Aliyefanya Ubaya Hana Haki ya Kuelekeza Wahanga Namna ya Kulia

 



Adeladius Makwega-MBAGALA.

Tulipokuwa tunasoma Chuo Kikuu kundi kubwa la wanachuo waliyokuwa wanatoka kaya masikini walikuwa na shida, mambo magumu na jahazi linazama hivyo wakaamua kupambana kupata haki yao iliyokuwa inawekwa mustakabali wao masomoni. Huku hapa chuoni kulikuwa na makundi kadhaa wale wenye shida ambao ni wengi na wale wasio na shida ambao walikuwa wachache, huku hawa wasio na shida ambao walionekana vijana kutoka familia bora wachache na wap waligawanyika katika makundi mawili. Wapo waliosema kuwa hao masikini achaneni nao kwanza wanatupoteza muda wetu wa kusoma, walikuja kufanya nini kusoma taasisi yenye gharama kubwa wakati wazazi wao hawana kipato?

Pia kulikuwa na kundi miongoni mwao hawa kutoka familia bora ambalo waliungana na makabwela huku wakitumua akili zao, ujuzi wao na rasilimali zao kuungana na wale masikini ili kufanikisha jambo lao.

Msomaji wangu nakuomba rejea makundi haya matatu:

Masikini ambao waliamua kujipambania kufa na kupona, wele kutoka familia bora walikuwa bize ya mambo yao na wale kutoka familia bora walioungana na masikini wakisema kuwa hawa ni wenzetu tuwasaidie.

“Kwa wanaomfahamu Mwanakwetu na namna anavyoishi yeye alikuwa kundi la masikini ambao walikuwa tia maji tia maji na jamii ilifahamu hilo lakini kwa ukweli wa Mungu Mwanakwetu hakuwa katika kundi hili Mwanakwetu alikuwa kundi lenye nafuu lakini kutoka moyoni alichukizwa na namna wale masikini wanavyofanyiwa na hapa hapa akaungana nao ili kuongeza nguvu. Huku Mwanakwetu aliweka ari ya hali ya juu kufanikisha lengo lao kulipambania.”

Wakati hili zoezi linaendelea Profesa mmoja ambaye ni marehemu akamuita Mwanakwetu na kumuuliza kwa nini hali ipo hivi? Majibu ya Mwanakwetu yalikuwa haya:

“Hivi Profesa mathalani wewe umenifanyia ubaya, je wewe uliyefanya ubaya unayo haki kunielekeza namna ya kulia?”

Profesa huyu akajibu akisema hapana, kisha akasema sawa Makwega nimekusikia na nimekuelewa.

Mwisho wa siku makabwela walifanikisha jambo lao vizuri tu huku Mwanakwetu moyoni akiwashukuru mno kundi la wale matajiri ambao hawakuwa na shida lakini waliungana na makabwela kufanikisha jambo hilo.

 

Kwa hakika hivi ndivyo TANU na ASP walivyofanikisha harakati zao.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Hapa kuna mambo mawili:

Kwa jamii wa Wapogoro familia ikifiwa huwa kunakuwa na utaratibu wa jumla wa kulia msiba huku ngoma ya msiba ikipigwa siku zote hadi mazishi, naye kila mwana ndugu analia, mwingine mchozi humtoka, mwingine ulia moyoni, kwa  namna Mungu alivyomjalia kulia. Wote mkiwa na majonzi ya msiba.

Hapa kila jamii huwa na utaratibu wake wa kulia msiba na hakuna mtu yoyote mwenye mamlaka ya kumfundisha mwenzake namna ya kulia pale anapokuwa na simanzi. Kikubwa aliyefiwa asilie na kumkufuru Mungu tu.

Kwa jambo la pili ni juu ya makundi haya matatu wale makabwela, wale wenye nafuu waliogawanyika mara mbili.

 

Katika maisha hoja siyo kuwa masikini au tajiri bali hoja ni pale unapoona kuna shida pahala Fulani unaweka jitahada zako kulitatua jambo hilo? Iwe mwenye shida wewe au mwenzako?

Unaweza ukawa masikini lakini ukawa mbinafsi, mambo yako yakiwa mazuri ndiyo basi tena au ukawa tajiri wewe ukajali maslahi yako tu. Kikubwa uwe masikini au tajiri je wewe unamtazamaje binadamu mwingine katika kila hatua anayopitia?

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Aliyefanya Ubaya Hana Haki Kuelekeza Wahanga Namna ya Kulia.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

0/Post a Comment/Comments