Adeladius Makwega-MBAGALA.
Aprili19, 2026 ni Jumapili ya tatu baada ya Pasaka ambapo Mwanakwetu alisali Kanisa la Mtakatifu Agustino , Parokia ya Mwisenge Jimbo Katoliki la Musoma nchini Tanzania. Misa hii ilipambwa na injili kutoka kwa Luka Mtakatifu 24, 13-35 miongoni mwa sura muhimu katika Ukristo zinazoeleza visa vya Yesu Mfufuka mbele ya wanafunzi wake. Katika kuipamba dominika hii Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki inayojishughulisha na Unjilishaji wa Watu Ulimwenguni Kadinali Luis Antonie Tagle aliyahubiri haya:
“Mtakatifu Luka anatuambia kwamba wanafunzi wawili wa Yesu waliondoka Yerusalemu; walipokuwa njiani kuelekea Emau, walikutana na Bwana, lakini hawakumtambua. Walimweleza yaliyompata Yesu ambaye alikuwa ‘mwenye nguvu katika maneno na matendo,’ lakini alisulubiwa, na sasa, kulingana na ‘wanawake wa kundi lao,’ yu hai. Waliposikia hayo, Bwana aliwaeleza, akianza na Musa na manabii wote, akifafanua yale yaliyomhusu katika Maandiko yote.
Wanafunzi hao waliokuwa wamekata tamaa walimtambua Mwalimu wao pale tu alipouchukua mkate, akaubariki, akaumega, na kuwapa. Neno lake na kushiriki kwao mkate kulirudisha nguvu mioyoni mwao, kiasi kwamba waliinuka mara moja na kurudi Yerusalemu, ambako walikutana na wenzao wakisema, ‘Kweli Bwana amefufuka, naye amemtokea Simoni!’ Nao pia wakasimulia walichokiona .
Ndugu zangu, habari njema ya Ufufuko ni kwa wote. Yesu anataka kushiriki amani yake si tu kwa wale waliobaki Yerusalemu, bali pia kwa wale waliokuwa wameondoka. Aliwakusanya hapo awali; atawakusanya tena na tuombe sote zawadi hii ya Bwana aliyefufuka. Tuombe neema hii nzuri ya kutafutwa na Bwana, ya kuutambua uso wake, ya kuungana tena na ndugu zetu, na kuwa kweli watu aliowakusanya.”
Haya ni kutoka Vatikani. Je Tanzania kuna nini? Akihubiri katika misa hii katika Kanisa la Mtakatifu Augustino Padri Julius Ogolla alisema kuwa kulingana na mila za kiafrika anapokuja mgeni nyumbani kwenu makabila mengine humpa maji, wengine pombe ,wengine uji na wengine chakula yote hii ni ukarimu kwa mgeni.
“Wengine humpa mgeni chakula ale na mtoto huku mgeni huyo akiwekewa chungu kilichojaa minofu ya nyama nono kama vile vidali, mapaja na maini kukiwa na pia na miguu, vipapatilo na vichwa vichache ambapo mgeni huyu hula chakula chake na kijana/ binti mdogo ambapo wakati wa kula binti/ kijana huyu huambiwa kuwa unapokula na mgeni wewe kula vichwa, vipapatilo na miguu tu vinono ni vya mgeni maana jukumu la mgeni kula vinono. Utaratibu wa jamii unabadilika kutoka mila moja kwenda nyingine huku ikikatazwa wakati unakula na mgeni usile kwa matonge/finyango kubwa kubwa wewe kula kwa nidhamu wewe kula kidogokidogo.”
Kama jamii za Kiafrika zinajua namna ya kula na mgeni na nani wa kula na mgeni na ukila na mgeni unakulaje? Ndiyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Yesu walijua namna Yesu alivyokuwa akila nao huku kabla ya kula kwanza alisali na kisha aliumega mkate ndipo hawa jamaa wakashituka kuwa ni Bwana.
Haya ni sehemu ya maelezo ya mahubiri ya Padri Ogolla kutoka Injili ya Luka 24, 13-35 na yale ya awali ya Kadinali Tagle yalimkumbusha Mwanakwetu miaka 10 nyuma iliyopita alikuwa Sinza Jijini Dar es Salaam alitokea Mahakama ya Kazi hapa alifika eneo linaloitwa Vatikani ambapo kando ya eneo hilo Mwanakwetu alikuwa anamgonja mgeni, upande wa pili wa barabara kulikuwa Mkutano Mkubwa wa Injili wa Makanisa ya Kipentokoste walikuwa na spika kubwa nyingi zikinadi mahubiri yap , hapa mhubiri kwanza aliisoma Luka 24. 13-35 kisha akasema maneno haya.
“Hii Injili iliyosomwa ni miongo mwa shuhuda za ufufuko wa Yesu kwetu sisi na kwa wanafunzi wake mara baada ya Yesu kusulubiwa na kuuwawa na kufufuka, hapa inaonekana baada ya matukio haya wanafunzi wake walikata tamaa na wengine kuamua kurudi katika shughuli zao za awali maana mchungaji wa kondoo amepigwa na kundi limetawanyika. Kama Yesu asingaliwatokea wanafunzi wake inawezekana hata Injili hii ya Yesu Kristo pengine leo hii isingalisomwa hapa Sinza Vatikani Dar es Salaam, hapa mkutanoni. Kwa hiyo Bwana Yesu amefufuka na hapa anawatokea wanafunzi wake waliokuwa wanarudi kijijini baada ya mambo kuharibika, kwa hiyo ndugu zangu msikubali kurudi Emau hata kama mambo ni magumu kiasi gani, msikubali kurudi kijijini maana sasa mnatakiwa kubaki Yerusalemu. Kwa hiyo mnatakiwa kubaki wapi?(mchungaji aliuliza) Yesusalemu(Waamini walijibu)Nabaki wapi? Yerusalemu… Nabaki Yerusalemu…Narudi Yerusalemu.”
Kwa hiyo msomaji wangu haya juu ni Kadinali Tagle,pia ya Padri Ogolla na Mchungaji wa Kanisa la Kipentekoste pale Vatikani Sinza miaka 10 iliyopita juu ya Injili ya Luka 24,13-35 na ndiyo maana hapa Parokiani Mwisenge Padri Ogolla alimalizia mahubiri yake kwa maneno haya:
“Jamani waamini kwa sasa Yesu tunaye, tunashiriki naye katika Ekariste Takatifu tunatakiwa kubaki kwake, kubaki kwake ni kuwa na matendo mema na mfano kwa kila mmoja wetu japokuwa tutapitia kipindi gani kigumu , tubaki kwa Yesu. Kama kuna jambo lilikuondoa kwake iwe ndoa au chochote kile rudi kwake”
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Narudi Yerusalemu.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257

.gif)
.gif)




Post a Comment