Miongo ya Tengua Teuzi

 

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Mapema ya Aprili, 2026 nchini Tanzania kumefanyika utenguzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) DKT. CPA. James Andilile Mwainyekule. Mara baada ya utenguzi huu Mwanakwetu amekuwa katika tafakari kubwa juu ya mamlaka inayoteua na kufanya utenguzi hasa akilini mwa Mwanakwetu akiwa na swali hili:

“Je tenguzi hizi zina tija au hasara kwa Watanzania?”

Mwanakwetu alisema moyoni kuwa:

“Kama lipo faili serikalini linalokusanya barua la tenguzi kwa hakika faili hilo limejaa barua za utenguzi tele, barua nyingi tangu mwaka wa 2016 hadi 2026. Hii ikiwa Miaka Kumi ya Tengua Teuzi.”

Mwanakwetu ana hakika faili hilo sasa litakuwa limejaa barua hizo. Huku Mwanakwetu anajua kuwa yupo Mtanzania mwenzetu ambaye yeye jukumu lake ni kulitunza faili hilo na kila likisogezwa karibu anajua kuwa kuna mtu anatenguliwa. Ndugu yetu huyo yeye na wanaoifanya kazi hiyo hawajui machungu ya kutenguliwa ngoja leo Mwanakwetu awasimulie machungu ya kutenguliwa. Kwa hiyo ndiyo kusema tangu kwa Rais John Pombe Magufuli na hata Rais Samia Suluhu Hassan kama tenguzi hizo zina faida basi faida hizo wamezileta wao na kama tenguzi hizo zina hasara wao wameiletea Tanzania hasara hizo.

“Kiongozi yoyote atake asitake lazima abebe furushi la mazuri na furushi la mabaya yake.Changamoto ni moja tu je kati ya furushi la mazuri na furushi la mabaya lipi limelizidi lingine?”

Mwanakwetu bila ya kutafuna maneno anasema haya:

“Tenguzi hizi ni hasara kubwa kwa taifa; kwanza ni ule ujuzi anaoupata mhusika akiwa na taasisi aliyekuwapo, namna kazi zinavyofanywa, ujuzi na uzoefu wake unapokwa gafla kisha anakuja mtu mwingine ambaye akifika pale anakuja kujifunza hili na lile hapa ni tatizo. Mathalani kwa sasa kazi nyingi zinafanyika kimifumo mtu aje na awe na uwezo wa kujifunza lakini akiwa hana uwezo kujifunza kwa haraka, taasisi itakwama inapiga mark time hapo hapo kwa muda mrefu badala ya kusonga mbele.”

Hilo la ujuzi na uzoefu ni la kwanza, jambo lingine ni hili:

“Kiongozi anapokuwa katika taasisi anayajua yale mambo ya wazi na ya siri ya taasisi husika ambapo ni hatari watu wengi kukalia nafasi ya juu taasisi kwa muda mchache na kisha kurudi kuwa watumishi wa kawaida katika taasisi zingine.”

Mathalani huyu Dkt. CPA Mwainyekule kwa sasa anaifahamu EWURA tangu ilipoanzisha hadi utenguzi wake unafanyika. Kwa sasa hata baada ya miaka 10 EWURA inaweza kufanya maamuzi kadhaa huku kwake DKT. CPA Mwainyekule akilini mwake atajua kuwa uamuzi A, Uamuzi B au Uamuzi C siyo sahihi au ni sahihi kwa hoja A,B,C na D kwa sababu amefanya kazi hapo kwa ngazi ya maamuzi labda iwe Dkt. Mwainyekule hakuwa mtu makini alipokuwa EWURA au alikuwa mvivu wa kusoma sheria , kanuni na mafaili ya wazi ya siri ya taasisi yake.

 

Jambo la tatu kiongozi anapofanya kazi na taasisi huwa kuna makundi ya wafanyakazi ambao wamefanya nae kazi vizuri, kwa desturi kundi hilo kama kiongozi wao ametenguliwa, kundi hilo linateseka sana wakihusishwa moja kwa moja na uongozi uliotenguliwa. Hapa ndipo balaa zaidi na taasisi nyingi hazifanyi vizuri baada ya utenguzi wa kiongozi wake mkuu.

Jambo la nne:

“Marupurupu ya mshahara wa kiongozi aliyetenguliwa, kwa hakika kila utenguzi unaofaywa na Rais, yule anayetenguliwa anabaki na mshahara wake na kiutumishi, huu unaitwa Mshahara Binafsi. Kwa mfano Dkt. CPA Mwainyekule kabla ya kuwa Mkurugenzi huyu jamaa alikuwa Mhasibu Mkuu (I) na mara baada ya utenguzi kwa cheo hiki cha EWURA Katibu Mkuu Kiongozi ataituma nakala ya utenguzi kwa Katibu Mkuu Utumishi ili kumpangia majukumu mengine kama taaluma yake ya awali ilivyo. Labda Katibu Mkuu Utumishi akaona kwa kuwa huyu jamaa ni mume spika mstaafu ili awe jirani na mke ikaamuliwa ampangie kazi ya Uhasibu Mkuu (I) ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya au akaamua ampangie majukumu hayo hayo ya Uhasibu Mkuu (I) Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Huyu ndugu lazima anabaki na mshahara wake wa Mkurugenzi Mkuu wa EWURA lakini majukumu anayoyafanya ni yale ya Mhasibu Mkuu (I) ambayo ni kuandaa  bajeti , kuhakiksiha nyaraka za malipo zinakaa vizuri ili kuepusha hoja za ukaguzi … hapa kazi ni Mhasibu Mkuu (I) lakini mshahara ni Mkurugenzi wa EWURA, hapa kunakuwa na mishahara ya wakurugenzi wakuu wa EWURA wawili. Nani anayelipa mishahara hiyo? Hapa ni mimi na wewe, huko ni kulitia hasara taifa.”

Hoja ya tano ni ya kibinadamu hivi watu wanaofanya utenguzi wanajua uchungu wa kutenguliwa? Usumbufu wa kuhamisha vyombo katika nyumba? Usumbufu wa maneno ya jamii ambayo haijui ukweli wa mambo? Taharuki kwa ndugu vijijini? Je maisha ya anayetenguliwa baada ya tukio hilo yanakuwaje?

“Makwega sikia… mimi huwa nakaa nyumba ya Serikali mara chache mno, nakaa kwa tahadhari mno maana lolote linaweza kutokea muda wowote ule…”

Haya ni maelezo ya Dkt Faustine Ndungulile ambaye aliwahi kuwa Waziri katika Serikali ya awamu ya tano na awamu ya sita nchini Tanzania.

 

Mwanakwetu amebebwa na tafakari hii.

Hizo hoja tano tu ambazo ni baadhi tu ya hoja chache zilizochaguliwa na ndugu yetu Mwanakwetu siku ya leo ili kuyajenga makala yake.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Ni kweli Rais anapewa mamlaka ya kuteua na pia kufanya utenguzi na haya siyo mamlaka binafsi bali ni mamlaka kwa niaba ya… WANANCHI WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.

Kwa utenguzi wa Dkt. CPA Mwainyekule lazima tujue huyu ndugu huyu kafanya kosa gani? Hii ni haki ya jamii kufahamu lakini pia lazima ionekane kuwa baada ya utenguzi tukiyajua makosa yake kwa aliyotenguliwa tuone kama bei za mafuta zimepanda lazima tuone bei ya mafuta zimeshuka na hatua zionekane zinachukuliwa, siyo utenguzi ufanyike kisha tuone kimya huko ni kumuonea Dkt. Mwainyekule lakini pia ni kumyima raha mkewe Dkt.Tulia Artikson, Mwanakwetu atamani spika wetu mstaafu awe na amani.

 

Jambo la mwisho katika haya yote ambalo linampa tafakari kubwa Mwanakwetu ni la kushangaza kidogo John Pombe Magufuli na hata Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa mawaziri wa serikali zilizotangulia lakini hawakuwahi kutengulia nafasi zao hata mara moja. Swali ni je walikuwa malaika kutoka mbinguni? Jibu lake hapana, bali ni binadamu wenye damu na nyama na hata waliowahi kufanya nao kazi Serikalini wanayafahamu mengi. Sasa iweje wao wawe hodari wa kufanya tenguzi hizi ambazo zina hasara kwa hili taifa? Tatazama hoja tano za Mwanakwetu. Mwanakwetu hapa hana majibu.

Jambo la kusikitisha tu hata zile Idara zinazofanya kazi ya kumshauri Rais zenyewe ndiyo zinazoongozwa kwa viongozi wake kufanyiwa utenguzi, kwa mfano aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara hiyo Afande Diwani Athuman Msuya, mpaka sasa ndiye Mtanzania aliyetenguliwa mara nyingi kuliko wote tangu uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, wakati Rais Samia akiweka mkono wake kumtengua na hata Rais John Pombe Magufuli hivyo hivyo. Tanzania Nchi Yangu Tunakwendaje Katika Hali Kama Hii?

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Tanzania Nchi Yangu Tunakwendaje Katika Hali Kama Hii?”

Mwanakwetu sasa nimekata tamaa.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments