Adeladius Makwega-MBAGALA.
Hii ni Aprili 23, 2026 Mwanakwetu anatoka zake Benki ya NMB Musoma, mfukoni mwake anakadi mpya ya benki hii, mara baada ya kubadilishiwa huku kadi yake ya awali nzima kabisa. Hapa akiwa amejawa na furaha tele, baada ya kuhudumiwa na mama mjamzito anayeitwa Hafsa Athumani, hili likiwa tukio jipya maishani mwake. Sasa Mwanakwetu hapa anatembea kurudi alipokuwa awali.
Akiwa njiani akawa anawatafakari wafanyakazi wa Benki ya NMB Musoma, hapa kumbuka kulikuwa na binti alikuwa amekaa kaunta namba moja ambaye Hafsa Athumani alimwambia Mwanakwetu kuwa ahudumiwe naye, Mwanakwetu alikataa na kusema
“Leo nataka nihudumiwe na mama Mjamzito.”
Mwanakwetu japokuwa alihusudu kuhudumiwa na mama mjamzito lakini binti wa kaunta namba moja macho ya Mwanakwetu yalimtazama vizuri sana alikuwa mweusi, mrefu, mwili uliojengeka, mtulivu huku akiwa amesuka nywele zake vizuri. Huyu binti wa kaunta namba moja wajihi wake ulikuwa unafanana sana na mama wa Mwanakwetu:
“Daa huyu dada amefanana na marehemu mama yangu Doroth Mlemeta vile vile.”
Hapa Mwanakwetu akilini mwake anamkumbuka marehema mama yake namna namna alivyokuwa , hapa tulivyokuwa wadogo mimi na wadongo zangu Modestus, Michael na Samweli.
Msomaji wangu kumbuka hapa Mwanakwetu anatembea kwa miguu anarudi alipokuwa baada ya kuhudumiwa na hawa jamaa wa NMB.
Hapa akilini mwake akakumbuka tukio la mwaka 1985 akiwa darasa la tatu Shule ya Msingi Mkuranga Mkoani Pwani.
“Siku hii ilikuwa ni majira Pasaka na shule zimefunguliwa kama ilivyo Aprili 23, 2026 bali tarehe tofauti Mwanakwetu niliugua gafla kisha nikamjulisha mama yangu Doroth Mlemeta ambaye aliyekuwa mwalimu wa shule hii. Mwalimu huyu akasema nenda hospitali na uongozane na rafiki yako mmoja. Mwanakwetu akarudi darasa la III na siku hii walikuwa wanasoma hesabu za Ankara akafunga daftari zake akabeba mfuko wake wa kitambaa, akamueleza rafiki yake anayeitwa Shaha Uwanga akakubali kumsindikiza na hivyo kuanza naye safari ya Zahanati ya Kijiji Cha Mkuranga.”
Huyu Shaha Uwanga:
“Hili jina Uwanga lilikuwa jina la utani jina lake halisi la baba yake ni MOHAMMED maana Shaha alikuwa muuzaji unga uliyowekwa sukari, maarufu mithili ya bwibwi(Uwanga) kila siku anakuja nao shuleni asubuhi alikuwa anauza taslimu ikifika majira ya mchana anakopesa kisha kesho yake tunamletea pesa yake.
Wakati huo kwa wale wanaokumbuka watoto wengi wa Kiisilamu waliozaliwa miaka 1970 na kuendelea walikuwa wanaitwa Shaha kwa sababu Iran iliwahi kuwa na kiongozi aliyekuwa na jina hilo kumbuka hii ipo hata katika Ukristo mathalani kipindi cha Papa Yohane Paulo wa Pili watoto wengi walilitwa majina haya.”
Msomaji wangu katika hili unaweza kufaya utafiti mdogo, kila mara kama ukienda kuzika makaburi ya Waisilamu kama makaburi yao wameyafanyia usafi vizuri angalia vibao vya utambulisho kaburini utabaini hili la jina Shaha litakuwa linajirudia sana.
Siku hii Mwanakwetu na Shaha wakaongozana hadi Zahanati ya Kijiji cha Mkuranga kupitia ile Barabara ya Kisiji Pwani ambapo ilikuwa ya vumbi na Zahanati ya Kijiji cha Mkuranga ilikuwa pale ilipo Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga. Hapa pia palikuwa na Mahakama ya Mwanzo.Walipofika zahanati Shaha akasema maneno haya:
“Kuwaka … Nimemleta huyu mwanafunzi mwezangu anaitwa Kazimbaya Makwega anaumwa sana anaomba dawa.”
Kuwaka akaingia ndani ya chumba hicho cha zahanati akachukua kopo jeupe akatoa tembe mbili za dawa kisha akampa Mwanakwetu anywe, hapo hapo huku amemsimamia. Kisha Shaha akamuongoza Mwanakwetu hadi kwao nyumba ya Mkuu wa Shule ya Msingi Mkuranga, akamfikisha kisha Shaha Uwanga kuanza safari ya nyumbani kwao nadhani alikuwa anakaa Magogo Matatu kwa bondeni kama unaelekea Hoyoyo.
Msomaji wangu kumbuka haya anayakumbuka Mwanakwetu Aprili 23, 2026 lakini tukio hili ni la mwaka 1985 Kijijini Mkuranga Pwani ya Tanzania Mwanakwetu akiwa mtoto. Mwanakwetu alipofika nyumbani kwao alijibwaga kitandani na kuuchapa usingizi na hadi wazazi wake wanarudi kutoka kazini kalala fofofo. Baadaye mama yake mzazi akamuasha na kumwangia maji ndipo akazinduka na kuulizwa alipewa dawa hospitalini? Majibu yalikuwa ndiyo na Mwalimu Mlemeta akauliza dawa hiyo kakupa nani? Majibu yalikuwa haya:
“Dawa hii Kanipa Kuwaka vidonge viwili na tangu nilipotoka pale hadi nafika hapa nilikuwa napepesuka kwa usingizi.”
Mama wa Mwanakwetu akambeba mgongoni mwanae hadi kijijini jirani ya Kituo cha Mafuta cha Mkuranga kabla ya kufika hapo kulikuwa na nyumba nyingi na nyumba moja muuguzi / mkunga wa zahanati ya kijiji hiki alikuwa amepanga. Walipofika hapa akamueleza kuwa Kuwaka kampa dawa mwanae tangu mchana na amelala hali yake siyo nzuri muuguzi akaomba msaada wake. Mama muuguzi alikuwa na jokofu linalotumia nguvu za jua, hapa hapa akachukua maji ndani ya jokofu lake akayachanganya na maji ya kawaida kisha kumfuta Mwanakwetu kwa kitambaa mwili mzima, mama muuguzi akahangaika huku na kule nayeye Mwanakwetu kulazwa chumba cha mabinti wa huyu mama kwa mapumziko.
“Mimi nilikwenda Kisarawe kuchukua mshahara, huyu Kuwaka anaweza kutuletea shida na baadaye mashetani ya Wapogoro yatatusumbua maana Wapogoro hawawezi kukubali mtoto afe akiwa mdogo kiasi hiki, mashetani ya Wapogoro yatatueleleza-Yatasumbua na mimi hili silitaki maishani mwangu. Huyu atakuwa kapewa vidonge vya usingizi tu, lakini hazina shida, kesho akiamka atajisikia vizuri tu lakini Kuwaka yeye ni Mgambo tu wa Kijiji kwanini anajiingiza kutoa dawa kwa wagonjwa? Mgambo wa Kijiji amekuwa na mamlaka haya?
Leo nimejifunza sitakuwa namuachia tena ufunguo wa zahanati .”
Mama wa Mwanakwetu akasema sasa usipomuachia Kuwaka hizo funguo za Zahanati na Mahakama yetu mtamuachia nani? Yeye ndiye mlinzi wa Zahanati na Mahakama na yeye ndiye anayeaminiwa hapa kijijini, hapa hakuna namna kama utamuachia mwingine ni hatari kwenu hamtabaki salama.
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu kapewa mapumziko chumba cha mabinti wa huyu muuguzi ambaye alikuwa na mabinti wengi huku mmoja akisoma na Mwanakwetu.
Baadaye hali ilitengema mama wa Mwanakwetu alimbeba mwanae hadi kwao na siku iliyofuata Mwanakwetu alikuwa mzima.
Mwanakwetu alipopona akiwa shuleni alikuwa akiwatania mabinti wa yule mama muuguzi kuwa alishalala kitandani kwao siku nyingine atakweda kulala usiku mzima ili afaidi kulalia maua mazuri yaliyofumwa katika shuka zao. Huku mabinti wa mama muuguzi walikuwa wanacheka mno.
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu anarudi alipotoka na hii ni Aprili 23, 2026 alifika pahala hapo na kuendelea na mambo mengine. Akiwa hapa Mwanakwetu alikuwa ameketi pahala ambapo kulikuwa na runinga kubwa awali walipanga wasipoteze muda kuiangalia taarifa ya tume ya Jaji Mohammed Othman Chande. Baadaye akaja jamaa mmoja akasema jamani mbona hamuangalia taarifa hiyo? Ndugu huyu akajibiwa kuwa unafikiri hawa ndugu watakuwa na jipya? Jamaa huyu akasema ahaa jamani tuisikilize! Jamani huyu akaondoka zake. Katika eneo hili kukawa na kuingia na kutoka kwa muda hivyo yupo mtu ambaye Mwanakwetu hakumfahamu aliiwashwa hiyo runinga na kisha kuonekana mwenyekiti huyu wa tume ya yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuatwa baba mmoja mrefu mweupe anaisoma taarifa yake. Hapa katika kundi tulilokuwapo mmoja wetu mdogo wake alipigwa risasi jijini Dar es Salaam yaani hata kuupata mwili wake ni Mungu Bahati tu, jamaa huyu nayeye alikuwa na ile ingia toka kama Mwanakwetu katika eneo hili na akakutana ripoti inasomwa, jamaa akawa anaingia na kutoka mara nyingi. Huku awali alipanga akale ugali na samaki na hili la kula likawekwa pembeni, jamaa anaingia na kutoka. Jamaa hakuweza kukaa kitini, baadaye akaaga akisema kuna mtu atakuja kumuulizia akifika aambiwe. Mwanakwetu akasema sawa. Kweli baada ya muda fulani alipofika huyu mgeni wake akaitwa, akaja akaongea naye na kisha kurudi alipotoka. Hadi Jaji Chande anamaliza kuisoma taarifa yake ndugu huyu hayupo.
Mwanakwetu akawaambia jamaa kando kuwa mnajua huyu mwenzetu kafiwa na mdogo wake Oktoba 29, 2025 sasa ilipowasha runinga na hii ripoti inamkumbusha kifo cha mdogo wake, hii taarifa inamnyima amani jamani naombeni tuizime hii runinga hili likafanyika.
Hapa hapa kumbe jamaa mwingine yeye alilibaini hili mapema, hivyo basi wakati Jaji Chande anaanza kuisoma taarifa yake jamaa huyo alinyanyuka kitini mbio na kutoka na simu yake akavaa earfoni na kwenda kuisikiliza msituni ili kumpa amani huyu Mtanzania mwenzetu aliyefiwa na mdogo wake. Baadaye huyu jamaa aliyefiwa na mdogo wake alipokuja alipoona runinga haioneshi kitu alirudi alipokuwa awali alibebea vifaa vyake na kurudi tulipokaa, hapa akakaa kwa dakika kama 45 lakini hakujisikia vizuri tena na baadaye aliaga kurudi kwake mapema sana kuliko ilivyo desturi yake.
Hapa Mwanakwetu alitaka amsindikize lakini kunakazi aliyokuwa anaifanya hajaimailiza hivyo ndugu huyu alirudi nyumbani kwake mwenyewe. Tukio hili lilimnyima amani sana ndugu huyu n ahata Mwanakwetu huku akijiuliza Jaji Chande na wenzake wanayajua haya? Wakumbuke na wao wamezaa na wana wajukuu, je ripoti yao iliyotumia fedha za Watanzania imetimiza matakwa ya walipa kodi?
Msomaji wangu huu ni muhtasari wa siku hii ya Aprili 23, 2026 tangu pale NMB Musoma Mjini hadi pale alipokuwepo Mwanakwetu.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu anamlinganisha Jaji Mohammed Othman Chande na Kuwaka Mgambo wa Kijiji cha Mkuranga wakati wa UJAMAA, ndugu Kuwaka badala ya kufaya kazi yake ya ulinzi vizuri yeye akaingilia majukumu ya utabibu na kuanza kutoa vidonge vya usingizi balaa likawa kubwa. Hii ni hatari na haya ndiyo makosa makubwa ya Jaji Chande yapo madai kuwa Majaji Mara Nyingi Wamezoea vya Kunyonga vya Kuchinja Hawaviwezi ati wao wenyewe wakusanye ushahidi na kisha wao wafanya maamuzi tu-Hawawezi. Mahakamani ushahidi unakusanywa na mwingine yeye Jaji anafanya uamuzi tu sasa kumpa Jaji Chande asimamie kukusanya ushahidi hilo ni kosa wengine wakisema lilifanywa makusudi, umri wao mkubwa nalo likiwa tatizo.
Haya yakiaminika kuwa yalifanywa kuwalinda wale waliohusika na matukio haya ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata:
“Inasikitisha mtu mzima anasimama hadharani hata kugusia kuzimwa kwa mitandao, huu ulikuwa mkakati maalumu wa kuficha ushahidi wa matukio haya?”
Ndugu mmoja alimwambia Mwanakwetu.
Mizimu wa waliofariki Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata unadhani utawaacha salama?
Katika hili la Jaji Chande Mwanakwetu akakumbuka kisa chake cha kupewa dawa za usingizi pale Zahanati ya Kijiji cha Mkuranga na huku mama muuguzi alisema:
“Mizimu ya Wapogoro Haiwezi Kukuacha Salama.”
Hili la Oktoba 29, 2025 waliofariki ni wengi kutoka makabila kadhaa , dini kadhaa unadhani Mungu atawaacha wahusika salama? Hili ni ngumu bali muda utakuwa muamuzi.
Msomaji wangu angalia hali ya Watanzania waliyofiwa na ndugu zao Oktoba 29, 2025 na siku zilivyofuata namna wanavyoteseka? Fikiria Kama aliyefiwa na ndugu yake, anapata shida hii, huyu hajamuua ndugu yake, bali mtu mwingine ndiyo amefanya hivyo, hali siyo nzuri. Mungu atuepushie mbali hili tusipokuwa makini inaweza kuibua hali ya kulipiziana visasi.
Wewe uliyefanya uharamia huu unadhani utabaki salama? Wewe unayeshabikia uharamia huu unadhani utabaki salama? Wewe uliyepanga uharamia huu unadhani utabaki salama? Huyu ni mtu mmoja kati ya wengi waliofiwa, jamani angalieni hapa dunia hauishi wewe tu , toa nafasi ya ukoo wako na ndugu zao waje kuishi kwa amani hapa duniani.
Makala haya yatabaki kuwa rejea kwa wale ambao hawakushuhudia matukio haya iwe ya kisa cha KUWAKA pale Mkuranga au haya ya Jaji Chande wakati anasoma ripot iyake.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Hawawezi Kukuacha Salama.”
Nakutakia Siku Njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257








.gif)
.gif)
Post a Comment