
Adeladius Makwega-MBAGALA.
Aprili 6, 2026 Mwanakwetu alikuwa Musoma Mjini, siku hii mvua kubwa ilinyesha kwa muda kama wa dakika kama 50 ambapo tangu mwezi wa Aprili uingie mji huu ulikuwa haujapata mvua.
Mwanakwetu akawa anafanya usafi wa vyumba vyake huku akipika chai ili ainywe na kipolo cha pilau yake alichopika siku ya Pasaka yaani Aprili 5, 2026.
Namna mvua hii ilivyokuwa inanyesha ilimkumbusha Mwanakwetu mazingira fulani, eneo fulani ambapo Mwanakwetu aliwahi kuishi akiwa kijana sana, ambapo kulikuwa mbali sana na nyumbani kwao Mbagala. Eneo hili lilikuwa ni kijijini na Mwanakwetu alikumbuka wakati anakwenda huko babu yake Mzaa Baba Mwalimu Fidelis Makwega Kazimbaya alimwambia maneno haya:
“Mjukuu wangu unakwenda kufanya kazi huko, ni mbali na sisi lakini maisha ni popote pale, nakupa shuka mbili za kujifunika, saa moja aina motima na begi la ngozi. Ukifika huko usisahau kusali dominika na jitahidi sana ukiwa hapo tafuta mzee mmoja unayesali naye ambaye atakua na umri mkubwa, kisha awe rafiki yako, awe anakushauri kwa hili na lile hakikisha angalau kwa mwezi uwe unamtembelea kwake angalau mara moja ukiwa na hata kilo moja ya sukari mkononi. Huyu mzee atakuwa kinga yako mno na hakuna mtu atayekusumbua maana jamii itashangaa huu urafiki wa kijana na mzee una nini? Hapo mjukuu wangu utakuwa salama ugenini.”
Msomaji wangu nikuchekeshi kidogo hili begi mpaka leo nililopewa babu yangu bado ninalo na aina ya mabegi ya ngozi rangi ambayo yanapigwa brashi ya kiwi na kung’aa vizuri.
Msomaji wangu tambua kuwa:
“Viatu, mikanda ya kuunoni na mabegi huwa yanangarishwa kwa kiwi. Japokuwa sasa hili limebaki kwa viatu tu.”
Mwanakwetu alifika eneo hili akaanza kazi huku alimzoea sana mzee mmoja anayefahamika kama Protas na akawa rafiki mkubwa wa Mwanakwetu. Huku historia ya kijiji hiki ilidokea kuwa mzee Protas wakati wa UJAMAA alikuwa mwenyekiti wa kijiji hiki.
“Kwa mwezi mara moja nilikuwa naenda kwa Mzee Protase na yeye akajenga utaratibu mara nyingi akitoka dominika ya tatu ya kila mwezi kusali ibada ya pili anakuja nyumba kwangu na mkononi alikuwa anabeba kuku au bata, tunaongea huku unapikwa ugali tunakula naye vizuri kisha saa tisa anakwenda kilabuni maana siku hii eneo hili kulikuwa na gulio.”
Zawadi hizi za kuku na bata kutoka kwa mzee Prptase zikabasabisha Mwanakwetu ajenge banda na kuwa mfugaji mzuri wa kuku na bata huku akiongezea na bata wengine aliowanunua gulioni. Kuku wa Mwanakwetu walikuwa wanakufa sana lakini bata walishamiri mno hadi wanakijiji wakawa wanasema ukitaka bata nenda kwa yule jamaa wa Dar es Salaam ana bata wengi.
“Hii nyumba ambayo alikuwa anaisha Mwanakwetu ilikuwa na vyumba vinne mmiliki alikuwa mzee mmoja Muisilamu safi akiwa na mabinti wengi warembo, wenye sura nzuri maumbo ya kuvutia na wachokozi sana.
Wapangaji walikuwa wanne, chumba kimoja alikuwa anaisha kaka na mdogo wake (Wakatoliki) , chumba cha pili mdogo mtu alikuwa na kaka yake(Wakatoliki) , chuma kingine alikaa kijana mmoja peke (Mlokole) huyu mlokole usiku alikuwa anasali mno na hata kama mchana wake amefanya dhambi wapangaji wenzake tutajua maana namna anavyotubu, kwa kusali muda mrefu huku akijuta kwanini amezini? Hapa tunajua huyu jamaa leo alikuwa na binti wa watu. Hili lilimsaidia mno Mwanakwetu kujua kumbe walokole na wao huwa wanaanguka dhambini. Kumbuka numba hii ina vyumba vine na chumba cha mwisho alikuwa anaishi Mwanakwetu peke yake.”
Katika nyumba hii chumba cha pili alichokuwa anakaa mdogo mtu na kaka yake maana yake mdogo mtu ndiyo alikuwa mpangaji (mlipa kodi). Huyu kaka mtu alikuwa mkatoliki mzuri sana kila siku misa ya asubuhi anasali na dominika anasali.
Msemakweli ni mpenzi wa Mungu Mwanakwetu nilikuwa nasali dominika tu.
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu haya yote anayakumbuka tu ambayo ni matukio ya miaka mingi akiwa kijana mdogo.
Urafiki wa mzee Protase na Mwanakwetu ukawapa mashaka jamii ya Waisilamu wakidhani kuwa Mwanakwetu atakuwa na mpango kuoa, hivyo basi mzee Protase ndiye anayemsaidia kumtafutia mrembo wa kijiji hiki. Lakini mbona katika mji huu Waisilamu kuna warembo wengi ? Kwanini Mwanakwetu asiseme neno la mapenzi? Au Mwanakwetu mdomo wake mzito? Hapa anahitaji msaada?
Awali Mwanakwetu hakujua kama kuna hoja hii lakini rafiki mmoja anayefahamika kama Rajabu kuna siku alimfuata Mwanakwetu na kumwambia hili:
“Makwega sema kama unataka kuoa tukupe binti yetu. Usiwe muoga maana tunamuona mzee Protase ni rafiki yake. ameshakutafutia binti wa hapa?”
Mwanakwetu alimjibu rafiki yake Rajabu kuwa hili hapana na mzee Protase ni rafiki yangu ananielekeze tu namna bora ya kukaa na nyinyi hakuna kingine.
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yupo kwake anafanya usafi wanyumba anayoishi na hapa anayakumbuka haya matukio ambayo ni visa vya maisha yake akiwa kijana sana.
Jumapili moja tumeenda kusali vizuri na kisha kurudi nyumbani pamoja huku yule mlokole kenda katika kanisa lake kusali ambapo ibada ilikuwa inatumia saa nyingi.
Katika kundi hili la watu watano vijana Wakatoliki kukawa na vijana wawili hawakupokea Ekarist Takatifu Kanisani , kukawa na mjadala mbona nyinyi hamjapokea? Haya yanasemwa na kaka yule mtu mzima ambaye alikuwa anasali sana kila siku misa za asubuhi na dominika haposi huku hapa akikaa kwa mdogo wake.
“Jamaa hii jumapili ya tatu au ya nne, fulani na fulani kwanini hampokei? Kama kuna shida nendeni mkaungame. Parokiani kuna Mapadri wawili.”
Haya yakiwa maneno kaka mmoja mkubwa ambaye alikuwa na mke huko alipotoka miongoni mwa ambao hawakukomonika Mwanakwetu hakuwa miongoni mwao.
Kimoyomoyni kila mmoja akawa anasema huyu kaka maana yake kanisani anakufuatilia kuwa leo fulani hajapokea?
Huyu kaka akasema hapa tunapokaa tunajamii ya Waisilamu wengi inatutazama namna Wakristo tunavyoishi. Humu ndani yupo mlokole na yeye anatuangalia namna sisi Wakatoliki tunavyoishi na sisis vile vile tunamtazama yeye anavyoishi na jana niliwasikia mlikuwa mnatania kuwa alikuwa na mwanamke mmejua wakati anatubu usiku. Mkumbuke na yeye anatuangalia vizuri. Haya niambieni kwani hamjapokea?
Jamaa mmoja miongoni mwa wale ambao hawakupokea akasema:
“Mie mwenendo wa Padri fulani, mimi simuamini na hata akisalisha misa zake mimi huwa simpokei Yesu wa Ekarist Takatifu.”
Kikundi cha hawa vijana wakawa wanataka kujua shida nini? Hata Mwanakwetu nayeye alikuwa anatamani kujua tatizo nini la Padri huyu?
Jamaa akasema:
“Haiwezekani kasisi atoke kulala na mwanamke kisha aje altareni aje kuubadilisha mkate kuwa mwili wa Yesu na Divai kuwa damu ya Yesu…”
Hili ni jambo geni kwa Mwanakwetu anashangaa, huyu kaka mkubwa akamuuliza huyu kijana wa pili nayeye akajibu hivyo hivyo.Huyu kaka mkubwa alikuwa anatoka familia yenye watawa wengi akalibeba jambo akalifikisha pahala, akasema litafanyiwa kazi tu na kanisa.
Kwa hakika kibinadamu vijana hawa ndani ya nyumba hii akiwamo Mwanakwetu walitamani kuwajua hao wadada wanaotuhumiwa, majina kadhaa yalitajwa
Baadae akaja mzee Protase na bata wake mkononi, Mwanakwetu akapokea akamshukuru sana. Kisha hoja juu ya hawa vijana ikawekwa mezani na kukawa na mjadala mrefu sana: Mzee Protase akasema maneno haya:
“Katika maisha yenu zipo tuhuma ambazo binadamu anaweza kutuhumiwa na tuhuma mbaya ni tuhuma ya kufisha mwili kumuuwa mtu na kufisha roho na hii tuhuma ya kufisha roho za binadamu wenzakki inafisha imani ya dini. Katika ulimwengu huu ukiwa kiongozi wa watu iwe kisiasa au kiroho inapoibuka tuhuma kama hii ni mbaya sana, inaua imani ya walio chini yako... Jambo hili kama la kweli Kanisa litafanyia kazi.”
Mwanakwetu baadaye alihama eneo hili na hakujua kilichotokea kwa jamaa wale, parokia ile na kasisi yule.
Haya msomaji wangu Mwanakwetu aliyakumbuka tu Aprili 6, 2026 kuamua kuyaweka katika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mzee Protase aliyasema maneno haya:
“Katika ulimwengu huu ukiwa kiongozi wa watu iwe kisiasa au kiroho inapoibuka tuhuma ya kuwafisha watu kiimani au kimwili ni mbaya sana, inaua Imani ya unaowaongoz na kuwakatisha tamaa kabisa.”
Hapa lazima tuhuma hizo zichunguzwe na zifanyiwe kazi haraka ili kurejesha imani za walio chini.Kibaya kule kutuhumiwa tu hata kama siyo za kweli uhalali wa mhusika kukalia nafasi hiyo eneo hilo unaondoka ni heri ukafanye kazi mbali na hapo.
Mwanakwetu pia amemkumbuka mpangaji mwezake mlokole ambaye akifanya dhambi utajua tu maana inamnyima raha wiki nzima, unamuona namna anavyotubu kumbe waliokoka wanaanguka dhambini.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Waliohoka Huanguka Dhambini.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257









Post a Comment