
Adeladius Makwega-MBAGALA.
Aprili 14, 2026 Mwanakwetu alikutana na afisa mmoja wa serikali ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Tanga. Siku hii Mwanakwetu alikuwa anapanda ngazi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ahmadi (gafla) akamuona mtu mzima, mweupe sana, mrefu wa wastani, aliyevalia koti na shati rangi tofauti anaongea na simu.
“Ehee hiyo nitumie katika simu yangu… sawa sawa sawa sawa.”
Jamaa huyu anaongea na simu na nadhani na nduguze, Mwanakwetu amejawa na shauku ya kumsalimia, huyu Mjumbe wa zamani wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa Tanga. Hapa hapa mjumbe huyu akampa ishara Mwanakwetu kuwa akae kwenye benchi lililo jirani na Masjala Kuu ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara. Huku huyu ndugu anamalizia kuongea na simu, kisha akaanza kuongea na Mwanakwetu kumbe upo Mara? Mwanakwetu akajibu ndiyo.
Jamaa akasema nilipotoka Tanga nilihamishiwa hapa hapa na pale…Huku anacheka nayeye Mwanakwetu moyoni akiwa na bashasha tele kwa kukutana na ndugu huyu ambaye huwa anaandikia mkono wa shoto.
Huyu jamaa alikuwa ni miongoni mwa waliokuwa wakitoa mafunzo kwa viongozi wa Mkoa wa Mara, juu na mambo ya wakimbizi.
Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba ufahamu hili. Kamati ya ulinzi na Usalama Mkoa huwa inakuwa na wajumbe kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama, lakini huyu jamaa hakuwa Polisi, hakuwa Magereza na hakuwa JWTZ.
“Huyu anayeandikia mkono wa kushoto yupo vizuri sana, siyo mnafiki, kisha ni mtu mkweli.”
Mwanakwetu baadaye wakaagana na kisha ndugu huyu kurudi ukumbini nayeye Mwanakwetu akiwa na furaha sana alipofika ofisi alipokuwepo akawasilimulia jamaa zake juu ya kukutana na huyu Mjumbe wa zamani wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tanga.
Jamaa huyu kuna siku akasema maneno haya:
“Jamani Wakurugenzi wa Mkoa wa Tanga nawaombeni muwe makini, kazi hii ni Rais ameniagiza mimi niifanye, Mwenyekiti wangu Katibu Tawala Mkoa na mimi ni Katibu wake. Sasa kazi hii tuifanye vizuri atakayeniangusha mimi nitamuandikia taarifa kama Rais kama wewe ulivyoniangusha. Tambueni mimi nimepata kazi serikalini nikiwa kijana mdogo tu na tena nimemaliza kidato cha sita, sasa nikifukuzwa huku nitakwenda wapi?”
Jamaa wa Mwanakwetu wakawa wanacheka.
Mwanakwetu alifanya kazi zake vizuri sana kisha muda wa kurudi nyumbani ulifika, akabeba begi lake hadi kwake. Wakati anataka kulala akapigiwa simu na jamaa ambaye hakumfahamu jina lake:
“Mwanakwetu naona unamsifia sana Balozi Hussein Katanga, wewe hamjui tu ndiyo maana unasema mengi mazuri juu yake, haujua alivyowafanyia watu wengine akiwa pale nyumba nyeupe…”
Mwanakwetu akamsikiliza huyu ndugu kisha akamwambia nimekusikia vizuri sana lakini unaposema mimi simfahamu ndugu Hussein Katanga hilo siyo sahihi, binafsi namfahamu huyu ndugu tangu akiwa anapanda basi ya Ekarusi (Kumbakumba) na UDA anatoka Kurasini Shimo la Udongo anakwenda Tambaza Sekondari na wanafunzi wakati huo wanakata tiketi za UDA za msimu. Balozi Katanga alipenda sana kucheza mpira wa miguu na alikuwa kijana anayesali sala tano ya dini ya Kiisilamu.
“Namfahamu Balozi Hussein Katanga wakati akivaa kaptura ya Polister Grey na shati jeupe, miguuni kavaa laba anakwenda shule. Huyu jamaa alikuwa mhasibu wa kawaida kisha Mhasibu Mkuu wa Wilaya(DT), alafu akawa Mkurugenzi Mtendaji, baadaye akawa Katibu Tawala wa Mkoa, akawa anapanda ngazi hatua kwa hatua alafu akawa Katibu Mkuu, alafu Balozi na baadaye Katibu Mkuu Kiongozi.”
Mwanakwetu anamwambia huyu jamaa :
“Nakubaliana na wewe kitendo cha kupinga uonevu kwa watumishi wa umma tangu wale wa kawaida hadi wale wanaoteuliwa na Rais. Nakubaliana kuwa Katibu Mkuu Kiongozi ni mtu karibu na Rais lakini shida ni moja tu hawa vijana wetu wanaotuma taarifa kwa rais ni waadilifu? Wana nia njema? Hawa wanaotuma taarifa Ofisini kwa Rais juu ya mtu yoyote unadhani wananunua chakula soko gani? Matumbo yao hayana njaa? Wanapeleka watoto wao shule gani? Wananunua nguo zao duka gani? Naamini wanaenda pale pale unapopita mimi,wewe na wao humo humo , kwa hiyo wengine wananunulika na hapo ndipo upotoshaji unaweza kuja, hapa mtu sahihi anaweza akaondolewa na mtu dhalimu akabaki, kisa ni maslahi ya wale wanaotoa taarifa ngazi ya juu.”
Mwanakwetu akawa anaendelea kusema, mathalani Katibu Mkuu Kiongozi yeye anakusanyiwa taarifa kadhaa, kisha atamshauri Rais afanye maamuzi kwa taarifa zilizokusanywa au Rais anaweza kuamua kwa matakwa yake mwenyewe tu. Sasa kama hapa unapomlaamu Balozi Hussein Katanga alipokuwa Katibu Mkuu Kiongozi unakuwa umekosea, kwanza tuwalaumu hao wanaokusanya hizo taarifa tangu ngazi za chini hadi taifana hata tumlaumu Rais mwenyewe anayeamua. Mazungumzo haya yalikuwa mazuri sana kisha Mwanakwetu aliagana na ndugu huyu na kuendelea na kazi zake ndogo ndogo akalala na kulipokucha yaani Aprili 15, 2026 akaamua kuviweka visa hivyo viwili katika makala haya siku ya leo.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Katika makala haya kumbuka Mwanakwetu awali alikutana na yule Mjumbe wa zamani wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Tanga angalia namna Mwanakwetu alivyokuwa na shauku ya kuongea na mjumbe huyu, japokuwa mjumbe huyu alikuwa bize na simu lakini bashasha ya Mwanakwetu ilikuwa na subira yenye kiu kubwa. Msomaji wangu naomba ifahamike wazi huyu mjumbe huyu alipokuwa Tanga alikuwa mjumbe mwadilifu, mjumbe mzalendo na mjumbe kupigiwa mfano.
Kwa hakika katika hili hata wale wanatuma taarifa kwa Rais wajitahidi wawe wakweli, wawe makini maana taarifa hizo hizo zinazotumwa kwa Rais na kufanya maamuzi kama maamuzi ya mkubwa siyo sahihi zinaibua malalamiko kwa watu kadhaa wanaofanya kazi na Rais na hata serikali yenyewe inabeba mzigo wa lawama pia maamuzi ya Rais yakiwa mabaya yana madhara hata kwa wale wanaotuma taarifa hizo potofu na hata wale wanaozikumbatia taarifa zenye shaka.
Kwa mfano:
“Imetumwa taarifa iwe juu ya kiongozi yoyote wa wilaya ambayo wewe mtuma taarifa au wewe uliyezikumbatia hizo taarifa iwe Dodoma au Dar es Salaam, maamuzi ya Rais yakawa kiongozi makini akaondolewa kisha eneo hilo akapelekwa kiongozi dhaifu. Wewe uliyekumbatia/uliyetuma taarifa hizo kama upo Dodoma/ Dar es Salaam, kumbuka Dar es Salaam / Dodoma siyo kwenu –huko ni akina Mwanakwetu, Sasa umepata likizo unakwenda kwenu kule alipo kiongozi mpya dhaifu. Ukiwa likizo umepanda basi ukapata ajali Mungu kakujalia haujafariki ajalini lakini umepata majeraha makubwa. Waliopata ajali mnapiga simu Hospitali ya Wilaya ili lije gari la wagonjwa kuja kuwachukua mkimbizwe hospitalini mathalani mnajibiwa kuwa gari ya wagonjwa mbovu au mnajibiwa gari ya wagonjwa haina mafuta. Hapa unakufa kwa uzembe wako wewe mwenyewe uliyetuma taarifa za uwongo, ngazi ya juu na akaondolewa kiongozi mzuri na kupelekwa kiongozi dhaifu kwa hili unawaingiza adhabuni hata ndugu zako wa vijijini pasipo na sababu za msingi.”
Mwanakwetu anasema Balozi Hussein Katanga hana baya , wenye kutuma taarifa fanyeni kazi yenu kwa uadilifu kumbuke Ukifanya Mabaya Unajifanyia Mwenyewe na Mazuri Unajifanyia Mwenyewe.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Mabaya Unajifanyia Mwenyewe na Mazuri Unajifanyia Mwenyewe.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257


.gif)
.gif)

Post a Comment