Udikteta Hauna Jinsia

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Siku ya leo msomaji wa Mwanakwetu tambua kuwa ndugu yetu anaamua kuzifunga makala zile za lile jina Sege Igenge lililotajwa katika matukio mawili yanayodaiwa kufeli ambalo wahuni wanaokaribia 15 inadaiwa walitaka kumteka Kanali Augustino Polepole ambaye ni kaka wa Humphrey Polepole huko Swedeni.

Kulingana na taarifa zinazozunguka mitandaoni ambazo zilipazwa sauti yake na Recho Dangwa zilidai kuwa genge hilo linaloongozwa na mwanamke anayeitwa Sega Igenge ambapo Bi Recho Dangwa awali alidhani kuwa jina hili lilikuwa la bandia ambapo Mwanakwetu katika makala zake kadhaa alitoa ushahidi kuwa Sega Igenge ni jina la mtu ambaye yupo huku Mwanakwetu akirejea visa kadhaa vyake na Sega Igenge Chuo Kikuu na nyaraka ya ushahidi iliyokuwa utafiti wa Sega Igenge wa Shahada ya Uzamili. Recho Dangwa alidai kuwa watekaji hao waliingia Sweden huko Ulaya kama watali.

Kwa hakika suala la utekaji ni suala baya ambalo halipaswi kupigiwa makofi na ndiyo maana ndugu yetu Mwanakwetu alitumia muda wake kutayarisha makala kadhaa juu ya jina hili la Sega Igenge.

 

Katika kadhia hii ya utekaji Mwanakwetu anaamini haya:

“Watekaji hawawezi kutusumbua Watanzania kama sote tukiwa na nia moja, moyo mmoja na shabaha moja. Hivi kama mtekaji ni miongoni mwa watoto waliozaliwa na matumbo ya wanawake wa Tanzania, ati tukaishi nao vijijini/ mitaani, tukasoma nao miaka saba ya shule ya msingi na kisha kusoma nao sekondari au elimu ya kati na Chuo Kikuu kisha aote manyonyo au awe ndevu alafu aje kutusumbua!

Tumekaa naye shueni tunasaidiana ili na lile tukisaidiwa na walimu wetu hilo haliwezekani. Hapa Ashakumu si matusi inaheshimika:

’Jamani nimeona damu zinatoka ati hii nini? tunamshauri nenda kwa matroni atakuelekeza cha kufanya… anakwenda huko anaambiwa hii ni damu ya hedhi/hii ni damu ya nifasi, itakuwa inatoka kila mwezi , huu siyo ugonjwa, huku ni kuvunja ungo, hivyo damu ya nifasi ikitoka tu uwe unafanya hivi na vile…’

Ati huyu mwingine tumeona balehe yake sisi wenyewe, tumekubeba wenyewe hadi kwa ngariba Mganga wa Zahanati ya Kijiji/Mtaa au kwa Ngariba Jandoni msitu wakati wa likizo, ukakatwa govi lako na tunajua govi lako tulipolitupa, utawasumbua wengine na siyo sisi na ndiyo maana tunakwambia hadharani wala hakuna mficho. Hatutaki utekaji kama wewe hodari wa kuteka teka mama yako mzazi na baba yako mzazi uone kama watakuvika taji.”

Kwa ndugu yetu Sega Igenge jina lako limetajwa ni vizuri ukatoka huko ulipo na kujibu tuhuma hizi kama ni wewe Sega Igenge tunayekufahamu.

 

Kama wewe ni Sega Igenge tunayekufahamu naomba urejee utafiti wako wa Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara wenye jina -Uongozi wa Mabadiliko na Ubunifu:Umuhimu Husika wa Jinsia, utafiti wa mwaka 2009 katika Chuo KIkuu cha Tumaini Iringa, ukurasa wa 18 kuna pahala unasema maneno haya:“…wanawake wanapenda kutumia uongozi wa mabadiliko wakati wanaume wanapenda kutumia uongozi wa kidikteta ... wanawake wanapanda ngazi vizuri na wanafanya kazi kwa ushirika..

 

.”Haya ni ya utafiti wako wewe mwenyewe Sega Igenge na kwa hakika mwaka huu wa 2026 Watanzania wanajua mbivu na mbichi juu ya tabia za watawala awe mwanamke na awe mwanaume. Kwa hakika ukiangalia utawala wa Rais John Pombe Magufuli Watanzania wametekwa na kuuwawa na hata utawala wa Samia Sluhu Hassani Watanzania wametekwa na kuuwawa mara dufu, kibaya zaidi Rais Samia alitakiwa kuchukua mazuri ya John Pombe Magufuli na mabaya yake kuachana nayo, likawamo hili la utekaji … huku Rais Samia alitakiwa kushughulikia yale mabaya yote ya John Pombe Magufuli ambapo Watanzania walikuwa wanalalamika mathalani kuwakamata waliomdungua risasi Tundu Lissu, lakini hilo halikufanyika kazi zaidi ya yote Tundu Lissu kusekwa mahabusu na kesi ya uhaini juu yake. 

 Katika hili Rais Samia akumbuke anayabeba mabaya yote ya John Pombe Magufuli maana Samia alikuwa Makamu wa Rais na pia Rais Samia Suluhu Hassan anayabeba na mabaya yake yote kaipindi cha utawala wake , Rais Samia hapa ana mizigo miwili, likiwamo hili la utekaji ambapo jina la mtafiti Sege Igenge nalo limeingizwa katika orodha ya kutuhumiwa katika utekaji.Kiongozi ni kiongozi tu tambua kuwa tabia za kiimla hazina jinsia na mara nyingi tabia ya kiimla mara nyingi zinatumika ili kufanikisha matakwa ya kiutawala, kwani kwenye utawala kuna nini jipya?Utawala ni jambo la muda mchache sana duniani watawala walikuwa wengi sasa hawapo.

  Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?Kwa hakika msomaji wangu shabaha ya kubwa ya makala ni kupinga utekaji, anayewatuma watekaji na vibaraka wake hakuna kuwachagulia maneno wote ni maharamia bini madharimu.

Hapa nakuomba msomaji wangu kumbuka maneno haya ya Mwanakwetu awali katika makala yake:

“…kama WATEKAJI ni miongoni mwa watoto waliozaliwa na matumbo ya wanawake wa Tanzania hii, ati tukakuwa nao vijijini / mitaani, tukasoma nao miaka saba ya shule ya msingi na kisha kusoma nao sekondari au elimu ya kati na Chuo Kikuu wewe ! Abadani hawezi kutusumbua kabisa:

’Jamani nimeona damu zinatoka ati hii nini… tunamshauri nenda kwa matroni atakuelekeza cha kufanya… anakwenda huko anaambiwa hii ni nifasi/hedhi itakuwa inatoka kila mwezi, nifasi siyo ugonjwa, huko ni kuvunja ungo, hivyo ikitoka tu uwe unafanya hivi na vile…’

Hiyo nguvu ya kutusumbua mtu kama huyu anaitoa wapi? Ha  washenzi wanaitoa wapi? Labda tuseme kuwa watekaji ni wanamgambo wa kukodi, je watawezaje kuingia nchini na kuwadhulumu Watanzania nafsi zao huku sisi Watanzania wenyewe tunawatazama? Hili haliwezekani.”

Wapo Watanzania wale wanaoamini katika ushirikina wakisema kuwa hivi kwanini hawa watu wasiojulikana hapatikani? Basi tutumie mchawi wa kuwaroga? Tuchukue damu zao za nifasi /hedhi na magovi yao tuwamalizie mbali maana wanatunyima raha katika ardhi yetu. Watu wasiojulikana tambueni Watazania wamechoka na nyinyi na ndiyo maana hadi maneno makali kama haya yanasemwa dhidi yenu.

 

 

Kwa hakiki utekaji unaaminika unafanywa na watu wasiojulikana lakini pale linapotajwa jina ambalo tunalifahamu hatuna budi kupaza sauti zetu, kwa kutumia taarifa tulizonazo katika jamii yetu maana katika maisha yetu lazima tutapata alama za maisha yao, huku anayetajwa lazima atoke na kujibu hoja kama ni yeye au siyo yeye siku la tukio hilo alikuwepo huko kufanya nini?

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Udikteta Hauna Jinsia.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257



 









 

 

 
 
 

 

 

 

 















0/Post a Comment/Comments