Katika maisha ya mwanadamu duniani, Mwenyeenzi Mungu anatoa nafasi ya kiumbe hiki kuishi katika uso wa dunia, swali ni moja tu je unapoondoka unaacha alama gani ambayo inakuwa mwongozo wa kumsaidia binadamu mwenzako kupita salama katika dunia hii?
Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza.“Wapo ambao wanaweza kuiachia dunia miba na mbigili juu ya nyao zao na hata hakuna mwanadamu anayetamani kupita mle walipokanyanga.Je nyayo zako zinakanyagika na kumfikisha mwanadamu mwenzako pahala salama?”
Lazima tujitahidi kuacha nyayo salama zinazokanyagika na kumfikisha mwenzako pahala salama.
Hii tafakari inamjia Mwanakwetu wakati akiyatazama maisha ya Mhashamu Askofu Antony Petro Mayala ambaye katika uhai wake alikuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma Februari (12, 1979) na baadaye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza (Novemba 18, 1987) ambapo historia inadokeza alizaliwa Kijiji cha Ibindo Kwimba Mkoani Mwanza Aprili 25, 1940 na kufariki Agosti 19, 2009.
“Mhashamu Antony Mayala alikuwa ni Askofu aliyeamini kuwa huyu mwanadamu ili aweze kujikomboa na kumfahamu Mungu ilihitaji apate elimu, hivyo aliamua kuweka misingi ya kujenga taasisi kadhaa za elimu ambazo sasa zinatoa elimu tangu shule za msingi hadi vyuo vikuu, shule maeneo ya vijiji na mijini ilikusaidia kumkomboa mtoto kike kwa kiume hususani Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza.”
Haya ni maelezo ya Padri Abel akizungumza kwa njia ya simu akiwa nchini Uganda ambapo alikuwa huko katika ziara maalumu ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Askofu Mkuu Antony Mayala iliyopo Ibindo Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza wakiwa katika ziara za kimasomo.
Kwa hakika unapolitazama Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza ni jimbo lenye wakulima na wafugaji wakiheshimu mno jembe na Ng’ombe.
“Wasukuma wanaheshimu mno mifugo huku wakisisitiza mifugo hiyo kupita sehemu sahihi, japokuwa ina umuhimu mkubwa ni nadra mno kusikia mfugaji kapitisha mifugo katika shamba la mkulima. Ndiyo kusema nyayo za mifugo huwa zinapita njia sahihi kuelekea machungani maana mfugaji anahitaji ugali ili ale na nyama au maziwa nayeye mkulima anahitaji nyama na maziwa ili ale na ugali wake wakitegemeana mno huku maisha ya mkulima na mfugaji sehemu kubwa ya Mwanza ni kidugu.”
Kama ilivyo nyayo za mifugo zinavyotakiwa kupita njia sahihi, ndivyo alivyo binadamu anatakiwa kupita njia sahihi katika maisha yake pale anapopata elimu ili kumuongoza kufika pahala sahihi.
Hii ndiyo ilikuwa falsafa ya Mhashamu Antony Mayala, hii ndiyo alama ya Mhashamua antony Mayala na alama za Mhashamu Antony Mayala zipo tele, hizi ni nyayo(hatua)zinawanufaisha wana Mwanza iwe katika sekta Afya na Elimu na hadi leo hii nyayo mojawapo ni uwepo wa Shule ya Wasichana ya Askofu Mkuu Antony Mayala iliyopachikwa jina lake ambapo inawanufaisha wasichana wa eneo hili na maeneo mengine ya Tanzania wakipata elimu bora huku ikifanya vizuri kitaaluma.
“Shule yetu inatoa elimu ya sayansi, Sanaa, lugha na masomo mengine huku wanafunzi wanajifunza mbinu mbalimbali za maisha wakijengwa na malezi bora ya kiroho.”
Haya yakiungwa mkono na Padri Abel miongoni mwa walezi wa shule hii.
Kwa mwaka wa 2026 shule hii iliamua kufanya ziara nchini Uganda ili kutoa nafasi ya wanafunzi wao kujifunza mambo kadhaa ya kitaalamu na ya kiroho katika taifa hili la Uganda , taifa ndugu na Tanzania kwa pamoja wakiwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tulitembelea taasisi kadhaa ikiwamo shule ya Wasichana ya Mtakatifu Aloysius iliyopo Masaka, pia tulifika shule ya Sekondari ya Divine Mercy iliyopo Fort Portal, kisha tukafika Shule ya Bright Future iliyopo Kampala na mwisho kutakifika Chuo Kikuu cha Mashahidi wa Uganda ili kuongeza maarifa zaidi ya kitaaluma.”
Padri Abel alisema kuwa Shule ya Wasichana ya Askofu Mkuu Antony Mayala inayo sifa kubwa ya kusomesha kwa umahiri lugha kadhaa za Kimataifa ikiwamo Kiingereza, Kifaransa, Kichina na Kiswahili ambalo hili limekuwa jambo la msingi kwa sasa ambapo dunia imekuwa kama kijiji kimoja. Je kama dunia ni kijiji utawasiliana kwa kutumia lugha gani? Padri Abel aliuliza akisema umahiri wa lugha ni jambo la msingi.
Wakihitimisha juu ya ziara yao nchini Uganda ya siku 10 Aprili , 2026 Padri Abel alisema kuwa pia walifika eneo la HIJA la NAMUGONGO kuwakuza kiroho wanafunzi wao ambapo mashahidi wa Uganda waliuwawa na Kabaka Mwanga wa II wakati wa mwanzo mwanzo wa Ujio wa Wamisionari eneo hili la Afrika ya Mashariki.
“Elimu ya Tanzania ipo vizuri kwa sasa kwa kuwa mwanafunzi anapata fursa ya kuchagua kusoma masomo akiingia kidato cha tatu ambapo nchini Uganda wanayasoma yote, hapa hoja ya uchaguzi wa masomo mapema ni muhimu unamuongoza mwanafunzi kuweza kufanya vizuri kitaaluma na kufikia lengo lake baada ya kuchagua mchepuo husika.”
Hii ilikuwa ni tathmini ya jumla ya taasisi hii wakiwa ziarani nchini Uganda.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Shule ya Wasichana ya Askofu Mkuu Antony Mayala ni miongoni mwa shule chache za Kanisa zilizoanzisha maeneo ya vijijini katika Jimbo Katoliki Kuu Katoliki la Mwanza. Kwa utafiti wa Mwanakwetu akiwa Mwanza aliambiwa na wenyeji kuwa Askofu Mkuu Antony Mayala akiwa hai alihimiza mno watoto wa kike wapate elimu zaidi ya wavulana au kama ilivyo kwa watoto wa kiume maana mwanamke ndiyo hukaa na watoto muda mrefu kuliko mwanamme na huku baadahi ya jamii hata mgao wa urithi kama vile mashamba na mifugo wanawake wamekuwa hawapati japokuwa mabinti wamekuwa wakizingizi koo zao makundi makubwa ya ng’ombe kama posa, hapo ndiyo maana shule hii ilikuwa ya kwanza kuanzishwa ukanda huo.
Kwa hakika Shule ya Wasichana ya Askofu Mkuu Antony Mayala ni Nyayo zisiyofututika za kiongozi huyu wa kanisa aliyefariki mwaka wa 2009.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Nyayo Zisifutika Za Mhashamu Antony Mayala.”
Nakutakia Siku Njema
0717649257









.gif)
.gif)
Post a Comment