miradi yote ni ya jumla ya shilingi Bilioni 13.5 na kazi zote Mkandarasi ni Msemakweli & Sons na huku Mshauri Elekezi ni Kikulacho&Sons.”

Hiki ndicho kilichofanywa na Wizara hii, haiwezekani miradi yote iwe inafanywa na Mkandarasi huyo huyo na Mshauri Elekezi huyo huyo

Tetea Makini Hatagi Mayai Katika Kiota Kimoja, sasa kuna haja gani ya kuwa Wakandarasi wengi na kuna haja gani ya kuwa na Washauri Elekezi wengi? Ukitafiti utabaini Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo mara nyingi inamuhusudu Mshauri Elekezi mmoja Kampuni cha Chuo cha Ardhi. Kwanini iwe kampuni hii tu? Mwanakwetu anafahamu mara nyingi Mshauri Elekezi katika taasisi za umma huwa inapendeza kuwa kampuni za Serikali ambapo gharama zake huwa nafuu, hili halina ubishi lakini ubishi unakuja kampuni zingine za serikali hazipo?Kwani tuzinyime kampuni binafsi? Hapa Mwanakwetu anafahamu gharama huwa juu hadi asilimia 10 ya mradi mzima. Mwanakwetu anatambua kuwa kuwa Bodi ya Wakandarasi na hata Msajili wa Wakadiliaji Ujenzi (AQRB) huwa zinasaidia mno katika kuyaweka mambo sawa lakini Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na michezo imejichanganya kuwapa kazi nyingi taasisi zile zile, hapa wamepika wali mbichi.

Mwanakwetu haya anayaandika kwa heshima ya CAG Dkt Charles Kichere tu, vinginevyo angekuwa bubu maana watu sasa hatuaminiani katika taifa letu wenyewe.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Shida ya maamuzi haya ni zifuatazo:

“Mkandarasi na Mshauri Elekezi wanalindana madhaifu yao kwa mfano Mkandarasi anaondoka site muda kadhaa ukiuliza malipo yamechelewa. Hapa ndipo kinachoonekana. kwanini malipo yachelewe? Kama siyo mbinu ya kukaribisha penati zisizo na maana? Kuongeza gharama za miradi Kwanini tunaanzisha mradi hatuna pesa? Hili likiwa tatizo ya miradi mingi ya wizara hii, wakandarasi hawapo kwenye miradi huku gharama zikipanda maradufu na miradi kutoka kamilika kwa wakati.”

Sasa hoja ni moja kama Mshauri Elekezi anafunga ndoa na MKANDARASI hiyo siyo ndoa bali ndoano. Kinachotakiwa kufanya mamlaka ya uteuzi inaweza kujua kuwa Wizara husika tumepeleka miradi mikubwa, pesa za malipo ya miradi zilipwe kwa wakati huku mkiboresha rasilimali watu katika wizara husika kama katibu Mkuu au Naibu Katibu Mkuu lazima mmoja awe na ujuzi wa mambo ya ujenzi akae hapo hadi miradi ikamilike.

Haya Mwanakwetu anayaandika ni kwa heshima ya kaka yake tu Dkt. Charles Kichere vinginevo alingeamua kukaa kimya viwanyo na iwe maana watu hamuaminiki.

Mwanakwetu Upo?Kumbuka:

“Siku Njema Huonekana Asubuhi. ”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257











 

0/Post a Comment/Comments