
Adeladius Makwega-MBAGALA.
Makabila ya Wazaramo na Wandengereko ni makabila ambayo kwa asili yanaamini mno katika ushirikina, kama yalivyo makabila mengi ya Afrika Mashariki ambapo ushirikina ni sehemu ya maisha ya jamii husika, huku hakuna kinachoweza kufanyika hadi kupigwa ramli wenyewe wanaita kupiga bao.
“Mtu hawezi kufanya safari hadi apinge ramli, mtu hawezi kulima shamba hadi apige ramli, mtu aweze kutafuta mke lazima ramli ipigwe… kikundi cha ngoma hakiweza kwenda ngomani lazima ramli ipigwe na hata watoto hawawezi kupelekwa jandoni hadi ramli kupigwa, hata binti mwali hawezi kutolewa nje lazima ramli ipigwe maana ramli ndiyo mwongozo na huku mpiga ramli yupo bize na kazi hiyo mwaka mzima.”
Siku ya leo msomaji wangu nakuomba nikusimulie visa vitatu vya kweli ambavyo vilitokea Kijijini Mkuranga Wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani miaka 1980 na nadhani baadhi ya wahusika inawezekana bado wapo hai na umri wao unalingana na rika za Mwanakwetu.
Kwa desturi shule za Msingi nchini Tanzania kwa miaka mingi hufungwa kwa juma moja miezi ya karibu na Pasaka ya kila mwaka. Hali hii ndiyo ilivyokuwa siku hizo hapa Shule ya Msingi Mkuranga ilikuwa ni siku ya kufunga shule, hivyo wanafunzi wote toka darasa la kwanza hadi la saba walifika shuleni, wakafanya shughuli zao kadhaa vizuri. Kama ilivyo desturi mwanafunzi ambaye anaaminika sana hupewa jukumu la kufagia ofisi ya walimu na hata Ofisi ya Mwalimu Mkuu. Binti mfagizi wa ofisi ya walimu asubuhi hii alifika na kuifungua na kuanza usafi ofisi hii ya umma, huku Mwanakwetu yeye anafagia mraba wale aliyopangiwa nyuma ya darasa lake.
“Kwa hakika ndugu yetu Mwanakwetu japokuwa alikuwa mtoto wa mwalimu lakini hakupata bahati ya kuwa mfagizi wa ofisi ya walimu, kuwa mfagizi wa ofisi ya walimu kuna posho kadhaa hawezi kununua madaftari na peni lakini bahati ya mwenzio usiilalie mlango wazi.”
Ili kuingia ofisni kwa Mwalimu Mkuu ilibidi huingie kwanza ofisi ya walimu wote. Binti huyu alipoingia akaanza usafi na aliposogea upande wa dirisha la Mwalimu Mkuu pembeni akakutana na nyoka mfu, binti akapiga yowe…
“Ahmad ! Nyoka,Nyoka, Masaafu na Mtume Nyoka, Nyoka.”
Binti akakimbilia kwa Kaka Mkuu akaeleza kilichotoke, kisha akaambatana naye hadi ofisini kwa Mkuu wa Shule, hapa likachukuliwa jembe kumchukua nyoka huyu mfu kwanza wakamkata kichwa kisha kumchimbia shimo na kumfukia jirani na shimo la takataka nyuma ya ofisi hii. Zoezi la usafi likafanyika ofisini na shule nzima vizuri kisha alipokuja mwalimu wa zamu akaelezwa kilichotokea.
Shuleni kukawa na hoja tele, nyoka hawezi kutambaa sakafuni huyu ni nyoka wa namna gani?Kwanini akutwe amekufa? Wanafunzi wakakaa mstarini kisha kuingia madarasani, huku simulizi ya tukio la kukutwa kwa nyoka mfu ofisini kwa Mkuu wa Shule likijadiliwa.
Kwa desturi siku ya kufungwa shule hasa likizo fupi huwa ni siku ya kuwagawia wanafunzi karatasi za mitihani tu maana likizo fupi hakuna haja ya kuwataja nani kawa wangapi bali hilo ni kwa likizo ndefu ile ya mwezi wa sita na ile ya Disemba . Muda wa kufunga shule ulifika, kengele ikagongwa na hakukuwa na haja ya kukaa chini ya mti wenye kizuli bali kusimama hapo hapo mstarini .
Wakati kengele inagongwa wanafunzi wakawa mbio kila mmoja anakimbilia pahala darasa lake linaposimama, kijana mmoja mdogo akagongana kichwa na mwenzake damu zikawa zinawatoka, wakabebwa haraka haraka hadi Zahanati ya Kijiji cha Mkuranga ambayo ilikuwepo pale ilipo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga kwa sasa, hapa wakatibiwa na huku nyuma mstarini shule ikafungwa na tarehe za kufunguliwa kutajwa.
Wanafunzi wakarudi nyumbani kibindoni kila mwanafunzi anasimulizi mbili:
“Nyoka kukutwa Ofisini kwa Mkuu wa Shule na ya pili watoto wawili kugongana vichwa na kupasuka wakati wanakimbilia mstarini ikiaminika kuwa hapa shuleni kuna JINI linalokunywa damu za binadamu hivyo jinni hili lina kiu sana.”
Likizo kila mtoto yu nyumbani kwake na wale Wakristo ndiyo juma la likizo lilikuwa na Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, Jumamosi Kuu, Pasaka na Jumatatu ya Pasaka. Shule ilifugulikwa salama na baada ya likizo ila mmoja akimuuliza mwenzake yu wapi?
Kijana mmoja wa darasa la tano yeye alipokuwa likizo alitumwa na wazazi wake shambani, akalima huku wakati anarudi akawa anaokota kuni kijana huyu mtiifu kwa wazazi wake akagonga na nyoka, akakimbizwa zahanati na hali ilikuwa mbaya, akabebwa hadi Hospitali ya Temeke hali iilikuwa tete na inasemekana mguu ukawa unaoza , huku ukitoka wadudu, hivyo madakatri wakaamua kijana huyu akatwe mguu mara moja. Wakati shule inafunguliwa kijana huyu amekatwa mguu na amelezwa Temeke Hospitali na wale wanaokaa nae jirani na kwao na ndugu huyu wakawa wanasimulia kilichotokea kwa wenzao. Baadaye huyu kijana kidonda cha kukatwa miguu kilipona na kurudi shuleni huku sasa akitembea na mguu mmoja na akisaidiwa na magongo.
Hapa sasa Shule ya Msingi Mkuranga wanafunzi wana simulizi nyingine mpya ya huyu kijana aliyegongwa na nyoka na kukatwa mguu, shule imezizima juu ya majini yanayotaka kunywa damu za binadamu
Simulizi shuleni zikawa tele:
“Hapa tulianza na nyoka yule ndani ya Ofisi ya Mkuu wa Shule, baadaye wale watoto waliopigana dafrao mstarini kisha tatu huyu mwenzetu aliyekatwa mguu na jambo hili lilikuwa kubwa sana, Mungu bahati lilitaka kuingia katika familia kubwa, familia ile ina zindiko kubwa na ndiyo maana huyu jamaa kakatwa mguu, ingekuwa familia nyingine ndogo ndogo saa hizi tungeshazika. Unajua Damu huwa inaanza kidogo kidogo, ngazi kwa ngazi na mwisho inapiga kule juu zaidi.”
Hawa wanafunzi wanaongea, kisha simulizi hizi zinarudi hadi majumbani kwa wazazi wanasimuliwa.
Msomaji wangu, haya ni Shule ya Msingi Mkuranga ambapo Mwanakwetu alikuwa mwanafunzi wa shule hii kwa darasa la pili hadi la tano na leo hii ameikumbuka na pia amemkumbuka huyu jamaa aliyekatwa Mguu yu hai hadi kesho na sasa anajukuu. Mwanakwetu aliamua kuiweka hii simulizi katika maandishi ili wale ambao hawakuwepo wajifunze namna mambo yalivyokuwa na jamii ya Wazaramo na Wandengereko wa Mkuranga namna wanavyoamini.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Katika makala haya kuna maelezo haya:
“Damu huwa inaanza kidogo kidogo, ngazi kwa ngazi na mwisho inapiga kule juu zaidi…”
Hawa ni Waafrika namna wanavyoamini na kuhofiwa kumwaga damu hovyo hata ya mnyama huwa wanaamini ina madhara makubwa kwa binadamu . Simulizi hii ni kitoto ambayo Mwanakwetu kama alivyosema ameikumbuka tu. Mwanakwetu hana hakika kama nduguze Wazaramo na Wandengereko wa Mkuranga bado wanaamini haya. Swali la kujiuliza ni moja tu je unajifunza nini katika simulizi hii?
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Umwangaji Damu Huwa Ngazi Kwa Ngazi.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257



.gif)
.gif)
Post a Comment