Ngo Ngo Ngo Hadija Yule

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Walimu walikuwa shuleni wanatekeleza majukumu yao, mwalimu wa kwanza aliingia darasani akasomesha somo lake hadi mwisho, kengele ya kubadilisha kipindi ilipigwa na mwalimu wa somo la pili alijongea jirani na darasa lake. Wakati mwalimu huyu anaingia alikaribishwa na salaam ya wanafunzi wake, huku wanafunzi wakiwa na kelele tele…Mwalimu huyu akaitikia salaam hiyo huku kelele nyuma ya darasa zikioongezeka. Mwalimu huyu akauliza haya jamani nyinyi nyuma ya darasa mnashida gani? Jibu lilitolewa:

“Huyu hapa alipanda juu ya dawati alafu hajavaa chupi…”

Majibu yalipotolewa darasani shangwe ikawa maradufu, haya ni mambo yale ya Ngo ngo ngo Hadija yule wanafunzi haya waliyapenda mno. Mwalimu yupo mbele anataka kuanza kufundisha lakini hoja ya mwanafunzi mmoja wa kike ambaye alipanda juu ya dawati kuwa hajavaa chupi inabadilisha upepo wa darasa, wanafunzi wanashangilia. Mwalimu akafuatilia hoja hii vizuri akamuita huyu binti mbele na kutoka naye nje, akamuangalia alibaini kuwa ni kweli binti huyu alivaa sketi na shati juu yake na ndani hakuvaa chupi. Wanafunzi darasani wanasema kuwa mwanzao kila siku havai chupi na hilo lilitoa nafasi ya wanafunzi wa darasa hili waone sinema ya bure.

“Sinema iliyopachikwa jina Ngo Ngo Ngo Hadija Yule.”

Mwalimu huyu alitoa pesa yake ya pikipiki ya kumrudisha nyumbani shilingi 2000 na akamtuma binti mmoja akanunue chupi ya shilingi 1000 na pini mbili kubwa duka jirani, vifaa hivyo vilipofika alimuongoza binti huyo hadi chooni na kumpa binti huyu akavaa na pale kwenye kiuno ambapo palikuwa na uwazi akachukua pini mbili na kuziba uwazi wa eneo hili na ili kulinda heshima ya mwalimu, heshima ya binti huyu na heshima ya wanawake wote kisha wakarudi darasani na ndipo akaendelea kufundisha somo lake. Mwalimu huyu anasema haya:

“Niliagiza mzazi wa huyu binti aje shuleni, mama huyu hakufika kabisa kwa juma zima na baadaye alikuja dada wa binti huyu huku akisema kuwa mama yao ana kazi nyingi ni vigumu kuweza kuja shuleni maana nyumbani kwao maisha ni magumu sana, anahangaika na kutafuta chakula akitoka alfajiri anarudi usiku.”

Mwalimu huyu siku hii alirudi kwake kwa miguu maana shilingi 2000 ya bodaboda ilitumika kumsitiri binti yetu yule.

 

Kwa ukweli wa Mungu maisha ya Watanzania wengi ni ya kimasikini sana huku hata hao Watanzania ambao sasa wamesoma hata kama watajipiga picha maisha yao ya awali ni ya umasikini wa kutupwa, huku UJAMAA wa Mwalimu Julius Nyerere kwa sehemu kubwa uliokoa jahazi, ulificha aibu kubwa ya Watanzania shuleni. Hapa taswira iliyopo ni kwa sasa ni hii:

“Mwanafunzi hata kama karo ni ndogo au bure lakini viatu anachukua kwa mjomba, shati kwa shangazi, daftari na peni kwa Bibi huku sare anachukua kwa jirani na kisha kuweza kwenda shuleni kusoma hadi kuhitimu.”

Huo ndiyo Utanzania huku wapo wengine wachache wanaosoma kwa hisani ya taasisi zao za dini na wapo wengine ambao wazazi wao wanatimiza mahitaji yote ya kwa asilimia 100.

“Kwa hakika mchango wa Serikali ya Tanganyika/Tanzani kuwekeza katika kuwapa elimu ulikuwa mkubwa tangu mwaka 1961-1985 huku sare, viatu, vifaa vya elimu kama vile peni, kalamu ya risasi na madaftari vyote Julius Nyerere alitoa bure shuleni.”

Swali la kujiuliza kwa sasa hali ya familia nyingi za Kitanzania zikoje? Katika kulijibu swali hili Mwanakwetu awali alikutana na visa vitatu cha kwanza ni hicho cha binti huyo aliyekuwa anakwenda shuleni bila chupi kama kilivyo na kisa cha pili ni hiki: Mwalimu mmoja alikuwa shuleni anafundisha, mara darasa lake likapata mgeni, huku mgeni huyu jasho lete linamtiririka. Mwalimu huyu akasema haya mwenzetu Je(kulikoni) ?

“Mwalimu samahani, humu darasani kwako yupo dada yangu anasoma, leo asubuhi ametoka sijampa pesa ya kula hivyo nimekuja kumletea pesa ya kula maana najua nisipomletea atakaa na njaa hadi saa nane. Nilipoamka nimeuza chipsi ndiyo nimepata pesa samahani kwa usumbufu.”

Mwalimu akasema hilo halina tatizo, binti akaitwa akapokea pesa hiyo vizuri na kisha kurudi darasani. Maelezo ya mwalimu huyu yanadai kuwa binti huyu ni mrembo sana, huku wazazi wake waliachana na mama yao kurudi Morogoro baba yao hajulikani alipo na huyu kaka mtu yeye mwenyewe ni mdogo na kazi yake ni mchoma chipsi. Kibaya zaidi kaka na dada wanakaa katika chumba kimoja na wanalala kitanda kimoja. Kinachoendelea kwa sasa huyu mwalimu akiwa na harakati za kuwasiliana na jamaa wa Ustawi wa Jamii.

Msomaji wangu hivi ni visa viwili , kumbuka kisa cha tatu kipo nacho kitayafunga makala haya.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Katika Tanzania ya sasa anayeshughulikia sera ya Elimu ya Taifa hili ni Wizara ya Elimu huku TAMISEMI ya Profesa Riziki Shemdoe yenyewe inatekeleza kile kilichomo katika sera tu. Mathalani katika kisa cha Ngo ngo Hadija yule kama kungekuwa na utaratibu wa kila shule kuwa na sare za dharura, viatu vya dharura na hata sodo kulingana na mahitaji ya wanafunzi kwa hakika mwalimu yule asingalitoa shilingi 2000 yake ikanunuliwe chupi na pini na baadaye mwalimu huyu kurudi nyumbani kwa mguu. Huku mwalimu mwenye moyo huo leo yupo na kama kesho hayupo mwalimu kama huyu upi utakuwa usalama wa binti kama huyu? Hivi ndivyo ilivyo kwa kisa cha pili cha kaka na binti wa pili ambaye aliletewa pesa ya chakula cha mchana shuleni na kaka yake, huku watoto hawa kaka na dada wakilala chumba kimoja. Je upi utakuwa usalama wa binti huyu?

 

Kwa hakika katika visa hivi ukiitazama Wizara ya Elimu kwa sasa inayo Naibu Waziri mwanamke mheshimiwa Wanu Ameir, je ndugu yetu huyu anaweza kuja na suluhu ya kuwasaidia watoto wa kike? Je huyu Naibu Waziri anayajua haya?Je Naibu Waziri huyu anao uwezo na kusaidiana na Waziri wake na wataalamu wake kisha wakaja na sera maridhawa ya kumkomboa mtoto wa kitanzania? Kwa sasa jamii ya Watanzania imejaa mashaka makubwa, wapo wanaoamini kuwa Naibu Waziri wa Elimu aliyekuwa awali Injinia Kipanga alikuwa na nafuu kubwa, huku ikitajwa kuwa aliweza kusimamia vizuri ujenzi wa VETA kila mkoa nchini Tanzania nayeye mheshimwa Wanu Ameir amekuja kupakua tu baada ya mapishi kukamilika.

 

Je mheshimiwa Wanu Ameir ataweza kuthibitisha vinginevo? Hiki ni kisa cha tatu katika makala haya.

Mwanakwetu katika hili anashauri Katibu Mkuu Kiongozi waangalie vizuri pale wanapomshauri Rais katika teuzi zao. Pia suala la utatuzi wa maboresho ya mazingira ya magumu ya maisha ya watoto wa Kitanzania shuleni serikali isikwepe majukumu yake hata kama wazazi wapo lakini pia wazazi hawa uwezo wao unatafautiana lakini kuna changamoto za ndoa na vifo, serikali iwe jirani na watoto wetu kwa vitendo. Katika kulitatua hili Mwanakwetu anashauri Serikali ichukue Trioni 1.4 iliyopangwa kama matumizi ya kawaida kwa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na pesa hii ikapelekwa katika kila shule za umma tangu za msingi hadi sekondari hali itakuwa nafuu.

Mwanakweu upo?Kumbuka:

“Ngo Ngo Ngo Hadija Yule.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

































 

0/Post a Comment/Comments