Wewe Unatembea na Hoteli ya Mjomba Wetu Mpaka Muda Huu Mbona Sisi Hatusemi

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Mwanakwetu kuna wakati alitayarisha makala iliyokuwa inamzungumzia IGP Mstaafu Said Bini Mwema, katika makala haya wadau mbalimbali walitoa maoni na mdau mmoja yeye alikwenda mbali na kusema maneno haya:

“Kaka Mwanakwetu, IGP Mstaafu Omari Mahita ana nafuu kubwa, huyu IGP wa sasa Afande Camilius Wambura yeye ni hatari , yaani Tanzania haijawahi kupata IGP kama yeye.”

Mwanakwetu akacheka sana maoni haya, kisha akawa anayatafakari mwenyewe akilini mwake mawazo ya ndugu huyu. Mwanakwetu akilini mwake alimkumbuka Dkt. Aisha Mahita ambaye alikuwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga na mwaka wa 2016-2018 walifanya kazi pamoja na Mwanakwetu.

Siku moja Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati huo Mheshimiwa Martine Shigella alifanya kikao na viongozi kadhaa wa wilaya zote na Halmashauri zote za Mkoa wa Tanga, kikao hiki bahati nzuri kilifanyika Lushoto Mjini.

 

Siku hii kikao kilikuwa na ajenda nyingi mojawapo ni ajenda ya Ujenzi wa Stoo za Dawa(Buffer Stoo) katika kila Hospitali za Halmashauri ya Wilaya. Hii ni ajenda ya Katibu Tawala Mkoa wa Tanga wakati huo Injinia Zena Said , huku Dkt. Aisha Mahita Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati huo yeye aliwasilisha kwa niaba ya Katibu Tawala na watekelezaji wa ajenda hii ni Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya za Mkoa wa Tanga wakati huo kama vile Dkt. Nyaronga, Sabas, Haule, Kapteni Peter Nyalali, Jumanne Kiango Shauri, Mwanakwetu na wenzao kadhaa. Kazi hii ilifanyika bila bajeti maana Mkuu wa Mkoa wa Tanga aliagiza kazi hiyo ifanyike kwa dharura mara moja kila halmashauri itatufute chanzo ili pawepo na stoo ya dawa kulinda uhai wa wananchi wa Mkoa wa Tanga.

Wakati wa ufuatilijia Dkt Aisha Mahita analizunguka Wilaya zote na siku hii alikuwa anawasilisha namna agizo lilivyotekelezwa.

Ukishawalisha unapigwa maswali na unajibu kisha unarudi ulipokaa. Dkt Aisha alipokuwa akirudi kuketi Mkurugenzi mmoja wapo akawa anamtania:

“Dkt Aisha umejengewa Buffer Stoo Mkoa mzima bila bajeti pesa hakuleta lazima urejeshe.”

Dkt. Aisha Mahita akawa amechukizwa na kusongwasongwa na maneno haya, huku akijibu:

“Tumieni mapato ya ndani…Hawa wakurugenzi wa John Pombe Magufuli wananisumbua sana, yaani wanataka kuniharibia kazi, sijuhi Rais Magufuli kawatoa wapi?”

Wakurugenzi wakawa wamekakasirika sana huku Dkt. Aisha alikuwa bize na kikao cha usiku huu mara kadhaa anatoka anakwenda chumba kingine. Wakurugenzi wakawa wanamfuatilia baadaye ilibainika kuwa Dkt Aisha Mahita kumbe alikuwa ananyonyesha.

Aliporidi kikaoni, Wakurugenzi wakampiga kijembe Dkt.Mahita:

Ashakumu si matusi:

“Wewe mwenyewe mbona haueleweki, mpaka saa hizi bado unatembea na chakula cha mjomba? Kakae jirani na mjomba wetu umpe mkahawa wake.”

Dkt .Aisha Mahita akapita zake na kwenda kukaa jirani na mlango wa kutoka huku safari za ingia toka za kumpelekea mjomba wa akina Mwanakwetu hoteli yake zilikuwa haziishi. 

 

Jamaa mmoja akasema huyu Dkt. Aisha Mahita haeleweki kaka baba yake IGP Omari Mahita.

Kikao hiki kikaendelea hadi saa tano usiku, kisha kila mmoja kurudi hotelini alipofikia na yeye Mwanakwetu alirudi katika makazi aliyokuwa anaishi.

Haya ni maisha ya kidugu watu wanataniana na hata katika kundi la Whasaap la Katibu Tawala Mkoa wa Tanga na Wakurugenzi, utani ulikuwepo na kulikuwa na akina mama wawili Katibu Tawala mwenyewe na Mkurugenzi wa Muheza. Katibu Tawala wa wakati huo Injinia Zena Said muda mwingine alikuwa anaingilia kati akisema maneno haya:

“Jamani kaka zangu …haya mambo yenu punguzeni… humu mpo na dada zenu.”

Mwanakwetu anasema nini Siku ya leo?

Haya Mwanakwetu ameyakumbuka tu,  msomaji wangu kumbuka katika kikao kile pale Lushoto cha viongozi Mkoa wa Tanga nyuma ya pazia waliokuwapo Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Tanga na Dkt. Aisha Mahita aliyekuwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga walivyokuwa wakirushiana tambo za maneno:

“Dkt Mahita haeleweki kama Baba yake…Dkt Mahita anatembea na Mkahawa wa Mjomba wetu… Sijuhi Rais Magufuli hawa Wakurugenzi kawatoa wapi?”

Hizi ni tambo za maneno kwa watu wanaolewana kazini, maana watu wenye chuki hawawezi kutaniana kabisa kila mtu yu kimya.

 

Katika kisa hiki iwe kweli Dkt. Aisha Mahita ni mtoto wa IGP Mstaafu Omari Mahita au kufanana majina tu, kwa vyovyote vile Dkt. Mahita alibeba lawama za IGP Mahita. Kwa hakika IGP Mstaafu Omari Mahita anaweza kuwa mkakamavu, mstamilivu lakini je watoto wake, vijana wake wajukuu zake, ndugu zake wanaweza kuwa na roho hiyo? Hawawezi kuwa na roho hiyo.

Swali hili kama lilivyo linaweza kumuangikia IGP Camilius Wambura kwa jamaa zake iwe leo, iwe kesho , kesho kutwa au mtondo go.

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Wewe Unatembea na Hoteli ya Mjomba wetu Mpaka saa hizi Mbona Sisi Hatusemi.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

 

 














 

 

0/Post a Comment/Comments