Hawa Waligombana Lini?

 



Adeladius Makwega-MBAGALA.

Mara zote Mwanakwetu huwa anasema kuwa Mwigulu Nchemba ambaye sasa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mtu mwema/mtu mzuri na mtu muungwana kama mtu akimfuata na kumueleza shida/changamoto au tatizo linalomsonga kama lipo chini ya himaya yake huwa anampokea, anamsikiliza na anaitatua shida hiyo. Katika haya yote labda Mwanakwetu anachoweza kumwambia nduguye mhe. Mwigulu Nchemba ni hili:

“Mhe. Mwingulu Nchemba aangalie wasaidizi wake wasije wakaipoteza sifa yake hii.”

Kwa hakika hii ni sifa yake huyu ndugu yetu tukiyaweka kando yale yote yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata hiki ni kilio chetu bado tunangoja majibu.

Siku ya leo msomaji wangu nataka huitazame picha ya August 22, 2015 ya mhe. Mwigulu Nchemba akiwa ni miongoni mwa kundi la wana CCM waliochukua fomu ya Urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama cha Mapinduzi ambapo mwisho wa siku mhe John Pombe Magufuli alishinda.

Kwa hakika Mwanakwetu wakati huo hakuwa anamuunga mkono Mwigulu Nchemba hili lazima niliseme.

 

Picha hii wanaonekana watu watano ambao wamekaa katika chumba kikubwa chenye samani pembeni kabisa, kikiwa kimepambwa na zulia jekundu. Hii ikionesha wanausaka kweli Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawa jamaa walikuwa wanamuunga mkono Mwigulu Nchemba aliyeshika tama huku amekunja nne. Ukiitazama picha hii vizuri kuanzia mkono wa kulia wa kwako wewe unayeitazama anaonekana mwanamke amechuchumaa huku anaandika kitu, kisha anaonekana Hamisi Kigwagwala ambaye amevalia suti nyeusi akitoa maelekezo kwa huyu mwanamke aliyechuchumaa, alafu anaonekana Mhe. Mwigulu Nchemba pia kunaonekana jamaa amesimama na ameshika kiti alichokalia Mh Mwigulu, huyu jamaa aliyesimama anaitwa Dkt. George Nyaronga (Zamani alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe). Mbele ya Dkt Nyaronga yupo Maria Sarungi Tsehel kana kwamba akimsikiliza kwa umakini mhe. Mwigulu Nchemba.

 

Mwanakwetu kwa kuitazama picha hii anajiuliza je ndoto ya Mwigulu Nchemba kuusaka Urais ilipotea mwaka wa 2015?

Haya ni mambo ya miaka 11 iliyopita kwa mwaka wa 2026.

Mwanakwetu ameitazama kwa umakini picha hii huku akiwa na tafakari hii:

“Picha hiyo Mwigulu yupo na jamaa zake wa karibu Jijini Dodoma. Huyu Maria Sarungi hakuwa mpinzani wakati huo Maria Binti Sarungi Dada Mkuu wa Zanaki Sekondari zamani wakati huo alikuwa CCM.”

Ukiitazama picha hii unaweza kujiuliza hivi kwanini Hamisi Kingwangwala asimpigie simu Mwigulu Nchemba nakumwambia maneno haya.

“Mh Mwigulu Mwezangu umebahatika kuaminiwa na huyu mama, umekuwa Waziri wa Fedha na baadae Waziri Mkuu. Mh Mwigulu kumbuka wakati ule unautafuta Urais ulikuwa unajiita dogo janja, nikumbuke na mimi nduguyo.”

Kisha Maria Sarungu nayeye aseme maneno haya kwa Mwigulu Nchemba:

“Mimi nilikuwa mtu wenu wa habari, nairusha kwenye vyombo vya habari nazisambaza vizuri jamani mbona kimya, jamani mbona mmenisahau, jamani msione mimi kuwa upinzani ni uadui.”

Mwanakwetu anajiuliza maswali mengi kwani Maria Sarungi na Mwigulu Nchemba lini wamekuwa maadui?

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Wanaogombana ndiyo wapatanao lakini na viongozi wetu mkumbuke hili baadhi ya watu wakiwa na vyeo huwa wanawakimbia baadhi ya watu wao wa zamani wakidhani kwa ujirani wao na watu hao unaweza kusababisha vyeo vyao kupokonywa, hili siyo kweli, Mungu kama kapanga uwe na cheo hicho utakuwa nacho tu na kitakuja kuondoka kwa majaliwa ya Mungu siyo hawa watu uliyokuwa nao jirani zamani tusiwatenge.

Mwanakwetu anatarajia Mwigulu Nchemba akawa anawasiliana na nduguze hawa yasije kuwa yale ya Hamsi Kigwangwala kuwa barua pepe hazijibiwi na simu hazipokelewi.

Hivyo basi Usiwakimbie Ndugu na Rafiki Zako wa zamani.

 

Mwanakwetu Upo?Kumbuka:

“Hawa Waligombana Lini?”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments