Unamjua Mary Machogu Mwadili wa Wanachuo Chuo cha Ualimu Bunda?

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Siku hii Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi alikuwa akifanya uzinduzi wa kumezeshwa kwa dawa za Kichocho na Minyoo Kwa mkoa wa Mara kwa wanafunzi ambapo uzinduzi ulifanyika Chuo cha Ualimu Bunda, ndani ya ukumbi mkubwa wa taasisi hii ya elimu.

Mwanakwetu alifika mapema na alipoutazama ukumbi huu kwa viti vya nyuma, ukiwa umejaa watu, ukumbini nyuma hakukuwa na soketi wala kebo ya kupachika kompyuta yake mpakato ili uzinduzi ukifika aweze kufanya kazi zake za kihabari vizuri, kebo zote zilikuwa mbele ukumbini.

Hivyo basi Mwanakwetu alifika mpaka ofisi ya utawala wa chuo hiki, mara nyingi yupo karani wa Mkuu wa Chuo, binti mmoja muungwana sana, siku hii hakumuona binti huyu. Mwanakwetu alikuwa mnyonge sana, hivyo basi alikwenda ofisi ya pili na kuchungulia, kulikuwa na mama mmoja mweusi aliyevaa miwani, hapa Mwanakwetu alihofia miwani ya mama huyu, kisha Mwanakwetu akapita kando, kimya kimya na kwenda chumba kingine ambacho kilikuwa kompyuta tele, hapa alikutana na kijana mmoja mrefu machachari sana na kumueleza shida yake:

“Ndugu mimi natoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, nipo hapa tunamgoja Mkuu wa Mkoa aje, sasa naomba kukaa sehemu kwenye chumba jirani na ukumbi, chenye kebo na soketi iliniweze kufanya kazi zangu za kihabari vizuri, maana hapa spika zinasikika vizuri kama nipo ukumbini, wakati kiongozi anaongea, maana ukumbini kwa nyuma hakuna soketi wala kebo.”

Ndugu huyu alijibu kwa haraka mtafute mwalimu wa zamu akimaanisha mkufunzi wa zamu, kisha jamaa huyu akaenda zake.

Mwanakwetu alikaa hapo mkiwa kwa sekunde kadhaa, kisha akamuona mama mmoja na bintiye wanatoka katika chumba kile cha mama mwenye miwani ambapo Mwanakwetu awali alihofia kuingia.

 

Mama huyu anaongea na binti yake maneno haya:

“Huyu mwalimu mwenye miwani amekushauri vizuri binti yangu, wewe nenda tu ukarudie kusoma masomo hayo katika vituo hivyo alivyokwambia ili upate sifa za kupata nafasi ,iwe ya Chuo Kikuu au kusoma Vyuo vya Kati…mwanangu mambo ya wanaume achana nayo… si umeyaona yalivyokuyumbisha….”

Mama huyu na biniiye wanatoka huku wanaongea, wanakwenda kuelekea geti la kutoka nje na Chuo cha Ualimu Bunda kinachotoa Stashahada ya Ualimu kwa masomo ya Sayansi ya Jamii

Kumbuka hapa Mwanakwetu yu njia panda anajiuliza juu ya mwalimu wa zamu atampataje? Hapa ni mbele ya Ofisi ya Mkuu wa Chuo cha Ualimu Bunda? Karani aliyemzoea hayupo, maana hapa Chuo cha Ualimu Bunda Mkuu wa Mkoa wa Mara mara nyingi hufika kufanya vikao kadhaa vya kiserikali.

Mwanakwetu akwa anatafakari yake alijua kuwa huyu mtaalamu wa Kompyuta wa Chuo cha Ualimu Bunda siyo mjuzi wa misamiati ya Vyuo vya Ualimu maana matumizi ya misamiati ya Vyuo vya Ualimu vya Tanzania hayafahamu, hasa hili linaonekana namna alivyokuwa anajenga sentensi zake:

“Msubiri Mwalimu wa Zamu…”

Msomaji wangu katika Vyuo vya Ualimu kuna Wakufunzi hapa kuna Mkufunzi wa Zamu ambaye yeye ndiye anayewafundisha wakurufunzi ambao ndiyo wanafunzi wa mafunzo ya Ualimu. Kisha wale wakurufunzi wa ualimu wao ndiyo wanakuwa walimu wa zamu na hapa anakuwepo msichana na mvulana hapa wanajifunza namna wakiwa walimu majukumu ya mwalimu yanakuwa yepi mathani kuandika ripoti ya siku na kusimamia kazi zote za shuleni na hata kuwapokea wageni kuandika ripoti katika Log Book na Black Book.

Msomaji wangu tambua na hili:

“Siku hii hata Log Book ya Chuo cha Ualimu Bunda, kama walikuwa makini lazima Mkufunzi wa Zamu aliandika katika ripoti yake kuwa chuoni hapo kulikuwa na ugeni mkubwa wa Mkuu wa Mkoa wa Mara na alifika hapa kuzindua umezeshaji wa dawa za kichocho na minyoo.”

Ndugu huyu alikuwa anamaanisha, Mwanakwetu amgoje Mkufunzi wa zamu…sasa hapa Mwanakwetu mgeni hamjui mkufunzi wa zamu anafanyaje?

Mwanakwetu akawa anataka kwenda kwa yule mama mwenye miwani ambaye ofisi yake ipo katikati ya chumba cha kompyuta na Ofisi ya Mkuu wa Chuo lakini anasita, tamaa ya kwenda kumueleza shida yake ipo, lakini bado moyo unasita, kisha Mwanakwetu akakata shauri na akarudi kwa jamaa machachari wa kompyuta na kusema maneno haya.

“Ndugu! Sikiliza, mimi hapa ni mgeni, nitamjua wapi huyo mwalimu wa zamu? Kwangu mimi sasa hivi, wewe ndiyo mwalimu wa zamu. Sikiliza, naomba nitafutie pahala nifanye kazi hii ya umma…”

Mwanakwetu haya matukio ni ya ndani dakika 3 mpaka 5 na wakati huo Mkuu wa Mkoa wa Mara hajafika bado kufanya uzinduzi wa umezeshaji wa dawa za kichocho na minyoo.

Jamaa machachari akamchukua mzegamzega Mwanakwetu na kumtafutia pahala pazuri pa kukaa ambapo ilikuwa ni ofisi ile ya mama mweusi mwenye miwani ambapo katika ofisi hii kulikuwa na meza mbili.

Kweli Mkuu wa Mkoa wa Mara alifika, alifanya uzinduzi huo huku Mwanakwetu alifanya kazi hii ya kihabari vizuri sana na mwishoni alimuuliza jina huyu mama mweusi mwenye miwani na yeye alijibu:

“Mimi naitwa Mary Machogu ni Mwadili wa Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Bunda, cheo hiki kwa miundo ya sasa kinaitwa Mratibu wa Masuala ya Wanachuo… Karibu sana Chuo cha Ualimu Bunda, mlete mwanao na hata ndugu yako asome ualimu chuo petu.”

Baadaye Mwanakwetu alimpiga picha huyu Mratibu wa Masuala ya Wanachuo kisha Mwanakwetu kurudi zake Musoma Mjini.

 

Katika makala hayo ya siku hii ya Mkuu wa Mkoa, Bi Machogu alikuwemo hasa juu ya kozi za ualimu zinazotolewa chuoni hapa. Siku chache baadaye Mwanakwetu aliichukua picha ya Bi Mary Machogu na kuiweka katika mitandao yake ya kijami, huku Mwanakwetu akivutiwa sana na yale maelezo ya yule mama pale nje baada ya kutoka kwa Bi Machogu juu ya bintiye alivyoshauriwa arudie masomo yake aliyofeli, kumbuka wakati Mwanakwetu yupo nje akitafuta pa kukaa.

Picha hizi ya Bi Machogu akiwa ofisini kwake zilipendwa na watu zaii ya100 kulikuwa na maoni zaidu ya 100 na huku zikinakiliwa na watu kadhaa.

Watu maarufu waliyotoa maoni yao katika picha hii walikuwa kumi, kati ya hao nakutajia wawili tu wa kwanza ni Msomi wa Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam Dkt. Gilman Nyamumbi ambaye aliwahi kumfundisha Mwanakwetu wakati akisoma Shahada ya kwanza ya Sanaa ya Habari, hapa Dkt. Nyamubi yeye alitaka kujua :

“Huyu ni Mwadili wa Wanafunzi au Mwadili wa Chuo cha Ualimu Bunda?”

Hapa Mwanakwetu alilijibu swali hilo.

 

Mtu wa pili aliyechangia maoni yake alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mh. Antony Mtaka yeye alisema haya:

“Mwanakwetu! Unapoona meza ya mwadili wa wanafunzi imejaa vitabu vikubwa vikubwa, kama hivyo kama hapo, tambua kuwa mwadilili ni mkali sana… nitamtafutia kompyuta mpakato mwadili wetu ili nimpe… nitamfikishia laptop yake wakati nakwenda kwetu Suguti.”

Picha hii ya Mary Machogu ilileta mijadala kadhaa ikiwamo je Chuo cha ualimu ni vizuri kiwe na mwadili mwanamke au mwanaume? Katika hili wapo walikataa chuo kuwa na mwadili mwanamke na wapo waliopinga chuo kuwa na mwadili mwanaume. Huku wachangiaji hawa hawakujua kuwa kama chuo kina Mwadili Mkuu mwanamke basi msaidizi wake ni mwanaume na kama mwadili ni mwanaume basi msaidizi wake lazima awe mwanamke.

 

Mijadala ilikuwa mikubwa sana, huku wengine wakimpigia simu Mwanakwetu juu ya picha hii.

Katika haya yote aliyewavunja mbavu wachangiaji wote alikuwa ni Bundala Juma Bundala yeye aliyasema haya:

“Kama kuna mtu anajua siri za wanachuo basi dean of students mezani kwake kuna watu wametapeliwa na wapenzi wao, kuna wadada wametoa ujauzito wakapata changamoto za kiafya, kuna watu wanakopana pesa na wanasumbuana kulipa…”

Msomaji wangu kumbuka haya yote yanayojengwa ni juu ya Bi Mary Machogu Mwadili wa Wanachuo wa Chuo cha Ualimu Bunda Mkoani Mara ambapo Mwanakwetu alifahamiana naye katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Maea mapema mwaka wa 2026.

 

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Msomaji wangu siku ya leo nilitamani uyajue haya ambayo niliyaokota katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Februari 2026 pale Chuo cha Ualimu Bunda hadi nakutana na Bi Mary Machogu ambaye ni Mratibu wa Masuala ya Wanachuo wa Chuo cha Ualimu Bunda nikijifunza namna anavyofanya kazi vizuri ya kuwasaidia, kuwalea na kuwashauri vijana wetu chuoni hapo. Kizuri zaidi hata kila anayefika ofisini kwake anapokelewa vizuri na kutoa ushauri hata kwa wazazi ambao watoto wao hawasomi katika chuo hiki.Haya ndiyo majukumu ya mkufunzi, mwalimu na mhadhiri wa taasisi yoyote ya elimu.




 

Kizuri zaidi picha ya Bi Mary Machogu ikiibua mjadala hadi Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mheshimwa Antony Mtaka akimtunuku Kompyuta Mpakato Bi Mary Machogu. Mwanakwetu anasema Mh Antony Mtaka siku utakapokabidhi kifaa hicho nilijulishe nishuhudie. Hata kama mie sitakuwepo hakikisha wanahabari wanashuhudia tukio hili la kiungwana namna Mkuu wa Mkoa wa Njombe unavyovuka mipaka wa kitendaji ya ofisi yako. Hongera sana Antony Mtaka.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka:

“Unamjua Bi Mary Machogu Mwadili wa Wanachuo Chuo cha Ualimu Bunda?”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257











0/Post a Comment/Comments