
Adeladius Makwega MBAGALA.
Wakristo wameambiwa kuwa utaratibu wa namna ya mwongozi wa Ibada ya Misa ulivyo katika Kanisa iwe kuitikia, kupiga magoti au kukaa huo ni mwongozi ambao unamtaka kila muumini kuufuata isipokuwa kwa wale waamini wenye dharura tu. Haya yamesemwa Jumapili ya Tano ya Kwaresma na Padri Thomas Akello Machi 22, 2026 katika Kanisa Dogo la Warosimini Parokia ya Lushoto Jimbo Katoliki la Tanga.
“Unaweza kumuona muumini, wenzake wanapiga magoti yeye amesimama, huu ni mwongozi wa Kanisa tangu enzi, lazima ufuatwe huku ikifahamika dharura zipo.”
Akihubiri katika homilia ya Ibada hii ya Misa Padri Akello alisema kuwa Yesu wakati anamfufua Lazaro alilia, hili linaonesha kuwa Yesu Kristo aliishi katika maisha ya ubinadamu kamili huku akihuzunika na shida walizopata watu waliomzunguka:
“Dunia ya leo ina changamoto nyingi wakimbizi vita, magonjwa na mambo mengine je mimi na wewe tunazipokeaje changamoto hizi kwa walio jirani nasi na wenzetu wengine? Je tunazifurahia au tunawasaidia katika kuzitatua, lazima Wakristo tushiriki kuzitatua changamoto za wenzetu.”
Akigongelea msumari mkubwa wa mahubiri yake Padri Akello alisema kuwa mwanadamu anakabiliwa na kifo lakini kusudio la Mungu siyo mwanadamu afe, bali aishi milele lakini dhambi ndiyo iliyosababisha mwanadamu aingie katika kifo.
“Kifo siyo kile tu cha kimwili tu bali hata pale binadamu anapofika mwisho ambapo kwa hali ya kibinadamu huoni njia yoyote ile na hauoni njia mbadala, katika hili kama haujakutana nayo hali hiyo itakuja tu huku Yesu akisema kuwa yeye ndiye kimbilio.”
Padri Akello alisema kuwa katika Injili ya jumapili hii Yesu anapoambiwa kuwa rafiki yake Lazaro anashida kwanini anafanya katika hali ya kustajabisha! Tujiulize kwanini alikaa siku mbili bila ya kwenda huko? Kisha baaaye ndiyo anakwenda huko?
“Kibinadamu kama rafiki yako unampenda , lazima ungewahi ili kujua hali ilivyo na ujue cha kufanya, lazima utakuwa na shauku ya kwenda lakini lazima tutambue kuwa njia ya Mungu siyo njia ya mwanadamu.”
Padri Akello katika hili alitoa mfano wa rafiki yake mmoja ambaye alikuwa na umri miaka karibu 60 na mama yake mzazi alikuwa na miaka kama 80. Siku moja rafiki huyu wa Padri Akello huko India akapigiwa simu kuwa mama yake yule ajuza ni mgonjwa sana, mahututi , hoi bini taabani. Rafiki huyu wa Padri Akello aliomba ruhusa ya kwenda kumuona mama yake mgonjwa, kwa bahari mbaya mara alipopewa ruhusa alipokwenda kubuku tiketi ya ndege ya siku hiyo alikosa , akapata ndege ya kesho yake. Kesho yake alipokwenda uwanja wa ndege haikufika. Wakati haya yanafanyika hata simu ya kuuliza hali ya mama yake ikoje , simu hazikuwepo. Kesho yake ndege aliyopaswa kupanda alichelewa na ndege ikaondoka.
Balaa juu mabalaa yalimsonga ndugu huyu. Ndege ile iliyomuacha iliendelea na safari na kwa bahati mbaya ndege ilianguka Bahari ya Hindi wakati inakwenda India kwao. Aliposikia hili la ndege iliyomuacha kuanguka ndugu huyu alistaajabu mno, alishangazwa sana. Mungu bahati alipata ndege siku iliyofuata na alifika India kwa mama yake na kumkuta mama yake yu mzima na mara alipomuona tu ajuza huyu hali ya kiafya ilizorota na baadaye mama huyu alifariki dunia. Haya yakiwa maajabu ya Mungu. Huku rafihi huyu wa Padri Akello alishiriki mazishi na baadaye kurudi kule alipotoka.
Katika hili Padri Akello alisema kuwa:
“Hata kama tunaomba kitu kwa Mungu siyo kwamba hasikii bali Mungu ana malengo yake katika kila jambo. Maneno ya Injili ya leo yanasema Bwana Kama ungalikuwa hapa ndugu yangu asingalikufa lakini Yesu anamwambia lolote utakalo mwambia Bwana hakika atasikia.”
Ibada hii ya Misa iliendelea vizuri hadi tamati katika Kanisa hili Dogo la Warosimini linaloweza kukusanya waamini walioketi kama 150 ambalo lilijazwa na wanovisi kadhaa, watawa wakike wanne maburuda wawili na waamini wa kawaida wawili na mwishoni wa Ibada hii ya Misa wageni wawili walitambulishwa.
Wakati haya yakiendelea hali ya hewa ya mji wa Lushoto ni nyuzi joto 21, unyevunyevu ni asilimia 60, ujirani na mvua ni wa asilimia 87 na upepo ukivuma kwa KM 5 kwa saa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Waamini Fuateni Mwongozo wa Liturujia.”
Nakutakia Siku Njema.
makwadeladius @gmail.com
0717649257







.gif)
.gif)
Post a Comment