Adeladius Makwega-MBAGALA
Mwanakwetu alipokuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja, mara nyingi alikuwa anawahi sana shuleni, maana alikuwa anatokea mbali huku usafiri kati ya Mbagala na Mnazi Mmoja ulikuwa mgumu.H ivyo basi alidamka mapema sana na mara nyingi akiongozwa na Doroth Mlemeta mama yake mzazi ambaye alikuwa mwalimu wa shule hii.
Ikifika saa 11.45 ya asubuhi tayari walishaingia Shule ya Wasichana Uhuru, kisha wanatembea kwa miguu hadi Barabara ya Uhuru alafu wanaingia Kongo na kisha wanapitia mlangoni wa wa kupitia Shimoni Kariakoo, hapa muda huo mara nyingi walikuta foleni kubwa ya malori ya mbogamboga, ndizi, nazi, maharage, soya, ndegu, ngano, mchele na mahindi yakiingzwa sokoni humo. Foleni ndefu huku ikisidikizwa na nzi na harufu kali ya vyakula vinavyokwenda kuingia mdomoni na kukaa tumboni mwa mwanadamu ili kumpa nguvu afanye kazi zake.
Mara nyingi Mwanakwetu aliona kuwa yale malori yaliyo mbele ili yasipoteze muda wa foleni baadhi yao yalikuwa wanashusha mizigo huku yakiwa katika foleni, bila kujali yapo umbali gani na lori la kwanza na hata sehemu ya kuhifadhi mzigo. Hapa Dereva, utingo na wapagazi walionekana kwanza kujadiliana na kisha kukubaliana kuwa sasa wanashusa huo mzigo.
Wakishakubaliana unaona mara moja wanasafisha njia ile watakayopita hadi kutua yale magunia yawe na nazi, maharage, mahindi , mchele, vitunguu na bidhaa zingine.
Wakishasafisha njia wanavua nguo zao, walizotoka nazo nyumbani hadi viatu kisha wanavaa kaptura za kazi, mili yao ikiwa na malaika, masharafa na vinyoleo tele mithili ya nyani mkubwa katika mbuga ya Serengeti, kisha wanaanza kushusha mizigo hiyo hadi inakamilika na wakimaliza mwenye mzigo anawalipa wapagazi pesa yao na Lori linaondoka katika foleni na kurudi mitaani kusaka mizigo ya kurudi nayo iwe Lushoto, Njombe, Songea, Iringa, Makambako, Mahenge, Shinyanga, Tabora au Mwanza.
Kipindi hiki Mwanakwetu ni mdogo na mara nyingi aliambatana na mama yake maana Dar es Salaam ukabaji ulikuwa nje nje. Mwanakwetu anakumbuka hili:
“Kipindi hiki mara nyingi macho yangu yalishuhudia taswira tofauti tofauti za hizi harakati Sokoni Kariakoo: Muda mwingine magunia yapo mabegani mwa wapagazi yanashushwa na kupelekwa sokoni, muda mwingine wapagazi wanalipwa pesa zao baada ya kazi, muda mwingine wapagazi wanagawana pesa huku wakisema sina chenji pesa yako nitakupa baadaye, muda mwingine wakisema kuwa mzigo huu kazi yake tumekopwa hadi jamaa auze mzigo, muda mwingine macho ya yangu yaliona wapagazi wanasafisha njia, muda mwingine lori linaingia sokoni huku wapagazi wanadandia juu kuingia ulipo mzigo. Maneno kama haya yakisikika: Hii ni mali ya Shinyanga, Haya maharege ya Mbeya Maji na Kuni Mara Moja, Huu ni mchele mpya…”
Mwanakwetu anapita zake kwa kando huku akikabiliana na ukali wa mama yake:
“Wewe acha kushangaashangaa! Mwanangu unashanga nini?
Kashangae feri, meli inaelea huku shilingi inazama,
angalia mbao hizo, misumari na vitu vyenye ncha kali pembeni viliyotupwa kando na wapagazi wakati wanasafisha njia yao ! Utapamiwa na hao wapagazi, ongeza mwendo tuwahi shuleni.”
Mwanakwetu anaongeza mwendo na anaepusha kushangaashangaa na anawahi zake shuleni.Msomaji wangu haya ni ya mwaka wa 1987 jijini Dar es Salaam, huku Mwanakwetu akiwa kijana mdogo.Kwanini siku ya leo Mwanakwetu amekumbuka kisa hiki cha miaka tele nyuma cha pale Sokoni Kariakoo?
Mwanakwetu anailinganisha Tanzania ya leo na mzigo ndani ya lori hapa Sokoni Kariakoo ambapo malori kadhaa yanashusha mizigo huku mpagazi wa mizigo hiyo Mwanakwetu anamlinganisha na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye jukumu lake ni kuhakikisha lori letu linashusha mizigo salama ili iweze kuwafikia wateja ambapo ni mimi ,wewe na yule na tule ili tupate uhai. Mwanakwetu anavyomtazama Rais Samia ni kweli yu kando ya lori na anashusha mizigo hii, huku akiipenda kazi yake vizuri ya upagazi. Mwanakwetu anapomtazama kiongozi huyu anaona kuwa changamoto kubwa ni namna anavyoifanya kazi hii ya upagazi, hilo ndiyo tatizo.
Wenye Lori wamemuamini na kumpa mzigo aushushe lakini anaushusha mzigo huo huku akiwa amevaa viatu vya mchuchumio, huku njia hii hakuifanyia usafi kabla huku njia hii ina misumaria kadhaa na vitu tele vyenye ncha kali ambapo kuweza kutembea tu bila mzigo ni kazi vipi anapotembea na mizigo begani na viatu vya mchuchumio, je ataweza kuufikisha salama mzigo wetu bila ya kupiga dafrao?
Kwa hakika mzigo huu ni mzito mno tangu yale ya Rais John Magufuli maana kifo chake kimeacha yake na mzigo wake ulibaki ambapo Rais Samia alitakiwa kuhakisha kwanza anaumaliza kuushusha mzigo wa Magufuli wote na ndipo angeanza kushusha mzigo mpya.
Kwa hili msomaji wangu naomba nitoe mfao mdogo sana:
“Ukanda wa Pwani ya Tanzania unalalamika sana kuwa ndugu zao wengi wamepotea na hawajulikani walipo, mpaka sasa hakuna majibu baadhi ya familia wanawake walikaa eda hadi wakaolewa na wanaume wengine bila ya kujua mume wao kipi kilimkuta. Hapa rejea familia ya Minangu pale Mbagala Sabasaba,
haya ya kipindi cha Rais John Magufuli, jamii haijua mtu wao yu wapi wala maiti yake. Haya ni ya Ukanda wa Pwani ya Tanzania . Mara zote Rais kutoka Zanzibar watu wa ukanda wa Pwani huwa hauna maneno naye maana ni sehemu ya ndugu yao, jamii ya Pwani iliamini ujio wa Rais Samia angelishungulikia hili na ukanda huu ukapata majibu na akijumuisha kuyafanyia kazi na yale mengine ya maeneo mengine ya Tanzania watu waliopotea au kuuwawa na hata waliopigwa risasi na Mungu kuwajalia uhai na waliofanya haya wangejulikana na sheria ingefuata mkondo wake, hili linaonekana wazi Rais Samia Mungu hakumjalia kuliona na wala kulifanyia kazi kabisa.
Rais Samia angejaliwa kuliona hili na kulifanyia kazi angesafisha njia yake na neema zingemtembelea na huku angefuta machozi ya Watanzania hawa wanyonge.
Sasa hili halikufanyika bado Tanzania ina mzigo wa yale ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ambayo haya ni ya Rais Samia mwenyewe. Je atawezaje kuishusha mzigo hiyo katika mabega yake ndani ya lori huku njia ikiwa haijasafishwa?
Watu wa Pwani na watu wa Zanzibar ni ndugu, miaka mingi , siyo leo , siyo jana na siyo juzi na siyo kwa sababu ya Uisilamu.
Maana hii dini imekuta watu wanaishi. Katika hili nitoe kisa cha Mzanzibari Mkristo marehemu Balozi Isack Sepetu kuna siku alifika Kibaha nadhani kaika uchaguzi wa mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, wajumbe walikuwa na furaha sana namna Balozi Sepetu alivyosimamia uchaguzi huu na hata namna alivyokuwa anaongea maana waliona ni mithili ya ndugu yao akiongea nao kikaoni.”
Hizi ni jamii ndugu mbona Rais Samia anawaacha njia panda?
Msomaji wangu kumbuka katika kisa hiki cha wapagazi pale Sokoni Kariakao nafuu ilikuwa kwa wale wapagazi wa Sokoni Kariakoo walivyofanya usafi wa njia yao kwanza, huku zile mbao na misumari na vitu vyenye ncha kali waliviweka kando.
Rejea maneno ya Mwalimu Doroth Mlemeta kwa mwanae:
“Wewe acha kushangashanga! Mwanangu unashanga nini?Kashangae feri meli inaelea huku shilingi inazama,
angalia mbao hizo, misumari na vitu vyenye ncha kali pembeni viliyotupwa kando na wapagazi wakati wanasafisha njia yao ! Utapamiwa na hao wapagazi, ongeza mwendo tuwahi shuleni.”
Leo hii kuna mbiu ya Katiba Mpya , sawa, unaweza kusema Katiba Mpya ndiyo, huyo anayepiga zumari la Katiba Mpya watu wanamtuhumu akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya juu ya Shedrak Chaula na Mdude Nyagachi walipotea. Mpaka leo hii hana majibu. Kama mtu ameshindwa kumlinda binadamu mwenzake hadi anapotea yeye akiwa Mkuu wa Mkoa anawezaje kusaidia maandishi ya kuliongoza taifa kukaa vizuri na kuepusha mgogoro?
Hayasemwi haya kisa majina yenu ni mazuri sana la hasha bali kwanza mnalipwa mishahara ya umma ya kodi za Watanzania na pili lazima mjue tatizo siyo katiba Mpya tu, tatizo linawezekana hata hao wanaotakiwa kutuongoza kuelekea huko.
“Watu kama hawamtaki mpishi, ukalazimisha apike mpishi huyu huyu , hata kama chakula kinachopikwa, kikapikika kweli kweli, akaweka kila kiungo watu watakwenda meseni kula lakini nakwambia chakula hiki hakiwezi kupita kooni maana watatapika.”
Jiulize mtu huyu huyu anaongea na jamii juu ya KATIBA MPYA jamii inadai Mdude Nyagachi na Shedrack Chaula wapo wapi? Unaweza kusema Katiba Mpya watu wakakwambia Oktoba 29, 2025 Unajibu nini?Unasema Katiba Mpya watu wanakwambia Tundu Lissu , unasema Katiba Mpya Watu watakuuleza Humphrey Polepole yupo wapi? Je unawakamata na kufunga watu kama hawa?Kumbuka hawa ndiyo wanaokulipa mshahara wako wewe kukalia kiti hicho. Hapa msomaji wangu utabaini kuwa staili ya uongozi badala ya kupunguzamalalamiko kwa jamii inayoiongoza inaongeza malalamiko mapya kila uchao na hapa hata kipi cha kufanya kinajionesha.
Katika mazingira kama haya unaweza kushusha tenga la nyanya mbivu!
Mwanakwetu upo?Kumbua:
“Tunashusha Tenga la Nyanya Mbivu Katika Mazingira Kama Haya !”
Nakutakia Siku Njema
0717649257







.gif)
.gif)
Post a Comment