
Adeladius Makwega-MBAGALA.
“Si mtetei Dkt. Mpango lakini kumbukumbu zangu zinaonesha kwamba taarifa ilitolewa katika Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wa CCM Taifa kwamba Dkt. Mpango aliomba kujiuzulu mapema ila alikakataliwa. Tatizo letu ni katiba, tushughulikie hilo.”
Haya ni mojawapo ya maoni muhimu sana katika makala ya Mwanakwetu iliyopewa jina Nchimbi Asiwe Kama Mpango ya Aprili 17, 2026. Maoni haya Mwanakwetu ameyapokea kwa mikono miwili huku akiyachukulia kwa uzito mkubwa na heshima tele ili yaweze kujenga makala haya siku ya leo. Haya ni maoni ya mtu makini sana ambaye Mwanakwetu anamfahamu huku aliwahi kuwa mwandishi mzuri wa habari, makala na chambuzi za uchumi nchini Tanzania kwa miaka mingi. Kwa hakika ebu tuamini kuwa Dkt. Philip Mpango ni kweli alitaka kujiuzulu kisha Kamati Kuu ikakataa ombi lake.
Swali ni moja tu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza utaratibu gani wa kujiuzulu Makamu wa Rais? Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatoa mwongozo wa wazi kuhusu kujiuzulu kwa Makamu wa Rais. Hapa kuna mambo muhimu kulingana na Katiba hiyo:
“Makamu wa Rais anaweza kujiuzulu kwa hiari yake kwa kutoa taarifa ya maandishi kwa Rais. Kujiuzulu kwake kunakuwa rasmi pindi taarifa hiyo inapopokelewa na Rais au baada ya muda maalum uliotajwa katika barua hiyo.”
Hapa msomaji wangu rejea Ibara ya 37 na 50 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inazungumzia utaratibu wa kuingia na kutoka madarakani, ikijumuisha kujiuzulu.
“Kando na kujiuzulu, madaraka ya Makamu wa Rais yanaweza kukoma ikiwa kama atafariki dunia akiwa madarakani. Atapoteza sifa za kuwa Makamu wa Rais kwa mfano, kama atakuwa hana uwezo wa kuhudumu kutokana na maradhi ya mwili au akili. Ikiwa Rais atafariki, atajiuzulu, au kushindwa kuitumikia nafasi hiyo, Makamu wa Rais anapanda ngazi na kuwa Rais, hivyo nafasi yake inakuwa wazi.”
Kumbuka Ikiwa kiti cha Makamu wa Rais kitakuwa wazi kwa kujiuzulu au sababu nyingine, Rais atamteua Makamu Rais mwingine na hivi ndivyo ilivyotokea wakati Makamu wa Rais alipopanda kuwa Rais baada ya kifo cha Rais John Pombe Magufuli. Hivyo ndivyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyosema lakini kabla ya kujiuzulu Umakamu wa Rais-Makamu wa Rais mwenyewe kurejea kiapo chake cha kukalia nafasi hii kinasema nini? Kisha unafanya maamuzi. Wewe ukishaandika barua na ikamfikia Rais umemaliza kazi hivyo ndivyo katiba inavyoelekeza hakuna Kamati Kuu wala Halmashauri Kuu ya CCM Taifa hawa wote katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawatambua kama raia wa kawaida tu.
Hakuna mtu yoyote ambaye amepewa madaraka ya kukataa Makamu wa Rais au Rais kujiuzulu. Kama umeandika barua ya kujiuzulu kisha mtu anakwambia amekataa unamuuliza hiyo katiba gani? Hayo madaraka unayatoa wapi? Hauoni kuwa hapo hata wewe wewe uliyeandika barua ukibaki kitini unavunja katiba ambayo Makamu wa Rais/Rais wanaapa kuilinda? Kwa lugha nyingine wajumbe wa Kamati Kuu wale ni raia tu wenye maslahi yao wakati mwingine katika ngazi ya Serikali, hayupo anaweza kukwambia chochote maana kiapo cha kwanza cha Juu ni cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kiapo cha pili ni cha Makamu wa Rais.
Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu ebu tuwaangalia wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ni kina nani? Kwa hakika wajumbe wengi wa Kamati Kuu ya CCM Taifa wamejaa watu wa makundi mawili tu, wale walioshika nyadhifa kadhaa ndani ya serikali na kisha kuachia ngazi na wapo wafanyabiashara. Kwa miaka mingi kikao hiki kinajazwa na jamii ya ndugu hawa.Ndiyo maana baadhi ya watu huwa wanasema:
“Kamati Kuu ya CCM Taifa inakuwa kama Bussines Summit/Retired Leaders Summit tu na kwa muda mrefu imekosa uwakilishi wa makundi la WanaCCM kutoka mashinani ambapo TANU /ASP hawakuwa hivyo vikao vya TANU / ASP walijaa makabwela kutoka mashinani.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika kama hoja hii ina ukweli ati Dkt. Philip Mpango alitaka kujiuzulu kisha akakataliwa hapa huyu ndugu yetu hakuitendea haki nafasi hii na kama ingekuwa kunafanyika mapendekezo hata stahiki zake za Umakamu wa Rais hakupaswa kupewa. Hapa pendekezo la kunyimwa mafao yake Dkt .Philip Mpango linakuwa sahihi. Tuamini pia kama hoja hii ya kujiuzulu siyo ya kweli, swali nije upi ulikuwa msimamo wa Dkt. Philip Mpango kuelekea Bandari yetu kupelekwa sokoni? Kwa hakika Dkt. Emmanuel Nchimbi lazima ajifunze kupitia madhaifu makubwa ya Dkt. Philip Mpango maana Madhaifu Haya Yanatia Hasira ambalo hili ni shabaha la Mwanakwetu kuandika makala haya.
Kujiuzulu ingesaidia mambo mengi mabaya yasingalitokea maana yake CCM ingejitafakari mapema nahata yale ya akina Balozi Hussein Kattanga, Afande Diwani Athumani Msuya na kuondolewa Ukurugenzi wa Bandari akina Elias Hamisi yasingalitokea, migogoro ya akina Humphrey Polepole n hata Matatizo ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata , Tundu Lissu kuweka Kolokoloni n ahata hizo hoja za maridhiano leo hii zisingalikuwepo.
“Kwa hakika kujiuzulu ilikuwa njia sahihi na ingezuia kuendelea kwa mchakato wa lile jambo linalopingwa lakini kubaki Serikalini ilikuwa ni kuruhusu mchakato kuendelea ambayo hii ndiyo hali tuliyonayo leo hii.”
Kwa hiyo mzee wangu Dkt.Philip Mpango Shikamoo Yangu Hautoipata Kwame.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Kubaki Ilikuwa ni Kuupigia Makofi Mchakato.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257



.gif)
.gif)


.gif)
.gif)
Post a Comment