.gif)
Ni majira ya asubuhi ya Machi 15, 2026 Mwanakwetu anakwenda kusali dominika katika Kanisa Dogo la Warosimini Lushoto Mjini, Parokia ya Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga nchini Tanzania.
Huku akielekea katika misa hii ya inayoanza saa 1.30 asubuhi ya kila Jumapili, hali ya hewa ya mji huu uliyo Kaskazini Mashariki mwa taifa hili la Afrika Mashariki ilikuwa ya nyuzi joto 21, ujirani na mvua ni wa asilimia 84 na unyevunyevu ni wa asilimia 30 na upepo ukivuma kwa KM 3 kwa saa .
Ibada hii ya misa ilikuwa ya Wanovisi karibu 22, watawa wa kike watatu, waamini wengine wawili na Padri anayeongoza mmoja, aliyetambuliwa kuwa ni Padri Thomas Akello.
Misa hii ilianza huku masomo yote matatu yalisomwa kwa ustadi mkubwa na huku wimbo wa katikati ukiwa Zaburi ya 23, baadaye Padri Akello alianza mahubiri na kwanza aliipiga mbiu ya mgambo yake kwa kutoa chagizo kwa waamini wake kuwa:
“Kwa sababu hatuimbi haleyuya kama tunapungikiwa vile? Na hatuna mbadala? Kama ni hivyo sasa leo hii mimi nawapa mbadala-mnaujua huu wimbo?
‘Neno Hili Ndugu, Neno La Wakovu- Tena Jema, Neno Neno Hili Ndugu Lakuita Wewe Neno La Wakovu Tena Jema.
Siku zinapita Fikiria Mwezangu…. Zinapita Neno, Neno Hili Ndugu Lakuita Wewe Neno la Wakovu Tena Jema…’”
Padri Akello alipomaliza kuimba wimbo huu ambao ni miongoni mwa nyimbo za zamani za Kanisa aliingia katika kiini cha mahubiri yake ya dominika ya Nne ya Kwaresma kwa kusema kuwa wakati wa Kwaresma ni wasaa wa Mkristo kujisomea sana mafundisho ya Ukristo maana mara baada ya kubatizwa ili tuweze kuelewa imani yetu, tunarudia ahadi za Ubatizo, huku sote tumezalia kama vipofu na ndiyo maana tunapojadili juu ya Kristo tunajadili juu ya Mwanga.
“Tunapokaribia Pasaka tunausogelea Mwanga ambaye ndiyo Kristo.”
Padri Akello alisema kuwa maisha ya mwanadamu yana changamoto tele lakini shabaha ya changamoto hizo ni moja :
“Mateso yana sifa ya utakaso, hili Kristo adhihirishwe na huku dhambi zituongoze katika maungamo wakati kwa mnovise anatakiwa kuungama kila mwezi huku sheria za Kanisa kila Mkristo anatakiwa kuungama angalau kwa mwaka mara moja.”
Sambamba na hili Mwanakwetu alipotoka kanisani alisikiliza mahubiri ya Luis Kadinali Tagle ambaye ndiye Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki Ulimwengu inayoshughulika na Uinjilishaji wa Watu, yeye aliyasema haya:
“Tuko katika Jumapili ya nne ya Kwaresima, na Injili ya leo inasimulia hadithi inayojulikana ya Yesu kumponya mtu aliyekuwa kipofu tangu kuzaliwa kwake. Yesu alipomponya mtu huyo, wanafunzi wake wakamuuliza:
‘Rabi, ni nani aliyetenda dhambi—mtu huyu au wazazi wake—hata akazaliwa kipofu?’
Yesu akawaambia: Si yeye wala wazazi wake. Lakini kupitia kwake nguvu ya Mungu itaonekana.
Kisha akatengeneza tope, akalipaka kwenye macho ya yule mtu, na akamwambia aende akaoge katika bwawa la Siloamu. Uponyaji wa mtu huyo ulileta miitikio mbalimbali.
Majirani zake walishangaa lakini wakaanza kuwa na hamu ya kujua kuhusu Yesu. Mafarisayo walimuhoji yule mtu kisha wazazi wake. Na tazama, ndugu zangu, yule mtu ambaye sasa anaweza kuona lakini anadhihakiwa na Wayahudi, ndiye anayewafundisha wataalamu wa Sheria kuhusu Mungu. Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watenda dhambi. Lakini mtu akiwa mcha Mungu na akifanya mapenzi yake, Mungu humsikiliza. Haijawahi kusikika kwamba mtu yeyote aliwahi kufungua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu. Kama mtu huyu asingetoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote.
Tunaitikiaje kazi ya Mungu inayojidhihirisha kupitia watu wa kawaida na wanaoonekana wasio muhimu? Je, tunaipuuza au tunaikaribisha? Je, tunaamini kwamba Mungu anaweza kujifunua kupitia watu na mazingira tusiyotarajia?
Utukufu wa Mungu ulidhihirika kweli kupitia yule aliyekuwa kipofu hapo awali, kwa maana ndani yake ilizaliwa imani isiyohitaji kuona kwa macho. Aliamini hata kabla ya kumwona kwa macho Mwana wa Adamu aliyemponya.”
Baada ya kumaliza kusikiliza haya mahubiri ya Kadinali Tagle ndipo Mwanakwetu akaamua kuyatayarisha makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Haya ni machache kati ya mengi ya dominika hii ambayo Mwanakwetu amejaliwa kuyakusanya, nina hakika hata wewe Mkristo mwezangu unayo kadhaa uliyoyasikia katika mahubiri ya Jumapili hii ya Machi 15, 2026. Makala haya ni sehemu tu yatafakari ya dominika hii kama alivyojaliwa kuandaa ndugu yenu Mwanakwetu.
Mwanakwetu upo ? Kumbuka:
“Tunapokaribia Pasaka Tunausogelea Mwanga ambaye Ndiye Krsto.”
Nakutaki Siku Njema.
0717649257.

.gif)






Post a Comment