Adeladius Makwega-MBAGALA.
Aprili 5, 2026 ni Sikukuu ya Pasaka Ulimwenguni ambapo Wakristo tunasherekea Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo. Kwa desturi Mwanakwetu huwa hatayarishi makala yoyote maana hutoa nasafi ili Wakristo wenzake wausikie ujumbe wa Pasaka ambao mara nyingi hutolewa na Maaskofu kutoka majimbo na Dayosisi mbalimbali tangu siku ile ya Ijumaa Kuu na hata kama Jimbo Fulani ni wavivu wa kutumia vyombo vya habari lakini wakati wa Pasaka hilo hufanyika vizuri , hapa makala za Mwanakwetu zinakuwa likizo.
Siku hii mara baada ya Mwanakwetu kusali na kurudi anapoishi aliwasiliana na rafiki yake wa miaka mingi, huku walizungumza mambo mengi na ndani ya mijadala yao kulikuwa na jambo ambalo linagusa ustawi wa maisha ya Mtanzania mmoja mmoja kwa mwaka wa 2026 , jambo jili likamsukuma Mwanakwetu kuamua kuyaandika makala haya.
Kwa yule msomaji wa makala za Mwanakwetu kwa miaka mingi hili analifahamu vizuri lakini wasomaji wapya hilo naomba ulifahamu kuwa wakati wa Sikukuu za Kanisa Mwanakwetu kalamu yake huwa anaiweka chini, leo Mwanakwetu kalamu yake inaandika.
Mwanakwetu alimuuliza huyu ndugu yake ambaye ni Daktari wa Falsafa, amefundisha vyuo vkuu kadhaa huku aliwahi kuwa kiongozi vya ngazi ya Halmashauri na Mkoa juu ya changamoto ya mafuta kupanda nchini shida ni nini? Ndugu huyu aliyajibu haya:
“Ukiangalia tangazo la EWURA utabaini kuwa Mkurugenzi wa EWURA mbele ya waziri mwenye dhamani hiyo alitoa taarifa ya mafuta yaliyomo katika matanki yetu, huku akisema mafuta haya yanaweza kutumika kwa miezi mitatu ijayo.
Katika biashara ya mafuta hilo halitumika maana biashara ya mafuta tayari ina kanuni zake, bila kuuliza kwanini kanuni hiyo ipo hivyo. Hii kanuni ni kama vile zile kanuni za PAI katika hesabu.
Vita ikitokea au upungufu wa mafuta ukitokea unalazimishwa kutumia kanuni ya dunia ambapo lazima mtangaze bei iliyopo sokoni .”
Kwa maelezo haya Mwanakwetu anaona kuwa inaonekana wazi kuwa wakati aliyekuwa Mkurugenzi wa EWURA Dkt. CPA James Andilile Mwainyekule anaongea Waziri mwenye dhamana na Nishati nchini Tanzania ndugu Deogratius John Ndejembi alikuwepo na ndiyo maana aliyekuwa Mkurugenzi wa EWURA alikuwa akirudia sana maneno haya mawili- mheshimiwa waziri-mheshimiwa waziri.
Huki utenguzi wa Dkt Mwainyekule peke yake ni kama kumuonea, vipi mbona Waziri mwenye dhamana anabaki salama?
Kwa wale ambao hawamfahamu huyu Waziri Ndejembi ni mchanganyiko wa mama wa Kizanzibari na baba yake ni Mgogo wa Chamwino. Wale wenyeji wa Chwamwino wa asili huwa wanasema maneno haya:
“Deo Ndejembe siyo Mnyausi bali Mkonongo.”
Hapa wakimaanisha huyu waziri siyo mgogo asilia bali ni mgeni.
Haya msomaji wangu juu ya Deo Ndejembi yalimjia akilini tu Mwanakwetu wakati anaongea na simu hii.
Mwanakwetu akamuuliza msomi huyu kuwa kama hali ya Mafuta ni hivyo, sasa kipi cha kufanya kwa Taifa la Tanzania?
Msomi huyu aliyajibu haya:
“Ambacho kinafanyika mnaangalia mataifa ambayo yana hali sawa na nyinyi, wao wamefanya nini? Mathalani Malawi, Nambia na Ufaransa . Wenzetu Ufaransa wamewasiliana na Serikali ya Iran na meli zao zimepita salama na zimefika Ufaransa na sasa wao wana mafuta.
Kwa taifa la Namibia wao walichokifanya wametoa ruzuku kwa wafanyabiashara wao na mafuta yamenunuliwa .
Kwa Tanzania tuna matajiri sita ambao wameingia katika mktaba na serikali, kazi yao ni kuleta mafuta wanayaingiza nchini kisha mafuta yao wanawapa wale wasambaza ili yaweze kuwafikia wale wauzaji wadogo wadogo.”
Jambo jepesi kwa Tanzania kwa sasa kulingana na msomi huyu ni kutoa ruzuku kwa wafanyabiashara hao wakubwa wa mafuta. Je Tanzania inalifikiaje hili?
“Mwaka wa fedha ndiyo unafika ukingoni ambapo zimebakia siku 85 huku bajeti tulizopangwa kisheria kuwa tutakusanya hiki na tutatumia hiki. Je wapi pesa zitapatikana? Wapi tujinyime kama zinatakiwa Bilioni 200 nani anyimwe pesa ? Mathalani Labda RAS MARA, RAS Mtwara, RAS Lindi au RAS Singida kisha pesa hizo zikusanywe vizuri ili tuwape hawa matajiri.
Kuyafanya yote haya lazima yaingizwe bungeni kuwa kama Bilioni 200 au 300 zisiende mikoani hapa lazima Waziri Mkuu aingize muswaada huo Bungeni.
Kama hili ni gumu basi Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania aende kwa Balozi wa Irani akazungumze naye ili meli za mafuta zinazokuja Tanzania zipite salama kwa kupewa ulinzi ili hawa matajiri wasiingie hasara. Hakuna tajiri atakayekubali meli yake yenye mafuta ipigwe mabomu.”
Haya msomaji wangu ni mawazo ya Watanzania ambao wapo Serikalini. Hoja ni moja haya ni mawazo mazuri ili yaweze kutumika lazima huyu anayetoa hoja hizo umempa nafasi? Lazima kwanza uutambue uwezo wake, ukishafanya hivyo umpe nafsi ili uweze kumtumia lakini vinginevyo Watanzania tutabaki pale pale.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mambo ya msingi kwa leo ni mawili tu kupelekka hoja bungeni ili kuwapa ruzuku hao matajiri na hili ni jukumu la Waziri Mkuu hapa tunafanya kama walivyofanya Namibia. Jambo la pili na mwisho kwa leo Waziri wa Mambo ya Kigeni apige mdomo na Iran kama walivyofanya Ufaransa, kinyume chake ni hatari mno.
Msomaji wangu kumbuka leo ni Sikukuu ya Kufufuka Bwana Yesu Kristo , Ngoja mie nile pilau yangu ya Pasaka
Mwanakwetu upo? Kumbuka
“Ngoja Mie Nile Pilau Yangu ya Pasaka.”
Nakutakia Siku Njema.
makwadeladius@ gmail.com
0717649257



.gif)
.gif)
Post a Comment