Osie Baba Ushezachepuka

 


Adeladius Makwega-MBAGALA.

Aprili 21, 2026 ilikuwa siku ya kuchekesha kidogo Mwanakwetu alikuwa mufilisi sana na ili kujipa faraja alipita katika mitandao ya kijami kusoma kulikoni? Siku hii alipita huku na kule na kisha kuweka kambi katika ukurasa wa Rashidi Shangazi ambaye ni mbunge wa Mlalo huko Lushoto Mkoani Tanga. Hapa alizikagua na kuzisanifu picha kadhaa zikiwa na maudhui mbalimbali, picha moja baada ya nyingine.

Katikati ya hayo Mwanakwetu alikutanana picha ambayo inamuonesha mhe.Rashidi Shangazi akiwa kavaa kanzu maridadi huku akiingia bungeni, hapa Mwanakwetu akasema naam huyu ni Ustadhi Rashid Bini Shangaza wa Mlalo akiingia ndani ya bunge tukufu.

 

Mwanakwetu akapita huku na kule kisha akakutana na picha ya mheshimiwa Shangazi akiwa na ustadhat mmoja. Unajua macho ya Mwanakwetu ni ya uzee na siku hii miwani yake kaisahau nyumbani kwake, kurudi nyumbani kwake kuichukua ilikuwangumu maana bei za usafiri wa bodoboda nauli zimepanda mara dufu zimepanda sana, hivyo akaamua kukaa siku nzima bila miwani yaani anasoma maandishi kwa tabu mno .

Baadaye Mwanakwetu alipotazama picha hii vizuri aliwaona hawa ndugu wamependeza kweli kweli, hapa akajiuliza huyu ni mke wa mheshimiwa Shangazi? Mwanakwetu akasema mke wa mheshimiwa Rashidi Shangazi anamfahamu na alishamuona kule Mlalo mara mbili na pia nyumbani kwake pale Dodoma mara tatu, jumla kuu mara tano hata kwa mbali mke wa mheshimiwa huyu hawezi kumsahau .

Picha hii ikamvutia zaidi Mwanakwetu hivyo akakata shauri akisema ngoja atampigia simu mheshimiwa Rashidi Shangazi ili Mwanakwetu apatiwe namba ya simu ya huyu mama aliyependeza sana ili amsalimie. Baadaye Mwanakwetu alibaini kuwa Mheshimiwa Rashidi Shangazi alikuwa amepiga picha na Mkuu wa Mkoa wa Tanga mheshimiwa Batilda Buruani.

 

Mwanakwetu akasema moyoni lo salale mie mtoto wa Makwega naomba namba ya simu ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga? Hivi hapa najitakia mema? Asije akasema huyu anaifanyia mzaha serikali. Huyu anaifanyia mzaha Kamati ya Ulinzi na Usalama, huyu anamfanyia mzaha Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa. RPC mkamate muwekeni ndani. Mwanakwetu akawa mpole huku moyoni akisema:

“Batilda Buruani kaolewa Zanzibar na kweli mie Mpogolo wa Mbagala sina utani na Wazanzibari.”

Hapa Mwanakwetu akasema hataki hekaheka za Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na hataki ugomvi na Wazanzibar. Mwanakwetu akabaki nalo moyoni lile jambo lake la kuomba namba ya simu ya mama aliyekuwa kando ya Mheshimiwa Rashidi Shangazi. Mwanakwetu akasema fina li lai ngoja niendelee kukagua ukurasa wa mheshimiwa Rashidi Shangazi maana mtembea bure siyo mkaa bure huenda akaokota…Gafla Mwanakwetu akakutana na picha nyingine ya mheshimiwa Rashid Shangazi kavaa suti ya rangi ya samawati na mrembo kando yake, Mwanakwetu aliitazama picha hii akaipenda sana huku akijiuliza huyu aliyepiga picha ya Rashid Shangazi ni nani? Je ni mkewe? Mwanakwetu alimtazama vizuri huyu mrembo baadaye alitambua kuwa huyu siyo mke wa mheshimiwa Rashid Shangazi .

 

Mwanakwetu akanasa katika picha hii mithili ya ndege aliyenaswa katika ulimbo.

Kazi ya Mwanakwetu ikawa ni kusoma ujumbe wa waliyotoa maoni katika picha hii mmoja baada ya mwingine. Ujumbe mmojawapo ulikuwa wa Ali Kizigha yeye aliyasema maneno haya:

Mghoshi uyonndai mzaighanana”

Hapa akimaanisha mheshimiwa/kaka huyo ni nani mbona mmefanana? Maoni haya yalikuwa ya Lugha ya Kisambaa huku maoni mengine yalikuwa ya lugha tele Mwanakwetu yeye aliyahusudu maoni ya Kisambaa tu alisoma maoni kadhaa na hapa alikutana na ujumbe wa Yusuph Salim yeye aliyasema maneno haya:

“Osie baba ushezachepuka.”

Haya ndugu Yusuph Salim hapa alikuwa anamaanisha kuwa mheshimiwa/kaka vipi umeshaanza kuchepuka? Hapa Mwanakwetu alipoyasoma maoni yote alibaini kuwa huyu aliyepiga picha na Mheshimwiwa Shangazi ni pengine ni mbunge mwenzake wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na picha hii ilipigwa nje ya Bunge hili. Mwanakwetu alivutiwa na picha hii na akitaka kujua jina la  mheshimiwa huyu na anatokea Mkoa gani?  Mwanakwetu anakula kiapo kwa wasomaji wake kuwa ataomba namba ya simu ya mheshimiwa huyu mrembo huyu kupitia kwa Rashidi Shangazi na mhe Shangazi asipotoa ushirikiano Mwanakwetu atazungumza na Spika Idd Azan Zungu na namba ya simu itapatikana tu.

“Hapa siogopi maana uwoga wangu uliishia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na kwa Wazanzibari tu.”

Hii ni pitapita mitandaoni ya Mwanakwetu Aprili 21, 2026 ambayo ilifikisha kwenye picha hiyo ya mheshimiwa Rashidi Shangazi na Mbunge mwenzake.


 

Najua wasomaji wangu msije kuniambia kama walivyosema wapiga kura wa Mheshimiwa Rashidi Shangazi kusema:

“Osie Baba Ushezachepuka.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu akiipata namba hiyo ataongea na huyu mheshimiwa kisha atamkaribisha atembelee kwao Mbagala ili akapunge upepo wa Bahari ya Hindi kule mtoni Kijichi kisha atampeleka Kigamboni akaone Wanyama pale Dar es Salaam Zoo alafu atapata fursa ya kuogelea kando ya makutano ya Mto Mzinga na Bahari ya Hindi ili aoge maji ya chumvi ili apate Baraka za Pwani ya Tanzania awe mbunge wa Bunge letu kwa miaka mingi. Kisha Mbunge huyu atapelekwa Mahenge akatembelee Mbuga ya Selous kama huyu ni shemeji yetu mheshimiwa Rashidi Shangazi ninatanguliza samahani tele.

 

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Osie Baba Ushezachepuka.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257









 


 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments