Adeladius Makwega-MBAGALA
Haya ni majira ya asubuhi ya Aprili pili, 2026 Musoma Mkoani Mara, Mwanakwetu amepagiwa jukumu la kufika katika jengo la Makazi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara ambapo kunafanyika ukarabati mkubwa, huku Katibu Tawala Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya angefika kukagua ukarabati huo. Majira ya saa nne ya asubuhi ya siku hii ambayo ni Alhamisi Kuu, kiongozi huyu wa Serikali alifika katika makazi haya, aliingia na kukagua kazi hiyo, huku mafundi wakiendelea na kazi zao.
Katibu Tawala akiwa hapo ilibainika kupitia kwa Bi Irene Mosha ambaye ndiye Meneja Mradi kuwa:
“Mradi huu unatekelezwa kupitia mkataba namba RAS/077/2025/2026/NC/11, kwa kutumia force account ambapo ulianza Disemba 1, 2025 na unatakiwa kukamilika hivi karibuni.
Huku changamoto ni moja tu wazabuni kuchelewesha kuleta vifaa vya ujenzi kwa wakati.”
Katika Tawala Mkoa wa Mara ndugu Gerald Musabila Kusaya akiwa mradini akasema ikiwa miradi ya Serikali inazo fedha za kutosha hakuna haja ya mkandarasi yoyote kuomba kuongezwa muda, ni lazima miradi hiyo ikamilike kwa wakati na hasa miradi ya mkoa wa Mara maana pesa ipo shida iwe nini?Miradi hii hawapaswi kupewa wazabuni wa majaribio.
“Natambua kazi inafanyika vizuri lakini nataka kazi hii ifanyike kwa ubora maana hii ni nyumba ya kiongozi mkubwa wa serikali na pesa hii ipo,mimi ndiyo mwenye mradi, kwanini mradi uchelewe kukamilika?
Lazima ukamilike kwa wakati, kama shida ni wazabuni kuleta vifaa kwa wakati, basi watafutwe wazabuni wenye sifa na uwezo maana Miradi ya Serikali siyo miradi ya kuwapa wazabuni wa majaribio, Miradi ya Serikali siyo ya kuchezewa shere.”
Haya yanasemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara Ndugu Kusaya wakati akikagua ukarabati wa Nyumba ya Katibu Tawala Mkoa huu ambayo inafanyiwa ukarabati mkubwa, unaogarimu karibu shilingi milioni 60 ambapo nyumba hii ipo jirani na Ziwa Victoria.
Ndugu Musabila akiwa anakagua mradi huu akapita kando ya banda lake la kuku, hapa Ahmadi (gafla) akakutana na kuku wake wawili wamepasua yai huku wakilishambulia kwa kulila:
“Lo salale kuku wa Katibu Tawala Mkoa wa Mara wanakula mayai yangu! (watumishi kando wakacheka)
Ebu wafungie ndani hao kuku wawili mara moja! Kuku anayekula mayai lazimwa achinjwe maana atawafundisha tabia mbaya kuku wengine…”
Kuku hawa walifungiwa haraka bandani.
Zoezi la ukaguzi wa mradi huu baadaye lilikamilika huku kuku wa kiongozi huyu waliendelea kuwika katika banda hilo
Kwa hakika wakati Katibu Tawala anakagua ukarabati huo wa makazi yake, hali ya hewa ya Mji wa Musoma ni nyuzi joto 26 na unyevunyevu ni wa asilimia 25 na ujirani na mvua ni wa asilimia 63 na upepo ukivuma kwa KM 14 kwa saa.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu anajiuliza tu je kuku wale wawili waliofungiwa bandani kwa kosa la kula mayai yale waliyoyataga wao wenyewe kweli watakuwa salama? Au ndiyo wanatumika kuipamba meza ya Katibu Tawala mkoa wa Mara kama kitoweo katika chakula chake wakati wa Sikukuu ya Pasaka ya mwaka wa 2026? Mwanakwetu hana majibu.
Mwanakwetu upo ?Kumbuka:
“Kuku Anayekula Mayai Lazimwa Achinjwe.”
Nakutakia Pasaka Njema.
0717649257









Post a Comment