Adeladius Makwega-MBAGALA.
Aprili 23, 2026 Mwanakwetu alikuwa amekaa tayari kusubiri kusikiliza taarifa ya Tume ya Kilichotokea Oktoba 29, 2026 na Siku Zilizofuata nchini Tanzania iliyokuwa inaongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Othuman Chande. Mwanakwetu alipoona mbona wanachelewa kusoma taarifa yao alikata shauri kwenda benki ya NMB Tawi ya Musoma iliyopo katikati ya mji huu ili akachukue kadi yake mpya ya akaunti ambayo ilikuwa imeisha muda wake.
Alipofika hapa Mwanakwetu alichagua kuingia mapokezi na kumwambia mama mmoja mjamzito kuwa nimekuja kuchukua kadi ya akaunti yangu ile zamani iliisha muda wake.
Mama huyu mjamzito alimtaka Mwanakwetu kutaja namba za akaunti zake. Mwanakwetu alijibu kuwa zijazikariri namba hizo. Jambo hili lilifanya mama huyu amuelekeze Mwanakwetu kumuona binti mmoja nje ili amtajie akunti yake. Jambo hili lilimuuzi Mwanakwetu, kweli hili lilifanyika na kutajiwa akaunti yake na kisha kurudi kwa mama yule wa awali, mama mjamzito. Mama huyu alimuagiza Mwanakwetu ahudumiwe na kaunta namba moja. Mwanakwetu aligoma na kusema kuwa:
“Leo nataka nihudumiwe na mama mjamzito.”
Siku hii hapa NMB Musoma ndani ya benki hii hakukuwa na wateja wengi. Mjadala huu ulisababisha hadi askari wa benki kuwa jirani na Mwanakwetu maana Mwanakwetu alikuwa na maneno mengi, huku kando ya Mwanakwetu kulikuwa na kijana wetu wa JWTZ naye eye akipata huduma. Mwanakwetu akajiuliza moyoni yaani mgambo anakuja jirani na Mwanakwetu wakati mkono wa shoto wa Mwanakwetu yupo askari wa JWTZ?
“Au mambo ndiyo yale yale ya Oktoba 29, 2025 watu wanadunguliwa kwa risasi huku kando wapo vijana wa JWTZ wanatazama? kweli polisi awe zaidi ya JWTZ?”
Haya Mwanakwetu alikuwa anayafikiria moyoni tu. Wafanyakazi wa NMB Musoma waliyokuwa jirani wakiwa wanachekea moyoni hasa kutokana na maneno haya ya Mwanakwetu:
“Leo Mimi Nataka Nihudumiwe na Mama Mjamzito.”
Kweli mama huyu mjamzito alichukua karatasi yenye namba ya akaunti ya Mwanakwetu kisha akaangalia katika mfumo na kutaja jina la Kazimbaya Makwega, Mwanakwetu akajibu ndiyo. Mama Mjamzito akatoa kitabu akampa Mwanakwetu akakisaini kisha akapewa kadi yake. Mama mjamzito akakaa kimya, Mwanakwetu akauliza sasa nakwenda wapi? Majibu ya Mama Mjamzito yalikuwa haya:
“Hapa nenda kwa Meneja Mahusiano na yeye atashughulikia juu ya PINI yako.”
Kabla ya kuondoka Mwanakwetu akampiga swali mama mjamzito :
“Jina lako nani?”
Mama huyu akaandika katika karatasi yenye akaunti ya Mwanakwetu jina lake HAFSA ATHUMANI. Mwanakwetu akatoka na furaha tele kwa huduma nzuri ya mama mjamzito.
Mwanakwetu akaenda kwa meneja Mahusiano na hapa alikutana na foleni kidogo lakini ilikuwa inakwenda vizuri, zamu yake ilifika na kukaa kiti jirani na meneja huyu:
“Nimekuja kuweka password katika akaunti yangu.”
Meneja huyu Mahusiano wa tawi la Musoma akasema sawa lakini hapa unawekewa PINI na siyo NYWILA maana kuna tafauti kubwa katika Nyila na pini. Nywila ina namba na herufi wakati pini ina namba tu, hapa tunaweka pini karibu sana. Mwanakwetu aliweka pini hiyo na kisha kuuliza jina la Meneja Mahusiano huyu, mama huyu alijibu kuwa anaitwa Josephine Ndosi kisha kuagana naye. Mwanakwetu alipotoka hapa alirudi kumuaga Mama Mjamzito yule, Bi Hafsa Athumani na kisha kurudi zake huko madongo poromoka.
Mwanakwetu anasema nini siku ya Leo?
Kikubwa ni juu ya tabia ya wateja wa NMB kulazimishwa na mfumo kubadilisha kadi zao huku hii ikiwa ni lazima hata kama kadi ya mteja ni nzima. Hili Mwanakwetu anapingana nalo, huu siyo mwenendo mzuri. Katika utafiti wa Mwanakwetu amebaini kuwa NMB ina mkataba na kampuni inayotengeneza kadi inayotambulika kama SMART CARD. Hivyo wao wanalazimisha mabenki kubadilisha kadi za wateja katika kipindi fulani, hili likiwa takwa la lazima. Hoja yao ni dhahifu sana:
“Ohh unajua masuala ya usalama wa kadi na kile kilichomo katika akaunti, maana tekinolojia inabadilika kila mara. Zamani kati zilidumu kwa muda mrefu lakini sasa hali ni tofauti.”
Kwanini SMART CARD itulazimishe wateja wa benki kubadilisha kadi wakati kadi zetu mara nyingi bado ni nzima? Mwanakwetu hili anapingana nalo kwahoja tele. Smart Card wanaweza kutengeneza kadi zisizo bora ili kukamilisha takwa la kubadisha kadi kila baada ya kipindi fulani. Hapa Smart Card inajipatia pesa kwa kutumia njia ambayo siyo sahihi, huu ni ulaghai wa kibiashara. Hapa Labda niseme haya:
“Mwanakwetu ana akaunti ya Benki ya Sparkasse kutoka nchini Ujerumani, kadi ya benki hii inayo tarehe ya kuisha matumizi lakini wiki mbili kabla ya tarehe ya kuisha matumzi Sparkasse wanakutumia kadi yako mpya , wala hakuna mambo ya kutafutana, kwa gharama nafuu.”
Benki za Tanzania zijiulize mbona benki ya Sparkasse nani anawatengenezea kadi zao za benki imara? Tanzania ni nchi masikini kwanini kadi zetu zisiwe za muda mrefu zaidi? Wajumbe wa Bodi ya NMB walitazame hili. Huku wizara ya fedha kitengo kinachosimamia benki zetu ebu litazameni hili si kwa NMB tu bali hata benki zote pamoja na huyo mnyama anayetengeneza kadi kadi.
Mwisho Mwanakwetu anafuraha tele siku ya leo kwa kuhudumiwa na Bi Hafsa Athumani ambaye ni mama mjamzito maana tangu Mwanakwetu azaliwe hajawahi kuhudumiwa na Mama Mjamzito akiwa benki.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Nataka Nihudumiwe na Mama Mjmazito.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257



.gif)

.gif)
Post a Comment