Adeladius Makwega MBAGALA
Eneo hili analotoka msafari huyu lilikuwa la milimani ambapo kuna maji mengi yanayotiririka kuelekea bondeni, huko milimani wakilima mazao kadhaa ya mbogamboga; nyanya, karoti , vitunguu, pilipili hohoho, kabichi, koni flawa na brokoli . Majira haya ya milimani ni baridi na majira ya bondeni ni ya joto, hivyo basi watu wa milimani wenye uwezo wa kipato wana mashamba bondeni maana mazao yanayolimwa milimani ni tafauti na yale ya bondeni.
Msafiri huyu alitoka kwake milimani asubuhi na mapema akabeba mfuko wake wa nguo kadhaa na kuanza kutembea kwa mguu mwendo wa kushuka mlima kwa dakika 50, kisha akafika pahala penye kijito cha maji, akazivua zile nguo zilizotapakaa tope, akaoga na kuzifua nguo zilizotapakaa tope na kuvaa nguo zingine mpya na kisha kusogea barabarani ili apande basi aende huko aendapo. Msafiri huyu akawa kando ya barabara kubwa ya lami kugonja basi hilo kwa muda kidogo .
Msomaji wangu nakuomba ukumbuke haya:
“Huyu msafiri pale alipovua na kufua nguo zake alizotoka nazo milimani ambazo mara zote hujaa tope kutokana kupiga mieleka ya hapa na pale, Watu wa Milimani Mieleka Jambo la Kawaida. Hapa kama kuna nyumba jirani nguo hizo zinaanikwa ili ukirudi unazikuta zimekauka unavua nguo za mjini kisha unazivaa nguo za kupiga mieleka , hizi nguo za milimani kama hakuna nyumba jirani unafanya mambo mawili; unazificha kichakani katika mficho huku zikitiririka maji na kama siyo hivyo basi unaziweka katika mfuko kisha unasafiri nazo.”
Huu ndivyo watu wa milimani wanavyosafiri.
Huyu msafiri akangoja basi kwa dakika tano kisha likaja, akaingia basini nakulipa shilingi 5000 ya Kitanzania ambayo ni sawa na dola mbili za Kimarekani kwa mwaka wa 2026. Safari ndani ya basi ilitumia karibu dakika hamsini na jamaa huyu kushuka hapo na kukaribishwa na mandhari ya vijana wengi wanaofanya biashara ya bodaboda, hapa bila hiana alimchagua kijana mmoja makini ambaye anamuamini sana ili amfikishe huko aendapo. Kweli kijana huyu akambeba huyu jamaa na kuelekea shambani kwake ambapo kwa mguu ni mwendo wa saa karibu tano lakini kwa pikipiki ni dakika 50 tu, safari hii wakaenda mwendo wa dakika tano mara tano yaani dakika 25 ikiwa ni nusu ya safari hapa hapa wakakutana na mto mkubwa wenye maji tele lakini ulikuwa mto wa masika.
Kijana mwendesha pikipiki akasema maneno haya:
“Ndugu yangu, haya maji ni mengi na mara nyingi tunavuka hapa lakini leo maji haya ni ya hatari mno, hadi nywele zangu zinanisisimka, ngoja turudi, turudi nyuma, kisha kuna njia nyingine ya kuzunguka, hiyo njia ilivyo ni kama hapa maji yakiwa mengi kule huwa ni machache.”
Kweli jamaa huyu abiria akakubali, pikipiki ikageuzwa na kurudi nyuma kwa dakika karibu 20 na kisha kuanza safari na njia hii mpya kuelekea shambani kwake. Kijana huyu wa pikipiki aliendesha kwa nusu saa na ndipo walifika eneo lile lenye mto unaopitisha maji ambao unayapeleka kule walipokutana awali na mto mkubwa pale waliposhindwa kuvuka.
Hapa walikaribishwa na ngurumo za maji yakitiririka huku mvuto wa maji haya ulipambwa na saiuti ya ndege wa bonde hili maarufu la kilimo cha mahindi na mpunga. Muda huu ukiwa kama saa mbili na nusu ya asubuhi. Kijana wa pikipiki akasema:
“Ndugu yangu shuka , maana hapa hata mimi naikokota hii pikipiki maana haya maji nayo siyo machache ila yana nafuu na njia za kupita hapa mimi nazifahamu wakati maji yakijaa…lakini kumbuka unapovuka maji yanayotembea ambayo ynavuka magoti yako, usinyajue miguu yako, kama unapiga hatua mbele wewe fanya kama unauburuza miguu yako mmoja baada ya mwingine , unapopiga hatua kama unatembea nchi kavu maji yatakupiga mweleka, sasa hivi utasombwa na maji tutakusahau…”
Kweli huyu jamaa wa milimani alitii maagizo vizuri na kweli walivuka salama na kutembea kwa miguu mwendo wa dakika kama tano kutokana na matope ya hapa na pale na walipokuwa wanataka kupanda pikipiki hii wakaona kundi la watu watano wanaume, wana mapanga mikononi. Kijana wa Pikipiki akawasalimu na kuwauliza jamani mbona mapema hii mnarudi nyumba mapanga? Wanaume Mmelima Saa Ngapi?
Jamaa mmojawapo ambaye alikuwa mkuu wa msafara akajibu:
“Jana kuna mwezetu tulimuacha shambani analima baadaye mvua ikanyesha sasa hakurudi nyumbani, hivyo tumekuja kumsaka tangu alfajiri sasa tunamuangalia katika mto huu, pengine isije ikawa wakati anarudi nyumbani alisombwa na maji ya mto huu wa masika… au ameliwa na mambo hapa tupo kazini tangu alfajiri tunamtafuta…”
Jamaa hawa walipewa pole na hawa ndugu na kisha kupanda pikipiki yao kuelekea kule shambani, ndugu huyu alifika shambani kwake alichukua mzigo wake wa magunia matano ya mpunga na kuyafikisha pale stendi ambapo kulikuwa na mashine ya kukoboa, hapa aliukoboa mpunga wake na kupata kila hamisini hamsini tano za mpunga akiwa na kilo 250. Mzigo huo ukasogezwa kituo cha basi ili kupandishwa kwenda milimani. Kijana huyu wa bodaboda alilipwa shilingi 50,000 ya Kitanzania kwa kazi hii ambayo ni sawa dola 20 za Kimarekani. Jamaa alipanda basi na kufikisha mzigo wake hadi pale alipopanda basi asubuhi. Huu mchele ukagawanywa katika ujazo wa kilo 25 kukawa na mifuko 10, vijana kumi wakaibeba mizigo hiyo kuelekea kule milimani nyumbani kwa huyu ndugu. Ndugu huyu alivua nguo zake alizotoka nazo ndani ya basi na kuvaa nguo zake misurupwete za kupanda mlima na kuwafuata vijana waliobeba mizigo yake hadi mlimani na kufika salama safari yake.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika msomaji wangu ili kuweza kusafiri katika baadhi ya safari yako masharti ya kufuata lazima yazingatiwe mathalani kuna nguo za kuvaa katika eneo za tope, kisha unaoga kubadilisha nguo hizo na kuvaa nguo nadhifu ili uonekane binadamu kwa wenzako ndani ya basi, kisha unapotembea eneo lenye maji, maji yakiwa juu ya magoti usinyanyue miguu unatakiwa kuiburuza, kama utanyanyua miguu maji yatakupigwa mweleka na kisha utasombwa na maji na kufariki, ili uwe salama acha ukaidi tii masharti ili uweze kufika salama safari yako. Angalia huyu kijana wa milimani alivyo makini tangu mwanzao wa safari hadi mwisho wa safari anatii masharti huku akikaa vizuri na wenzake safarini huku akiwatendea haki ya usikivu na hata kuwalipa ujira wao.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Unapotembea Katika Maji yaliyo Juu ya Magoti Buruza Miguu.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257






Post a Comment