KM 1291 Za Vumbi Kiteto Zifike Ukomo

Adeladius Makwega-MBAGALA.

“Jimbo la Kiteto ni eneo kubwa, lina KM za Mraba 17,000 Kipenyo ni cha KM 500, wapo wakulima na wafanyakazi, wanachapa kazi vizuri sana lakini changamoto ni barabara. Hapa barabara za TARURA ni KM 1291 tu huku barabara zenye lami ni KM 4 tu…Hizi ni barabara chache lazima ziboreshwe kwa kuongezeka. Barabara hizi hazikwepeki kuongezeka zaidi, nitawakera sana kipindi hiki, hapa nitazungumza barabara tu, barabara ya Kongwa, Kiteto Simanjaro na Arusha Haikwepeki…”

Haya ni maelezo ya Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara Mhe.Edward Ole Lekaita Aprili 13, 2026 akiliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano kuwa wananchi wa Kiteto wamemtuma kupaza sauti yao moja tu juu ya tatizo la barabara katika jimbo hilo, akisema wizara yoyote ikitoa nafasi ya maswali yeye anatuzungumzia barabara tu, kazi yake yeye itakuwa ni namna ya kuliingiza swali hilo katika wizara hiyo.

 

Mhe. Lekaita ambaye ni mwanasheria pia aligusia Barabara ya Handeni Chemba, Kibirashi hadi Singida inapita mikoa kadhaa hadi Tanga ambapo bomba la mafuta litapita na Bandari ya Tanga itafunguka, hizi ni barabara mbili zitafungua uchumi wa watu wa Kiteto.

Wakati mhe. Edward Ole Lekaita akitoa hoja hii Bungeni Mwanakwetu aliguswa sana na changamoto ya barabara ya watu wa Kiteto ambayo ni wilaya yenye watu wanaokaribia 400,000 huku idadi ya watu wa mkoa huo inakaribia Milioni 1.9 na robo tatu wa wananchi hao laki 4 ni wa Kiteto ambao wanaotoka vijijini ambapo idadi hii ya wananchi ni asilimia 21 ya wananchi wote wa Mkoa wa Manyara.

 

Jambo hili wailaya ya Kiteto lilimgusa mno Mwanakwetu huku akibaini kuwa watu wa Kiteto wakimiliki wanyama karibu laki nne kama vile ng’ombe, mbuzi, punda na nguruwe.

Mwanakwetu akifuatilia hoja hii ya Mhe. Lekaita alisema moyoni kuwa kwa sasa kila mhe huyu atakapokuwa anatoa hoja zake Mwanakwetu atakuwa sambamba na Mbunge huyu kupaza sauti ya watu wa Kiteto na huko ni kuwa sambamba na watu wote Kiteto ambayo ni asilimia 21 ya watu wa Mkoa wa Manyara maana KM Nne Za Lami Kiteto Abadani Hazitoshi.

Najua wasomaji wa Mwanakwetu watasema inakuwaje leo Mwanakwetu Kijana wa Mbagala anaungana na watu wa Kiteto?Je Mwanakwetu kapata mrembo wa Kimasai kutoka kwa mhe Edward Ole Lekaita?

Vyovyote msomaji wangu utakavyodhani lakini tambua watu wa Kiteto wa KM 1291 vumbi, hili halikubaliki lazima KM za lami ziongezeka Wilayani Kiteto.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“KM 1291 za Vumbi Kiteto Zifike Ukomo.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 





















 

0/Post a Comment/Comments