Adeladius Makwega-MBAGALA.
Hii ilikuwa ni asubuhi ya Machi 31, 2026 siku ya mwisho ya mwezi Machi, Mwanakwetu alipokea ujumbe huu:
“Leo tupo St Justine Kituo cha Wenye Ulemavu Makoko, Musoma Mkoani Mara…”
Mwanakwetu alipopokea ujumbe huu aliulizia kilipo kituo hiki naye Gideoni Musa Chilongani ambaye ni Afisa Usafirishaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara alisema hafahamu kilipo. Majibu hayakupatika lakini ndugu Chilongani alimpigia simu Bi. Neema Ibamba Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, yeye alitoa maelekezo sahihi na hadi Mwanakwetu akafika eneo hili ambapo watumishi wawili wa Ofisi ya Waziri Mkuu walikuwa wakitoa mafunzo ya vitendo ya namna bora ya kuingiza takwimu za wenzetu wenye mahitaji maalumu.
“Tulifika katika majengo ya taasisi hii na kupokelewana Sista Regina Linda ambaye alikuwa akisimamia kupakuliwa chakula kingi katika baseni kubwa. Huku mabinti kadhaa walikuwa wakishona nguo. Hapa Mwanakwetu akajiuliza mbona watu ni wachache machoni mwangu na chakula kilichopikwa ni kingi?Mbona hawa ndugu zangu wanafanya isilafu ya chakula? Swali la moyoni hakuna aliyesikia na kisha Sista Regina Linda kumpokea Mwanakwetu na kunielekeza walipo watumishi wale kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.”
Hapa Mwanakwetu alikaribishwa katika ukumbi mkubwa ambapo kulikuwa na viti kadhaa, huku usajili wa wenzetu wenye mahitaji maalimu ukifanyika, nyaraka zikijazwa katika karatasi na mfumo ndani ya kompyuta, picha zikipigwa na kuingizwa katika mfumo.
“Hapa kinachofanyika ni kuingiza takwimu katika mfumo wetu kwa kila muhusika mwenye mahitaji maalumu na kinachofanyika leo ni kufanya kazi kwa vitendo baada ya mafunzo haya kufanyika kwa nadhalia kwa siku za awali.”
Haya yalisemwa na Josephy Humphrey afisa TEHAMA Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Kwa hakika Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mara wanaendelea vizuri na mafunzo haya na hili la kuingiza takwimu kwa vitendo wamelifanya vizuri, kila mmoja kama mafunzo yalivyotolewa. Binafsi ninatoa heko kwa Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mara.”
Haya yalisema na Bruno Mwakibibi ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Kwa sasa kazi hii nimeelewa na nina hakika nikirudi Halmashauri wa Wilaya ya Musoma nitaifanya vizuri na nitayafikia malengo niliyojiwekea kwa wakati.”
Haya aliyasema Elia Yahya Mshuza ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Kwa upande wake Nuhu Agustino ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Musoma alisema kuwa mafunzo haya yamempa mwanga mkubwa kwake na kazi hii inakwenda kurahisisha mno ukusanyaji wa takwimu na kufanikisha watu wenye mahitaji maalumu kufikiwa na kupata mahitaji yao kwa haraka.
Kwa upande wake Kabeba Charles Naiga alisema kuwa sasa kazi hii kupitia mfumo imekuwa nyepesi na haina tena ugumu kwake.
Mara baada ya pita pita hiyo Mwanakwetu alirudi kwa Sista Regina Linda na kuzunguka naye katika kituo hiki kinachomilikiwa na watawa kwa Kanisa Katoliki wa Shirika la Masista wa Imakulata wa Afrika lenye makao yake Makuu hapa Jimbo Katoliki la Musoma.
Katika makazi haya kulionekana kunafanyika shughuli nyingi ikiwamo mafunzo ya lishe na kazi zingine, huku wenzetu wenye mahitaji maalumu walioneka wakifanya shughuli zao vizuri.
“Hapa tuna changamoto ya bweni maana tunahitaji kuwa na bweni kubwa, hapa jengo linalotumika kama bweni ni bwalo la chakula na Mungu akitujalia kama tutapata nguvu zaidi tutajenga bweni lenyewe kwa ajili ya hawa wenzetu.”
Hapa hapa Mwanakwetu alikumbuka kuwa kumbe chakula kile kingi ambacho Sista Regina Linda alikuwa akikipakua kilikuwa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika kituo hiki na kwa bahati mbaya Mwanakwetu hakualikwa kula chakula hiki kabisa nadhani bajeti yake haikuwapo
Hadi Mwanakwetu anaondoka alikuwa akipiga miayo mara baada ya kuona wali ule mwingi uliojaa katika beseni na kwa hakika siku nyingine kama Mwanakwetu akijaliwa kwenda kituo cha Mtakatifu Justine atakwenda kula na wenzetu wenye mahitaji maalumu wanaolelewa katika kituo hiki cha Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu ameshuhudia mafunzo haya ya Maafisa Ustawi wa jamii yakitolewa vizuri na kwa ustadi mkubwa na jambo la msingi siyo kuhifadhi takwimu katika mfumo tu bali wenzetu wenye mahitaji maalumu wapatiwe mahitaji yao ikiwamo hata elimu ya namna ya wao wenyewe kuendesha maisha yao.
Jambo pili ambalo Mwanakwetu ameliona ni mahitaji ya Bweni katika kituo hiki cha Mtakatifu Justine na kwa yoyote mwenye mapenzi mema na wenzetu wenye mahitaji maalumu anayewiwa kuwasaidia ndugu na taasisi hii anaweza kuwasiliana na Baba Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Wali Mwingi Uliojaza Baseni.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
NB Makala haya ni maalumu kwa heshima ya Bi Neema Ibamba Mkuu wa Sehemu ya Maaendeleo ya jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.














.gif)
.gif)
Post a Comment