Same Sekondari ni miongoni mwa shule kongwe za umma nchini Tanzania, inayomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu ukoloni, huku ilikuwa shule maalumu ya kuwapokea vijana ambao walikuja kuajiliwa kama makarani katika mashamba ya mkonge.
Kwa asili shule hii ilipokea vijana wengi kutoka Mikoa wa Kilimanjaro, Tanga na hata Arusha ambapo wakati huo Manyara ilikuwa sehemu ya mkoa wa Arusha.
Kati ya mwaka 1991-1995 shule hii ilipokea wanafunzi kadhaa kutoka Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tambaza zamani H.H Agakhan Boys Secondary School kwa nyakati tofauti huu ukiwa ni mkakati wa serikali kuidhoofisha shule ya Tambaza na vituko vyake, maana kila ilipotokea migogoro wanafunzi hao waliotuhumiwa kuhusika walihamishwa kwa kutawanywa shule zingine za umma nchi nzima na kundi kubwa lilipokelewa kati ya mwaka 1993 na mwaka 1994.
Wakati huo Mkoa wa Kilimanjaro ulikuwa na Shule Binafsi tele lakini hili halikuwa hivyo kwa Wilaya ya Mwanga na Same japokuwa shule za binafsi kadhaa zilikuwepo ambazo nyingi zilikuwa mali ya taasisi za dini.
Mwanakwetu kwa anavyokumbuka pale Same Mjini hakukuwa na shule nyingine ya Sekondari ya Umma wala Binafsi zaidi ya Same Sekondari tu.
Kipindi hiki Serikali ilianzishwa shule za kutwa katika shule za bweni ilikutoa nafasi ya jamii jirani kupata nafasi ya kusoma na mwaka 1993 Same Sekondari ilipokea kidato cha kwanza kwa kutwa lakini wasichana tu na kumbuka wakati huo Same Sekondari ilikuwa ni shule ya Wavulana tangu kidato cha kwanza hadi cha sita na huku hawa wanafunzi wa kidato cha tano na sita walikuwa kwa michepuo miwili tu PCB na PCM.
Wakati wavulana wanavaa suruali ya rangi ya khaki na shati la mikono mifupi jeupe, wasichana walikuwa wakivaa shati jeupe na sketi ya rangi nyekundu isiyokoza.
Katika hili hapo Shuleni Same Mwanakwetu alikuwa ni mchezaji mzuri sana wa michezo ya kuigiza na vichekesho na haya yalikuwa yanafanywa sana na wanafunzi wawili Mwanakwetu na jamaa yake mmoja anaitwa Leonard Mgosi huyu jamaa alikuwa anatokea Lushoto.
Katika kila shughuli kubwa Mwanakwetu alikuwa lazima ataigiza, huku mtunzi hakuwa Mwanakwetu peke yake mara nyingine Mgosi.
Walimu wakaagiza lazima mshirikiane na wasichana kuigiza, maana sasa shule hii ina wasichana.
Mabinti wawili waliingizwa katika kikundi cha maigizo cha shule nao ni Siti na Doroth Mohammed.
Huyu Siti alikuwa anatokea jamii ya Waisilamu wa Same Mjini alafu huyu Doroth alikuwa anatokea jamii ya Walutheri wa Same Mjini na wakati huo kulikuwa na mgogoro mkubwa wa Kanisa la Kilutheri ukanda huu.
Shuleni hapo palikuwa na binti mmoja ambaye alikuwa anatokea vijijini sana upande ule wa Masandare alikuwa akiitwa kwa jina la utani FIDODIDO.
“Kwa wale mlikuwepo wakati huo mtakumbuka hawa jamaa wa Dare For More walikuwa na kikaragosi chao kimoja kilikuwa na jina hilo na wanafunzi wa Same walimpa jina hilo huyu binti huyu kwa kuwa alikuwa mrefu na mwembamba sana.”
Je wewe msomaji wangu unakumbuka shuleni ulipewa jina gani la utani?
Kumbuka Mwanakwetu anaelewana sana na Doroth Mohammed hata Jumapili akienda kusali pale Parokiani Jimbo Katoliki la Same akitoka alikuwa anapitia sokoni na kisha anapita nyumbani wa Doroth Mohammed ambaye alikuwa anaisha na bibi yake mzaa mama, hapa Mwanakwetu alikuwa akiongea na Doroth kisha anaagana nae kurudi shuleni.
Baadaye Doroth Mohammed aliacha shule kabisa na hakuna aliyejua kilichotokea, Mwanakwetu alikuwa mpweke. Je akienda sokoni anapita kwa nani kumsalimia wakati Same Mjini yeye ni mgeni?
“Jamani nilimpenda sana Doroth Mohammed kwa sababu kadhaa mojawapo ni kuwa jina Doroth ni jina la mama yangu mzazi , hivyo Doroth pale Same nilipokuwa naongea naye ilikuwa mithili naongea na mama yangu mzazi, hii ilikuwa siri yangu na leo siri hii naiweka hadharani kwa wewe msomaji wangu nakuomba na wewe uitunze usiumwage mtama huu kwa kuku wengi.”
Kumbuka msomaji wangu kuwa Doroth Mohammed alicha shule, huku ikidhaniwa kuwa pengine Doroth alipata ujauzito na kisha kufichwa na familia yake kusikojulikana na kuondolewa pale Same kwa siri na hakuna mtu aliyejua Doroth yu wapi.
Baadaye Mwanakwetu alikuja kumuona Doroth Kinondoni Sokoni mkabala na FM Studio ambapo mama yake alikuwa anafanya biashara hapa Sokoni.
“Swali ambalo halikujibiwa je Doroth Mohammed alipopata ujauzito alifichwa Dar es Salaam kwa mama yake?Au Bibi yake pale Same alishindwa kumtunza mjukuu huyu, hivyo mama yake akamwambia bintiye alichukue bintiye aende Dar es Salaam akafanye naye biashara?”
Maswali haya hayakujibiwa lakini baadaye Doroth Mohammed alikuwa mtumishi wa New African Hotel. Mwanakwetu alikutana na Doroth mara mbili pale kwa Mama yake dokoni jirani na FM Studio na kisha New African Hotel lakini hadi kesho hajapata bahati ya kuonana naye tena.
Nakuomba msomaji tumuache Doroth Mohammed na siri ya maisha yake, kila mmoja anayake lakini nakuomba msomaji wangu nikurudishe Same Sekondari kwa vijana wa wale wa Tambaza. Miaka ilisonga na mwaka 1995 mwenzao mmoja alibahatika kuwa Kaka Mkuu Msaidizi na kizuri zaidi hawa vijana wa Tambaza walikuwa wachangamfu kwa hiyo wasichana waliokuwa wakisoma kutwa na kurudi makwao walikuwa na ujirani sana na vijana wa Watambaza maana walikuwa na ule ujanja wa mjini kama ilivyokuwa kwa Mwanakwetu na Doroth Mohammed.
Mwezi wa tano mwishoni mwaka 1995 ikafanyika mitihani ya kufunga shule vizuri ikamaliza, jioni kama saa mbili usiku kijana mmoja wa Tambaza anayefahamika kama Lubua MUSTAPHA na siyo Mustafa na wenzake kama 60 waliongea na yule binti anayefahamika kama Fidodido jina kutoka Kikaragosi cha Dare For More kuwa kwao kuna harusi hivyo Ijumaa, Jumamosi na Jumapili usiku kutakuwa na burudani ya kukata na shoka, hivyo anawakaribisha waende katika sherehe hiyo maana dada yake anaolewa.
Katika mazungumzo yao wakasema Jumamosi kuja harusini wote hawawezi lakini watajitahidi waende Ijumaa usiku waje kufurahi na kuchangamsha sherehe maana shule imefungwa.
“Lubua Mustapha kwa sasa sina hakika alipo , baba yake alikuwa nahodha wa meli za mafuta za masafa marefu, kwa hiyo inawezekana hadi sasa Lubua Mustapha yupo huko kama Mwenyeezi Mungu bado anamjalia uhai.”
Kwa hiyo Lubua Mustapha na Fidodido wakakubaliana na kisha vijana wote waliotoka Tambaza wakaambiwa lakini Mwanakwetu wakamsahau.
Wakati wanataka kuanza safari wakabaini kuwa Makwega hayupo. Vijana hawa akiwamo Peter Mbezi wakasema Lubua Mustapha wewe unaelewana na ndugu yako Makwega kamfuate ili twende pamoja.
Lubua akamfuata Mwanakwetu na kumueleza juu safari hiyo na hapa Mwanakwetu alikuwa keshafunga begi lake ili arudi likizo nyumbani Dar es Salaaam na basi la Jumamosi. Mwanakwetu alipouliza wapi huko harusini? Alijibiwa upande wa Vijiji kando ya Masandare.
Mwanakwetu akajibu:
“Lubua Mustapha unakumbuka wakati tunahangaika ofisini kwa Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam Mwalimu Mbegu na yule karani wake mama mrembo mwenye ulemavu wa miguu? Tunakaa katika makochi tukingoja tarehe ya vikao vya kamati ya Nidhamu ya Mkoa wa Dar es Salaam? Kaka Lubua huku ni mbali na nyumbani kwetu, mimi sitaki ugomvi na watu, nataka nimalize salama nirudi zangu nyumbani salama.”
Lubua Mustapha ambaye alikuwa kijana mmoja mrefu , mweupe na ana mwili uliojengeka mchangamfu sana na kila akiongea anacheka akasema:
“Makwega unamkumbuka hadi yule karani mrembo mlemavu Ofisi ya Afisa Elimu jiji la Dar es Salaam! Makwega acha unyonge, sikiliza Makwega haya achana nayo, sisi hapa mambo ni mazuri maana hata kaka Mkuu Msaidizi anatokea Tambaza, haliwezi kutoka baya lolote kwetu, lazima tunayo ngao ya kutulinda na Nakwambia na nakiapia masaafu na mtume wote tutamaliza salama utaanza wewe kumaliza salama na kisha sisi tutamaliza salama. Kweli nakuomba twende kwenye harusi.”
Kweli Mwanakwetu akavaa sweta, makoti mazito ya baridi na kofia na usiku huo huo wakufunga safari ndefu ya mguu hadi huku vijijini mkono wa kushoto wa Shule ya Msingi Masandale, hapa akimbatana ni kikosi cha wanafunzi wenzake waliotoka Tambaza kama 60.
Kweli walipofika katika sherehe zikawa zinapigwa ngoma za asili za Wapare, huku kando kuna vikundi vya watu wanachoma nyoma.
Alitafutwa Fidodido akafika na kusalimiana na kundi hilo na alipomuona Mwanakwetu Fidodido akacheka:
“Na huyu mwana maigizo amekuja? Karibuni sana na huku ndiyo kwetu.”
Katika makazi haya kulikuwa na nyumba kadhaa za majani, hapa Fidodido akatengeneza genge la moto vijana kutoka Tambaza wakalizunguka na kati yao ikaletwa pande la nyama likawa linachomwa, huku wakila vipande vya nyama.
Wakiwa katika sherehe hii ilipofika saa sita usiku watu wakaambiwa ni muda ni chakula wakae katika makundi ya watu kama 10 , kisha ukaletwa ugali na nyama, ugali wa unga wa mahindi yalilowekwa , ugali mweupe huku mdomoni ulikuwa mchachu , watu wote walikula ugali huo kisha ngoma za asili zikapumzishwa na ukaanza muziki.
Kundi lile la vijana 60 wa Tambaza lilikuwa kubwa na ilichangamsha mno harusi hiyo usiku huu, vituko vya hapa na pale huku wakicheza muziki. Ilipofoka saa nane usiku Mwanakwetu akamwambia Lubua Mustapha ebu waambie jamaa asubuhi wengine tunasafiri turudi shuleni ili tujiandae na safari.
Kweli Lubua Mustapha aliwaita wenzake wote wakajihesabu wote 60 wamekamilika akaitwa Fidodido na kuangwa na kisha kuanza safari ya mguu mwendo saa nzima njiani, kurudi shuleni na asubuhi yake kila mmoja alipanda usafiri wake iwe trane au basi kurudi nyumbani Dar es Salaam.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Katika makala haya yenye kumbukumbu za kihistoria unaweza kupata burudani na kucheka namna maisha ya Mwanakwetu na wenzake kadhaa wakiwa vijana yalivyokuwa na vituko.
Siku ya leo nakuomba msomaji wangu weka kando vituko vyote na yakumbuke sana maneno haya ya Lubua Mustapha:
“…sikiliza Makwega haya achana nayo kabisa, sisi hapa mambo ni mazuri maana hata kaka Mkuu Msaidizi anatokea Tambaza, haliwezi kutokea baya lolote kwetu lazima Tunayo Ngao ya Kutulinda na nakwambia na nakuapia masaafu na mtume Maana Mambo Yetu Yatafanyika kwa Usalama.
Wote tutamaliza salama utaanza wewe na kisha sisi. Kweli nakuomba ondoa shaka twende kwenye harusi.”
Haya ni mwaka 1995 pale Same Sekondari vijana wa Dar es Salaam wanaongea kuwa wao wana ngao na hilo ndivyo lilivyokuwa na sote tulimaliza salama.
Je Tanzania ya mwaka wa 2021-2026 na hata Tanzania ijayo inajifunza nini katika maneno haya, hususani ukitazama hoja za watu kutekwa, hoja za watu kuumizwa, hoja za watu kulawitiwa, hoja za watu kubakwa na hoja za watu kuuwawa?
Hoja ni ile ile:
“Mambo Yetu Yatanyika kwa Usalama Maana Tunayo Ngao ya Kutulinda.”
Katika hili lazima kushughulika na watekaji na yule anayewalinda mmoja baadaye ya mwingine, mdogo hadi mkubwa ama zake ama zetu. Hapa hakuna kupepesa macho , utekaji lazima ukome na lazima Tanzania ibaki salama, iwe leo, iwe kesho au iwe kesho kutwa.
Mbaya zaidi ni huyu anayewalinda maharamia yeye ndiye haramia mkuu maana anawahakikishia usalama na ndiyo maana mambo yanaendelea.
Kwa hakika anayewalinda hawa jamaa awe Doroth Mohammed, awe Siti, awe Fidodido awe Msaidizi au Kiranja Mkuu lazima tushughulike naye.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Mambo Yetu Yatafanyika Kwa Usalama Maana Tunayo Ngao ya Kutulinda.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649247

.gif)
.gif)




.gif)
Post a Comment