Wazee Wangu Baba na Mama Zangu

Adeladius Makwega-MBAGALA

Mwanakwetu amekuwa akiifuatilia kwa karibu mno hii Tume ya Matukio yalitokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata inayongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Othuman Chande, huku Mwanakwetu akiwa na matumaini yaliyofubaa yenye kuchujuka kila siku na huku akiwa na huzuni kwa mzee wake Jaji Mkuu Mstaafu Chande mwenyewe pamoja na wajumbe wake mara baada ya kuimaliza kazi hii hali itakuwaje? Huu ni wasiwasi wa Mwanakwetu hasa taarifa yenyewe itakavyokuwa na je matumizi ya taarifa hiyo iwe kwa Watanzania wenyewe na hata nje ya Tanzania, je kazi hii itaheshima au itadharaulika?

 

Huku ukitazama umri wa wajumbe wote katika tume hii utagundua kuwa ni mkubwa tangu kwa Jaji Mohammed Chande aliyezaliwa Januari 1, 1952(74) na wenzake ambapo Profesa Ibrahimu Juma Jaji Mkuu Mstaafu aliyezaliwa June 15 1958(68), Balozi Mtaafu Ombeni Sifue aliyezaliwa Agosti 26, 1954(72) , Balozi Mstaafu Radhia Msuya inakadiliwa umri wake ni zaidi ya miaka 70, Balozi na Luteni Jenerali Mstaafu Paulo Meela aliyezaliwa mwaka 1955(71) IGP Mstaafu Said Mwema aliyeliwa mwaka 1953(73), Dkt Stegomena Tax aliyezaliwa Julai 6, 1960 (66) na Balozi David Kapya aliyezaliwa mwaka 1965(61).

 

Msomaji wangu siku ya leo naomba twende taratibu maana tunakwenda kwenye tarakimu, haya ni mahesabu: Hawa ndugu wanane umri wao kwa utafiti wa Mwanakwetu ni huu:

“Chade 74, Tax 66, Mwema 73, Meela 71, Msuya 70, Sifue 72, Profesa Juma 68 na Kapya 61.”

Ukichukua umri wa kila mmoja wa wajumbe hao na kujumlisha jumla unapata miaka 555 na ukigawanya na idadi yao unapata miaka 69.375. Huu ni umri wa wastani.

 

Wanasaikolijia wanasema kuwa watu wenye umri huo wanakuwa na hekima na huwa ni watu waliyeridhika lakini kibaya zaidi watu wenye umri huo huwa wameshatafuta  maisha na kama kupata wamepata. Hivyo basi huwa ni waoga mno wa kupoteza kile walichonacho maana hawana uhakika wa kurudi kutafuta maisha. Hata baadhi ya watu uamini kuwa kundi la umri huu siyo hekima siyo sahihi kuwahusisha na mambo ya haki za jamii hawawezi kuangalia maslahi ya umma.

Msomaji wangu kumbuka bado Mwanakwetu yupo katika takwimu:

“Kwa mwaka wa 2026 inakadiliwa kuwa idadi ya Watanzania inaweza kufika 72,363,780 huku Watanzania wanaoishi mijini ni milioni 29.6. Takwimu hizo zinadai kuwa Watanzania wenye umri kati ya umri sufuri hadi miaka 14 ni kati ya asilimia 42-44, Watanzania wenye umri wa kati ya miaka 15-64 wastani wa asilimia 52-54 na Watanzania kati ya miaka 64 na kuendelea ni asilimia 3 tu.”

Taarifa hii inakwenda mbali mno ikisema wastani wa umri wa kuishi wa mtanzania ni miaka 67.6 wakati wanawake wastani wao ni miaka 70.4 na wanaume ni miaka 64.8.

Mwanakwetu anaamini kuwa wajumbe wa tume hii kwa umri huo Mwenyeezi Mungu kawajalia sana uhai na hili wamshukuru Mungu.

 

Mwanakwetu(adeladius francis makwega) amezaliwa Septemba 19, 1974, umri wake wakati anaandika makala haya ni miaka 52 na miezi 6 huku umri wa Baba yake ambaye anaitwa Francis Fidelis Makwega amezaliwa Oktoba 20, 1950 (76) na umri wa mama yake anayejulikana kama Doroth Hezron Mlemeta amezaliwa Oktoba 29, 1956 amefariki kama angekuwa hai leo hii angekuwa na miaka 70.

Kwa hesabu ya wastani wa umri wa wazazi wa Mwanakwetu ni 76 jumlisha 70 unagawanya kwa mbili jibu lake ni 73.

Kwa hiyo wajumbe wa tume ya Kilichotokea Oktoba 29, 2025 na Siku zilizofuata kwa Mwanakwetu hawa ni baba na mama zake kabisa na ni kwa kigezo kimoja tu cha ujirani wa umri ule wa wastani wa wajumbe wa tume hii ambao ni miaka 69 na ile ya umri wa wastani wa wazazi wa Mwanakwetu yaani miaka 73. 

 

Mwanakwetu kwa heshima na taadhima anaomba wajumbe wa tume hii awaambie maneno haya:

Kazi mnayoifanya inazidi dhamana zote mlizowahi kufanya katika maisha yenu na kazi hiyo kama mkiifaya vibaya inaweza kuwaletea kero na mkajilaumu kwanini hamkuikataa wakati mnateuliwa kwa ushauri wa Mwanakwetu ambaye ni mtoto wenu wa hiari ili msiingie kwenye kujilaumu nafsini mwenu naomba ifanyeni kazi hiyo kwa moyo wote huku mkimbuka kuwa asilimia 97 ya Watanzania ambao wana umri mdogo ambao ni watoto wenu(akina Mwanakwetu), wakujuu zenu na vitukuu vyenu wanawategemea na kundi hilo ndiyo wengi waliopata tabu kadhia hii ilipotokea.

 

Mwanakwetu anatambua kuwa kati wa wajumbe nane ni wajumbe wawili tu ndiyo wanaonekana wazi kuwa waliwahi kuhudumu katika vyombo vya Ulinzi na Usalama ambao IGP Mstaafu Said Mwema na Balozi Luteni Jenerali Paul Meela lakini Mwanakwetu anaamini idadi ya wajumbe wenye sifa hiyo inawezekana kuwa zaidi ya wajumbe hao ambao wanatoka taasisi zingine za Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Wazee wangu, baba zangu na mama zangu, wajumbe wote mkumbuke hamuifanyii kazi taasisi yoyote ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama kazi hii, bali kazi hii mnawafanyia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiyo waliokadhiwa nchi hii Disemba 9, 1961.

Wazee wangu, baba zangu na mama zangu jambo la mwisho naomba niwambie hili kunaweza kutokea kukubaliana au kutokukubaliana katika tume yoyote ile, hili ni jambo la kawaida.

 

Kama kuna kutokukubaliana nawashauri msisite kulisema hilo , miaka 69 ya uhai ni bonasi tu Mwenyeezi Mungu amewapa, toeni hoja zenu mbele ya mwenyekiti wenu na pendekeza kile mnachoamini ni sahihi wakati wa kikao ili kuhakikisha kazi hii inakuwa iliyotukuka na kuna kutokubaliana yaandikeni kwenye kumbukumbu za kikao. Ikiwa changamoto zinaendelea, ombeni kupiga kura rasmi au katika hali ya kutokukubaliana zaidi ya hapo kwa misingi ya hoja angalieni dhamiri zenu, msisite kujiuzulu kutoka kwenye tume hiyo maana kujiuzulu itakuwa salama zaidi kuliko kubaki wakati haukubaliani na mwenendo wa mambo.

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu anazungumza na wazee wake, baba na nama zake wa hiari: Jaji Mkuu Mstaafu Mohammed Othuman Chande, Jaji Mkuu Mstaafu  Profesa Ibrahimu Juma, Balozi Mstaafu Ombeni Sifue, Balozi Mstaafu Radhia Msuya, Balozi Mstaafu na Luteni Mstaafu Paul Meela, IGP Mstaafu Afande Said Mwema, Dokta Stegomena Tax na Balozi David Kapya.

 

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Wazee Wangu Baba na Mama Zangu.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 




























 

0/Post a Comment/Comments