
Adeladius Makwega -MBAGALA.
Mwezi wa Machi wa mwaka wa 2026 umemalizika nchini Tanzania, huku hawa Watanzania nduguze Julius Nyerere wamekuwa na kilio kwa Serikali yao maana bei ya mafuta imepanda.
Nayo dhana kuwa Serikali yao hakuna inachofanya kutatua kero hii ikitamalaki, huu ni mtazamo kwa makundi kadhaa miongoni mwa jamii ya Watanzania wanaokaribia milioni 72.
Mwanakwetu kama Mtanzania hakuyanyua kalamu yake mapema kuandika chochote kile juu ya hali hii, huku baadhi ya watu wakisema maneno haya:
“Makwega mbona hauandiki chochote juu ya kero hii ya mafuta kupanda?”
Mwanakwetu alipokea malalamiko haya bila ya kuyajibu lakini alisema moyoni kuwa kuna kazi anaifanya akiimaliza ataandka kitu juu ya changamoto hii maana Watanzania ni ndugu zake lazima aifanye kazi yao.
Jumatatu ya Machi 30, 2026 Mwanakwetu alipanda bodaboda moja ya kijana mmoja na kumpeleka pahala fulani umbali wake ulikuwa ni wa shilingi 3,000 ambapo Mwanakwetu alilipa kiasi hicho kabla ya kupanda katika chombo hiki cha moto, kijana huyu alimfikisha kwa wakati katika eneo hilo lakini awali wakiwa wanakaribia kufika kijana wa boda boda akasema maneno haya:
“Mzee mafuta yamepanda sana bei ya Dizeli na Petroli ni kati ya shilingi 4000-4400/- kwa lita. Mimi zamani nilikuwa naweka lita tatu kwa siku ambapo nilikuwa nayatumia mafuta haya siku nzima na nilikuwa napata shlingi 7000-8000/- kwa lita moja, ndiyo kusema kwa siku nilikuwa naingiza 24,000/- hapa ukitoa pesa ya mafuta ya karibu 9000/- nilikuwa nabakiwa na shilingi 15,000/-. Kwa sasa mambo yamebadilika kabisa nikiweka lita tatu kwa shilingi 12,000/- nilitakiwa kukusanya hadi shilingi 30,000/- lakini hakuna wateja kabisa … Haya mafuta yanabaki kwa siku mbili na wateja hakuna leo hii wewe ni mteja wa pili tu.”
Mwanakwetu alifika anapokwenda na kisha kushuka na kuangana na ndugu huyu. Haya yalikuwa majira ya saa 10 jioni ya siku hii.
Mwanakwetu alifanya utafiti wa maeneo ya kazi kwa watumishi wa umma na binafsi wanazungumza nini juu ya hali hii? Utafiti huu mdogo ulifanyika Machi 31, 2026.
Hapa alikutana na haya-sasa leo unarudi nyumbani sasa ngapi? Hapa kuna kazi naimalizia. Basi ukimaliza hiyo kazi yako sisi tupo nje tunaomba tuondoke na wewe angalau tuweze kufika nyumbani kwetu. Vinginevyo kweli tutembee kwa miguu! Sisi akina mama tutachubuka mapaja?
Hawa wafanyakazi walikuwa wanaongea kisha muda ulipofika gari hilo liliwabeba watumishi hao kurudi makwao. Huku Mwanakwetu hafahamu kama kesho yake hawa akina mama walifikaje kazini.
Ilipofika Aprili Mosi, 2026 Mwanakwetu alikutana na ndugu fulani wamejikusanya pembeni wanaongea. Mwanakwetu kwanza akamsifia mama mmoja kwa kuwa na nywele nzuri , mama yule akasema asante. Mwanakwetu akiwa hapa mama mmoja akawa anasema maneno haya:
“Umbali kutoka kwangu kuja kazini kwa sasa ni shilingi 6000/- wakati awali ilikuwa 3000/- kwa mwezi nilikuwa nalipa 120,000/- lakini sasa natakiwa kulipa 240,000/-. Nimepiga mahesabu nimeona hesabu haikai sawa, kweli 240,000/- ni pesa ambayo ninatakiwa kumpa kijana wangu anayesoma Chuo Kikuu shahada ya Uandisi maana 100,000/- ya chumba alichopanga, 100,000 ya chakula na huku 40,000 ni pesa ya kutoa foto kopi ya nyaraka mbalimbali chuoni, kibaya zaidi mwanangu kakosa mkopo wa elimu ya juu.
Hivi kweli nikitumia 240,000/- nikilipia nauli si nitakuwa punguani? Mwanangu atashindwa kusoma, hivyo nimeamua nitembee kwa miguu.”
Muhuni mmoja akapita kando akarusha maneno haya ya utani:
“Mwambie shemeji akununulie gari !”
Mdau mwingine kando akamjibu yule ndugu- shemeji mwenyewe wewe, haya nunua gari! Jamaa yule muhuni wa awali akawa mpole hakusema neno lolote akaenda zake: Jamaa hawa wakawa wanaendelea kuongea:
“Hongera zao, si wameamua kupandisha bei ya mafuta ili sisi tutembee kwa miguu, tuchubuke mapaja. Yaani hata wenza wetu tusisalimiane nao usiku? Huu ni mwendo wa Kulala Mzungu wa Nne wamakonde wanaita mwendo wa kulala Chikundu moto.”
Baadaye hawa jamaa wakatawanyika kila mmoja akaenda njia yake.
Mwanakwetu aliendelea na utafiti wake nah ii ikafika Aprili Pili, 2026. Siku hii Mwanakwetu alitembea kwa mguu umbali kama wa KM tatu ambapo nauli ya awali kwa bodaboda ilikuwa 1000/- ikawa imepanda mara mbili sasa 2000.Njiani kulikuwa na watu wengi wanatembea kwa miguu, bodaboda zinapiga honi mno kusaka abiria, huko bodaboda hazina abiria hata mmoja. Njiani Mwanakwetu alipishana na bodaboda 31 ni boda 11 zilikuwa na abiria huku bodaboda 16 hazikuwa na abiria na pikipiki 3 zilikuwa siyo kubeba abiria.
Mwanakwetu alifika nyumbani kwake kisha kuamua kuyaandika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Hawa wanaotembea kwa miguu wanaongea hili na lile lakini kitu nilichobaini ni kuwa :
“Watu wanaotembea kwa miguu jasho linawatoka na pengine wakifika nyumbani wamechoka sana, huku njiani wamekuwa na desturi ya kutafakari maisha yao hili na lile. Tafakari hizo zinafanyika sana kuliko kwa mtu aliyepanda gari au pikipiki, ambapo tafakari hizo za watembea kwa miguu zina madhara makubwa katika kufanya maamuzi ya mambo kadhaa ya binadamu huyu maishani mwake.”
Jambo la pili ambalo Mwanakwetu amelibaini kuwa biashara ya usafiri wa bodaboda itadhohofika na pengine kufa kabisa maana itakuwa haina faida tena, watanzania wanarudi kutembea kwa miguu na kupanda baiskeli. Matokeo ya mafuta kupanda hata uingizaji wa pikipiki kutoka China na India utapungua mno.
Jambo la tatu, vijana waliyokuwa wanajiingizia kipato kufanya biashara ya bodaboda wataanza kurudi katika matukio ya uharifu na hali ya usalama wa Tanzania itayumba. Huku watu wabaya wanaweza kupenya kupitia magenge ya vijana hawa wasio na kazi maalumu.
Serikali ilipaswa kuhakikisha bei ya mafua ingebaki kama ilivyo na kikubwa mafuta yanayouzwa sasa yalingia nchini mapema iweje bei ipande gafla bini vuu? Kwa mafuta yanayoingia nchini sasa serikali ilipaswa kushusha kodi na tozo za mafuta haraka ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea na maisha yao kama kawaida.
Huku kwa kuzibiti kupanda kwa bei ya mafuta na kuzibiti kuficha mafuta ,Jeshi la Polisi Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi Tanzania kwa pamoja wafanye doria katika vituo hivyo wafanye doria ya pamoja katika vituo vyote binafsi vinavyouza mafuta ili kuzibiti michezo michafu.
Hii ni tafakari ya Mwanakwetu kama alivyoikusanya tangu mwishoni mwa Machi na mwanzoni mwa Aprili 2026 juu ya kinachotokea baada ya bei na mafuta ya vyombo vya moto kupanda nchini Tanzania, kipi kinachotokea na kipi cha kufanya.
Ka hali sasa malalamiko ya wananchi ni kuwa kana kwamba imewakumbatia wafanyabiashara wa mafuta na huku ikiwatenga wananchi wake, ambapo mtazamo huu ni hatari kwa umoja wa kitaifa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Huu ni Mwendo wa Kulala Chikundu Moto.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257





.gif)
.gif)
Post a Comment