Watasimulia Nini Dhidi ya IGP Camilius Wambura?

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Hii ilikuwa Machi 21, 2026 Mwanakwetu aliamka mapema sana huko kwake , huku akiongea na ndugu yake mmoja wa Mahenge Ulanga akiuliza kaka mbona haupatikani? Mwanakwetu aliongea naye ndugu huyu, huku ndugu huyu ambaye ni Muisilamu akisema kuwa Baraza la Waisilamu Tanzania BAKWATA linawayumbisha sana:

“Sasa linatuingiza katika ubishani wa mambo ambayo yalitakiwa kuamuliwa vizuri na wakubwa wetu…wao ndiyo wakubwa, sasa wenzetu Kenya Wanasema Iddi jana sisi huku tunasema Idd leo…Haya mambo yanatugawa mno.”

Msomaji wangu tambua kuwa nyumbani kwa Mwanakwetu kwa asili ya mababu na mababu kwa ukoo wa baba yake ni Kijiji cha Ikangao ambapo hapo kuna jamii kubwa mbili Wakristo na Waisilamu tangu enzi, huko ndipo anapotoka Aishi Manura Tanzania One ,mchezaji wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania.

 

Baada ya mazungumzo haya akilini mwa Mwanakwetu ilimjia taswira ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2010 ambapo pale TBC Taifa vipindi vyote vilisimamishwa alafu kukawa kunarushwa matangazo ya uchaguzi huku zikisomwa taarifa za habari tu, kutoka TBC Mikocheni. Watangazaji na watayarishaji vipindi wa TBC walipangiwa majukumu: Hapa wale wa mikoani walitakiwa kukusanya taarifa ya hali ya uchaguzi huo huko walipo na wale waliokuwepo Dar es Salaam walipangiwa kazi ya kuzunguka mitaani. Siku hii Mwanakwetu alikuwa katika gari maalumu la TBC Taifa ambalo lilipangiwa kupita Ubungo na Ilala kuzunguka vituo kadhaa vya maeneo haya mawili.

“Tulipofika ubungo tulitembelea Shule ya Msingi Mlimani ambapo palikuwa kituo cha kupiga kura, hapa tulizungumza na wapiga kura, wasimamizi na wagombea.”

Hali katika kituo hiki ilikuwa ya utulivu sana na wa kwanza aliyeisogelea mikrofoni ya Mwanakwetu alikuwa ni Martha Josephy Jally, yeye alikuwa ni msimamizi wa kituo kimoja hapa shuleni, mama huyu aliyekuwa mweupe sana alisema maneno haya:

“Hali ni ya utulivu sana, huku wapiga kura wakipiga kura zao kwa amani, tangu asubuhi sijaona askari anabishana na wala kumsukuma au kumkamata mwananchi yoyote yule, ndani ya kituo changu mawakala wa CUF, CHADEMA na CCM wapo wanafuatilia hali ya uchaguzi ilivyo.”

Mgombea wa Ubunge wa Jimbo hili kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Mtatiro aliposogelewa Mikrofoni ya Mwanakwetu na yeye alisema hali ilikuwa ya utulivu, huku wananchi wanapiga kura. Mwanakwetu na wenzake walizunguka vituo kadhaa na kisha kwenda Ukonga Mombasa ambapo kulikuwa na shule ya Msingi moja jirani na FFU Ukonga, hapa hali ilikuwa ya utulivu mno wananchi wakipiga kura.

Siku hii katika uchaguzi huu Mwanakwetu aliambiwa hili, kulikuwa na tukio moja la kushangaza huko Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, kijiji kimoja kilichokuwa karibu na mpakani wa Tanzania na Burundi Msimamizi wa Uchaguzi katika katika kituo kimoja cha shule moja ya Msingi aliyefahamika kama Maria Katabuhaga alimdokeza Mwanakwetu kuwa walikaa katika kituo hicho siku nzima wananchi hawakujitokeza kupiga kura kabisa, kijiji hiki wananchi walikuwa na malalamiko yao ambayo hayakufanyiwa kazi, hivyo hasira zao zilihamishiwa kugomea kupiga kura. Muda wa kufunga kituo ulipofika Mwalimu Mariam Katabuhaga na wenzake walifunga kituo na baadaye kukabidhi makaratasi ya Uchaguzi Mkuu kwa viongozi wao.

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu alikuwa katika mzunguko ndani ya gari lile baadaye Mwanakwetu aliomba ruhusa ili akapige kura nyumbani kwao Mbagala ambapo siku hii alipiga kura Shule ya Msingi Mbagala na kisha kurudi nyumbani kwake huku hali ilikuwa ya utulivu.

 

Mwanakwetu kwa nini amesimulia haya mambo matatu?

Kwanza ni malalamiko ya Muisilamu huyu wa Mkoani Morogoro haya malalamiko Mwanakwetu anayacha kama yalivyo. Pili ni hiki kisa cha Uchaguzi Mkuu cha wananchi waliogomea kupiga kura kule Kigoma mwaka wa 2010 watu walikuwa na hasira na tatu hali ilivyokuwa ya utulivu na wakati huku Jeshi la Polisi Tanzania lilikuwa likiongozwa na Afande Said Bini Mwema.

 

Hali hii ya uchaguzi wa utulivu ya mwaka wa 2010 iliwavutia mno Watanzania kuliko hali ilivyokuwa Uchaguzi Mkuu uliyotangulia ambapo awali Jeshi la Polisi Tanzania lilikuwa chini ya Afande Omari Mahita.

Mwanakwetu kwa makala haya anajiuliza tu, je Watanzania waliona vituko, balaa na misukosuko na hekaheka za uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2025 watasimulia nini dhidi ya Afande Camilius Wambura? Kama ndugu yetu Afande Said Bin Mwema hata kama ana madhaifu lakini yeye yalikuwa nafuu.

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Watasimulia Nini Dhidi ya Afande Camilius Wambura?”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257












 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments