Adeladius Makwega-MBAGALA
Mei Mosi ya kila mwaka Ulimwenguni ni siku ya Wafanyakazi Dunia ambapo hupambwa kwa kuvaa sare, maandamano , mikutano , kutoa risala na hotuba ndefu na kisha wafanyakazi bora kupewa zawadi, huku vyama vya wafanyakazi uhakikisha wanachama wao wanakuwepo katika eneo linapofanyika shughuli hizo alafu hupeana posho na kama mwanachama akikengeuka na kutoshiriki siku hii posho hapati. Kwa kawaida hekaheka huanza wiki ya mwisho ya mwezi Aprili ambapo Makatibu na Wahasibu wa matawi ya vyama vya wafanyakazi huwa bize kutawanya sare na kutoa pesa benki ziwe tayari kwa shughuli hii.
Wakati haya yakifanyika katika ulimwengu wa upande wa utawala wafanyakazi wanajitoa katika vyama hivyo, wakiona havina maana tena, japokuwa awali kukiwa na simulizi nzuri namna wafanyakazi walivyopigania haki zao lakini sasa hakuna simulizi hai, simulizi mpya zinazoonesha kweli haki hizo sasa zinapiganiwa na vyama hivi kwa pumzi ile ile ya awali.
Vyama vya wafanyakazi vikitazamwa kama sehemu ya utawala wa taasisi husika. Wafanykazi wakiwatazama viongozi wa wafanykazi kama wasaka fursa, wala michango ya wafanyakazi na wasaka tonge.
Swali la kujiuliza leo hii wakati wafanyakazi hawa nduguze Mwanakwetu wanasherekea sikukuu yao, Je kwa sasa kuna umuhimu wowote wa kuendelea kusherehekea sikukuu ya wafanyakazi duniani?
Hili ni swali muhimu maana awali vyama vya wafanyakazi vilishirikiana mno na vyama vya siasa vilivyokuwa vinadai uhuru kudai haki lakini kwa sasa vyama vya wafanyakazi vinashirikiana kwa karibu na vyama tawala. Huu ndiyo ukweli, Je haki za wafanykazi kwa sasa zimetamalaki? Jibu hapanam shida zile zile ikiwamo uchache wa mishahara, mazingira magumu ya kazi na mambo mengine kadhaa.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu anaona kuwa kwa sasa kuna umuhimu wa jambo hili kujadiliwa kama kuna haja ya maadhimisho haya na pamoja kufikiria je tuwe na vyama vya wafanyakazi au la? Kama kutakuwa na mjadala hili nina hakika vyama vya wafanyakazi vinaweza kujifanyia tathmini ya uhai wake na pengine kubadilisha mienendo au kukubaliana kisha vyama vya wafanykazi vifutwe.
Upo utetezi kuwa mfanyakazi akiwa na shauri katika Mabaraza ya Usuluhishi na Uamuzi na hata Mahakama ya Kazi na Mahakama ya Rufaa vyama vya wafanyakazi vitamtetea tangu mwanzo hadi mwisho kwa gharama za chama cha wafanyakazi, hili ni kweli. Swali ni je hilo ndilo jukumu pekee ya vyama vya wafanyakazi ulimwenguni? Jibu lake hapana. Majukumu mengine yamekuwa likizo kwa muda mrefu hatusikii vyama vya wafanyakazi hata kupaza sauti juu ya changamoto za jamii.
Msomaji wangu siku ya leo Mwanakwetu aliamua kuliwaza hili kama mtu mjinga, pengine ujinga wa Mwanakwetu unaweza kusababisha sote tuwaze pamoja kumbuka Mwanakwetu alishakuwa mwanachama wa chama wa Walimu CWT na pia baadaye alikuwa mwanachama wa RAAWU isitoshe CWT alikuwa Katibu wa Tawi , huku RAAWU alikuwa mwenyekiti wa Tawi ya TBC nchi nzima na baadaye Mwanakwetu amekuwa kiongozi katika taasisi kadhaa.
Je sasa tunaweka silaha chini? Hapana, kwa hakika lazima vijana(wanangu) wasiweke nguvu zao katika vyama vya wafanyakazi bali waongeze nguvu katika vyama siasa na kuhakikkisha wanachagua viongozi wazuri. Hapana hakuna kuchagua chama chagua kiongozi unayeamini ana uwezo wa kuisadia jamii yake vinginevyo dunia haiwezi kuwa sehemu salama. Maana ni heri hizi pesa wanazokatwa wanachama wabaki nazo wanunue uga wa watoto wao.
Mwanakwetu upo ? Kumbuka:
“Kwa Sasa Hakuna Haja ya Kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257


.gif)
Post a Comment