Mlemavu Mmoja Kwa Kila Watu Sita

Adeladius Makwega MBAGALA

Msomaji wangu ebu jiulize swali hili, hapo ulipo kuna watu wangapi waliokuzunguka jirani yako? Kwa hakika unaweza kupata majibu ya namba tafauti kati 1,2,3,5,6,7 au 10. Kama wewe huwa unakwenda Kanisani/Msikitini kila Jumapili/kila Ijumaa je benchi la Kanisani kwako/mstari wakati mnafunga sala wanakaa watu wangapi?  Jibu lake linaweza kuanzia 6-15. Haya ni mambo ya hesabu.

 

Katika hizi hesabu msomaji wangu siku ya leo tambua hili:

 

“Kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema takribani watu bilioni 1.3 duniani kote wana ulemavu mkubwa, idadi ambayo ni sawa na asilimia 16 ya idadi ya watu wote duniani. Watu bilioni 1.3 wanaishi na ulemavu wa aina fulani. Karibu asilimia 16 ya idadi ya watu duniani ikiwa wastani wa mtu 1 kati ya 6) ”

 

Ndiyo kusema iwe katika mkusanyo wa watu popote ulipo ifahamike kuwa kati ya watu sita mmoja ni mlemavu, huku viwango vya ulemavu vikitofautiana. Takwimu za WHO zinanadi na kugonga kengele ya hatari kuwa asilimia 80% ya watu wenye ulemavu yaani bilioni 1.04 wanaishi katika nchi zinazoendelea. Mlio wa king’ora hiki cha walemavu kutokana na takwimu za WHO juu ya watu sita kwa mmoja ilimshitua mno Mwanakwetu na kusababisha amtafute Katibu wa Chama cha Walemavu wa Viungo Mkoa wa MARA (CHAWATA) Ndugu Leonard Lameck Mkaruka, yeye alimkaribisha Mwanakwetu na kusema haya:

 

“Vipo vyama vingi vya watu wenye ulemavu kulingana na aina ya ulemavu mathalani Chama cha wenye Alibinism (TAS), Chama cha Wasiona (TLB), Chama cha Viziwi (CHAVITA), Chama cha watu wenye ulemavu wa viungo (CHAWATA) n.k. Sisi sote ni ndugu na ndiyo maana kila Disemba 3 ya kila mwaka tunaadhimisha siku ya Watu wenye ulemavu ulimwenguni.”

Ndugu Mkaruka alisema kuwa CHAWATA kina wanachama wa aina mbili:- Aina ya kwanza ni kwa wenye ulemavu wa viungo, hawa uanachama wao unatokana na ulemavu wake (yaani viungo) na wa pili ni yule mwanachama ambaye amejiunga na CHAWATA kwa mujibu wa Katiba, mwanachama huyu utambulisho wake ni kadi ya CHAWATA.

“Mwenye kadi anapewa kipao mbele kwa hiyo tunahimiza watu wenye ulemavu (viungo) kuwa wanachama wa chama hiki (CHAWATA) ili kuunganisha nguvu katika kutetea haki zetu. Hii haina maana kuwa Mwanachama asiye na kadi tunamtenga hapana tunatoa fursa kadhaa kwao pia ikumbukwe kuwa umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.”

Kwa utafiti wa Mwanakwetu kwa mkoa wa Mara CHAWATA kina takribani wanachama halisi 3,500 wenye kadi tangu ngazi ya Mtaa, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mkoa na hii inakwenda hadi ngazi ya Taifa huku tawi moja kigezo liwe na wanachama watano na kuendelea.

“CHAWATA kinaongozwa na Mwenyekiti taifa ndugu ni Ahmadi Komboza (0754555031) Katibu ni Boniface Mayengela (0658578467). Kwa mkoa wa Mara Mwenyekiti ni Bw. Yohana Magai Msanyila (0782133895) na Katibu ni Bw. Leonard Lameck Mkaruka (0688728130).”

Akizungumza na Mwanakwetu Ndugu Mkaruka amesisitiza walemavu wajitokeze katika zoezi la kukusanya takwimu zao ambapo hili litasaidia kuweza kuwatambua na kuwafikia walemavu popote walipo. Pia Bw. Mkaruka ametoa wito kwa Watu Wenye Ulemavu kujitokeza kuomba mkopo wa asilimia kumi ambao unatolewa na Serikali kwa watu wenye ulemavu, wanawake na vijana ili kuweza kujiongezea kipato.  Ndugu Mkaruka alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni ukosefu wa ofisi za CHAWATA kuanzia ngazi ya Tawi hadi Mkoa. Kwa sasa ofisi wanayofanyia kazi ni kwa hisani tu toka katika Taasisi za Serikali na huku akiomba kwa watu wenye mapenzi mema kusaidia wapate vitendea kazi ikiwamo Kompyuta, Printa na samani za ofisi yao. Haya ni ya hapa Mkoani Mara juu ya Walemavu wetu, huko ulipo msomaji wangu hali ikoje?

 

 

Kwa hakika Mwanakwetu alijifunza mengi juu ya CHAWATA hapa Mkoani Mara na idadi ya walemavu ulimwenguni. Baadaye Mwanakwetu aliagana na ndugu Mkaruka na kisha kwenda kuyaandika makala haya.

Mwanakwetu Upo? Kumbuka:

“Kila Watu Sita Mlemavu Mmoja.”

Nakutakia Siku Njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 
















0/Post a Comment/Comments